Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, May 30, 2014

HALMASHAURI YA WILAYA YA MBEYA YATOA SEMINA YA UKATILI DHIDI YA WATOTO NA JINSIA KWA WATUMISHI WAKE

 Afisa ustawi wa jamii Wilaya ya Mbeya, Magdalena Songoma akitoa mada kwenye Semina ya Watumishi na makundi maalum ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
 Washiriki wa Semina wakifuatilia kwa makini mada zinazotolewa.


 Washiriki wa semina wakijadiliana kwenye makundi.
 .Mratibu wa Ukimwi Wilaya ya Mbeya, Kelvin Kisoma akifuatilia jambo.
 Mwenyekiti wa Darasa hilo, Felix Lyaniva akisisitiza jambo kwa washiriki wa Semina.


  Wawakilishi wa makundi wakiwasilisha kazi kwa washiriki wa semina hiyo.

 Katibu wa dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi, Pudensiana Baitu akichangia mada kwenye Semina hiyo.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya kupitia kitengo cha Ukimwi na Ustawi wa Jamii imeendesha mafunzo ya Siku mbili kwa Watumishi wa Halmashauri hiyo pamoja na makundi mengine kuhusu Unyanyasaji wa kijinsia na ukatili dhidi ya Watoto vinavyochangia kuwepo kwa maambukizi mapya ya Ukimwi.
 
Mafunzo hayo yaliyoanza Mei 29 na kukamilika Mei 30, Mwaka huu yalifanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Walimu kilichopo Mbalizi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
 
Mratibu Kitengo cha Ukimwi Wilaya ya Mbeya, Kelvin Kisoma, amesema lengo la mafunzo ni kutoa elimu kwa watumishi kuanzia ngazi ya kata hadi Halmashauri ili nao wakawaelimishe watu wao juu ya ukatili wa kijinsia unavyochangia maambukizi mapya ya Ukimwi.
 
Aliwataja walengwa wa Semina hiyo kuwa ni pamoja na Viongozi wa Dini kutoka kila kata, Watu mashuhuri, viongozi wa Siasa, madiwani, maafisa maendeleo ya Jamii, Asasi zinazojishughulisha na jinsia na Ukimwi, Maafisa Tarafa, Walemavu na wakuu wa Idara za Halmashauri.
 
Aidha alisema viongozi hao wanatoka katika Kata za Utengule Usongwe, Mshewe, Tembela, Igoma, Inyala, Ilembo,Iwiji, Itewe, Bonde la Songwe,Swaya, Iyunga mapinduzi,Ihango,Ijombe, Santilya, Itawa na Nsalala.
 
Aliongeza kuwa moja ya vigezo au visababishi vya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi ni pamoja na Ubakaji, Unyanyasaji na Mafarakano katika ndoa.
 
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mbeya,Magdalena Songoma, alisema ni vema jamii ikasaidia kutoa elimu kwa wengine kuhusu kuzuia vitendo vya ukatili na sio kusubiri hadi vitendeke ndipo watoe taarifa.
 
Aliongeza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuifanya jamii ielewe juu ya visababishi vya ukatili, ukubwa wa tatizo na jinsi ya kukabiliana nalo ikiwa ni pamoja na kujua hatua za kufuata hali hiyo inapotokea.
 
Naye Katibu wa dawati la Jinsia kutoka Jeshi la Polisi, Pudensiana Baitu, alisema ndani ya kipindi cha miezi mitatu imeonekana wanaume ni wengi wanaofanya vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wa kike.
 
Alisema asilimia kubwa watoto wa kike hufanyiwa vitendo vya ukatili ambavyo ni ubakaji unaowakumba watoto wenye umri kati ya miaka 15 hadi 18 kutokana na mabadiliko ya kimwili.
 
Na Mbeya Yetu Blog.

No comments: