Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, May 28, 2014

UONGOZI WA KIJIJI MATATANI KWA KUFUJA FEDHA ZA MAENDELEO‏




Baadhi ya wanakijiji na Wanausalama wakifuatilia kwa Makini Kikao hicho.

*******
UONGOZI wa  Kijiji cha Ikhoho Kata ya Maendeleo Wilaya ya Mbeya unatuhumiwa kufuja fedha za michango ya maendeleo zaidi ya shilingi milioni tatu zilizochangwa na wananchi pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.
 
 
Tuhuma hizo zilitolewa jana mbele ya mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo ambao ulihudhuriwa na Polisi Tarafa,Mkaguzi wa Polisi Galusi Ligula, pamoja na  Mwenyekiti wa Kijiji aliyeondolewa madarakani, January Mwambole na Mtendaji wa Kijiji, Wakaa Nkembo.
 
 
Wakizungumza kwenye mkutano huo wananchi wamedai kuwa kwa kutumia madaraka yao viongozi hao waliwatoza wanafunzi 45 wa shule ya msingi ya kijiji hicho shilingi 525,000/- wanafunzi wakidaiwa kuvunja choo cha shule.
 
 
Walisema Wanafunzi 40 walitozwa shilingi elfu tano kila mmoja katika ofisi ya kijiji na wanafunzi watano wakilipa shilingi elfu sitini na tano katika Kituo cha Polisi cha Inyala ambapo waliwekwa mahabusu kabla ya wazazi wao kulipa pesa hizo.
 
 
Waliongeza kuwa kwa kutumia madaraka yao viongozi hao walianza kuwaandama wananchi waliokuwa wakihoji uhalali wa tozo hilo ambapo kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Bahati Kitundu alifunguliwa jalada la kutishia kufanya fujo kijijini kutokana na kuandika barua ya malalamiko kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya juu ya kero za michango mbalimbali Kijijini hapo.
 
 
Wananchi hao walisema mbali ya pesa za choo cha shule ya Msingi viongozi hao wanatuhumiwa kutafuna michango ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Ikhoho ambazo walikusanya kutoka kwa wananchi na kutoziwasilisha sehemu husika kwa muda mrefu na baadhi ya wananchi walikamatwa kwa kushindwa kutoa pesa hizo kwa wakati.
 
Aidha katika mkutano huo Jeshi la Polisi lilitumia fursa ya kutoa elimu kwa wananchi kutotumia mabavu katika shughuli za maendeleo na viongozi watimize majukumu yao.
 
 

Baada ya kumalizika kwa mkutano huo wananchi hao waliazimia kuunda tume ya watu watano kwa ajili ya kujiridhisha na tuhuma hizo kabla ya kuwasimamisha kazi viongozi wa Kijiji
Na Mbeya Yetu

No comments: