Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, May 28, 2014

HALMASHAURI YAFUTA USHURU WA MAZAO ILI KUONDOA MGOGORO.

 Wananchi wakifuatilia kikao cha baraza la madiwani Wilaya ya Mbarali.
 Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Modest Kilufi akichangia jambo kwenye mkutano wa Baraza.
 Baraza la Madiwani la Wilaya ya Mbarali likiendelea na kikao.
 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Kenneth Ndingo akiongoza kikao cha baraza la madiwani.
**************************
HATIMAYE Baraza la Madiwani Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya limefuta ushuru wa mazao wa shilingi elfu mbili kwa gunia uliokuwa ukitozwa kwa wakulima Wilayani humo ili kuepusha mgogoro ulokuwepo.
 
 
Kufutwa kwa ushuru huo kumekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro kupokea malalamiko kutoka kwa Wakulima wa Wilaya ya Mbarali ambao walidai kutozwa ushurukwenye mpunga ambao umevunwa kwa ajili ya chakula na siyo biashara.
 
 
Mkuu wa Mkoa aliagiza kuitishwa kwa Baraza la dharula ili kujadili mustakabali wa suala hilo, ambapo Baraza lilitii agizo na kufanya  kikao  Mei 27,mwaka huu katika ukumbi wa Maji Mbarali na kuamua kutengua ushuru huo uliokuwa umepitishwa na Madiwani hao.
 
 
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Keneth Ndingo, katika hotuba yake alisema Halmashauri inatakiwa kufikiria vyanzo vingine ili kuziba pengo hilo ambalo ni  hasara ya zaidi ya shilingi milioni 640.
 
 
Alisema  Baraza limeridhia kupunguza mawakala wa kukusanya ushuru kutoka kumi wa awali na kubakia wanne ili kuleta ufanisi wa mapato na kurahisisha udhibiti wa mapato ili kuondokana na hati chafu ya ukaguzi.
 
 
Alisema katika mpango mpya kutakuwa na kanda mbili za makusanyo ambazo ni kutoka Tarafa ya Rujewa na Tarafa ya Ilongo na kila Tarafa kutoa mawakala wawili watakaokusanya ushuru kwa ufanisi na kuboresha mapato ya Halmashauri.
 
 
Mmoja wa wakulima Christopher Uhagile aliyehudhuria kikao hicho maalumu alimpongeza mkuu wa Mkoa Abbas Kandoro kwa kuchukua hatua za haraka kuitisha Baraza hilo kwani amani ilitoweka kutokana na mkanganyiko uliojitokeza baada ya kuanza utekelezwaji wa sheria ya ukusanywaji wa ushuru kwa mkulima.
 
 
Baadhi ya Madiwani walimlalamikia Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Modestus Kilufi, kuwa kitendo cha kuhoji ushuru uliopitishwa na baraza ni usaliti.
 
Walisema  mkulima kutozwa ushuru wakati yeye ni mjumbe wa Baraza na alikuwa miongoni mwa wajumbe waliopitisha mkulima kutozwa ushuru wa mazao hivyo hakupaswa kuhoji chochote kwani kauli hiyo ni ya kuwachonganisha wakulima.
 
 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Gullam Hussein Kiffu aliwataka watendaji wote wa Halmashauri na Madiwani kushirikiana ili kukusanya mapato yatakayowezesha Halmashauri kujiendesha na kuleta maendeleo kwa wananchi.

NA MBEYA YETU

No comments: