Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Sunday, June 15, 2014

WAZIRI WA UCHUKUZI DK. HARISON MWAKYEMBE AZINDUA LIGI YA BODABODA MBEYA

WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe akiongea na waendesha bodaboda jiji la Mbeya  kabla ya kuzindua  ligi ya bodaboda
WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe akipiga mpira teke kuashiria kuzinduliwa kwa ligi ya bodaboda jijini Mbeya
Kabla ya uzinduzi huo wa ligi ya bodaboda kulitangulia maandamano ya waendesha bodaboda yalioanzia Kabwe mpaka kwenye viwanja vya Luanda Nzovwe
WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe ambae ndiye mgeni rasmi akipokea maandamano ya waendesha bodaboda wa jiji la Mbeya
Baadhi ya ya wazee wa jiji la Mbeya walishiriki katika uzindunzi wa bodaboda cup
WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe akimtunza fedha moja ya waimbaji waliotumbuiza katika uzinduzi wa bodaboda cup
Baadhi ya wadhamini wa bodaboda cup wakiwa makini kufuatilia matukio ya uzinduzi wa ligi hiyo
 Mmoja wa Wakurugenzi wa City sign Promotion, Geofrey Mwangunguru akisoma taarifa fupi jinsi mashindano hayo yakavyoendeshwa
Katibu wa Umoja wa waendesha boda boda Mbeya, Msenda Mdesa, akisoma Risala mbele ya Mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Waziri wa Uchukuzi Dk. Harison Mwakyembe
WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe akisalimiana na timu shiriki za ligi hiyo
WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe akiondoka uwanjani hapo mara baada ya kuzindua ligi hiyo





WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harison Mwakyembe,amezindua rasmi ligi ya mpira wa miguu itakayowashirikisha madereva wa pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda inayojulikana na Cocacola bodaboda cup 2014.

Uzinduzi huo ulifanyika jana jumamosi katika viwanja vya Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe iliyopo Ilomba jijini Mbeya ambapo zvikundi kumi vya madereva wa bodaboda vitashiriki ligi hiyo.

Akizindua ligi hiyo Mwakyembe amewataka madereva wa bodaboda kuendesha pikipiki zao kwa uangalifu na kuacha ulevi ili kupunguza ajali zisizokuwa za lazima.

Alisema waendesha boda boda wanapaswa kutumia mashindano kama njia ya kujikumbusha juu ya masuala muhimu ya usalama barabarani kwa kuepuka ulevu watumiapo vyombo hivyo huku akipongeza wadau wa michezo mkoani hapa kwa kuleta mapinduzi katika michezo nchini.

Alisema uwepo wa mikakati madhubuti baina ya wadau wa michezo mkoani Mbeya umewezesha kuibuka upya kwa amani,mshikamano na upendo baina ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya na kusababisha mshikamano wa hali ya juu tofauti na miaka kadhaa iliyopita.

Dk Mwakyembe pia aliwataka waratibu wa mashindano hayo kampuni ya City Sign Promotion and Marketing Agency kuwaalika wabunge wote wa Mkoa wa Mbeya siku ya mchezo wa fainali ili kwa pamoja waweze kujionea namna michezo ilivyowezesha watu wa makundi yote kukutana na kuzungumza mambo ya msingi wakiweka tofauti zao pembeni.

Awali mmoja wa Wakurugenzi wa City sign Promotion, Geofrey Mwangunguru alisema timu zinazoshiriki michuano hiyo zimegawanywa katika makundi mawili ya A na B ambapo kila kundi lina jumla ya timu tano na kila kundi litatoa timu mbili zitakazoingia hatua ya nusu fainali na baadaye kupatikana bingwa wa michuano.

Aidha Mwangunguru alisema dhamira ya kuanzisha ligi hiyo ni kutambua mchango wa sekta hiyo katika usafirishaji pamoja na kuwaunganisha na jamii ambayo imekuwa ikiamini kuwa kundi hilo halipaswi kuweko katika jamii.

Aliongeza kuwa kabla ya kuanzisha kwa ligi hiyo kampuni yake ilijiwekea vipaumbele vitatu ambavyo ni kuhakikisha umoja wa bodaboda unaanzisha saccoss, kujiunga na taasisi za Pensheni pamoja na kutafuta bima za afya kwa ajili ya maisha yao kutokana na ajali za mara kwa mara.

Kwa mujibu wa Mwangunguru katika kundi A zipo timu za waendesha bodaboba za Mbalizi standi Umalila,Iyunga,Shewe Sae,Kadege na Uyole wakati kundi B zipo timu za Mbalizi standi Chunya,Ilomba,Soweto,Kabwe na Mafiati.

Mwangungulu alisema bingwa wa mashindano hayo yatakayoendeshwa kwa muda wa siku 31 anatarajiwa kuzawadiwa pikipiki aina ya Boxer yenye thamani ya shilingi milioni 2.5,mshindi wa pili shilingi laki saba,mshindi wa tatu shilingi laki tatu na mfungaji bora shilingi laki moja.

Naye Katibu wa Umoja wa waendesha boda boda Mbeya, Msenda Mdesa, akisoma Risala mbele ya Mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Waziri wa Uchukuzi Dk. Harison Mwakyembe, alisema umoja huo umefanikiwa kuwaunganisha madereva wa bodaboda Mkoa mzima.

Aliongeza kuwa kutokana na umoja huo wamefanikiwa kuanzisha benki yenye wanachama 312 iliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria za uanzishwaji wa benki na kupewa Baraka zote na Benki kuu ya Tanzania.

Mwisho.

Na Mbeya yetu

No comments: