Picha ya pamoja
MIKOA ya Nyanda za juu kusini imeonekana
kuwa bado ni kinara wa magonjwa ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi kitaifa
licha ya kuwepo kwa mikakati na kampeni nyingi za kupunguza hali hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa shughuli
za Operesheni wa PSI Kanda ya Nyanda za Juu kusini, Elia Ndutila, wakati wa
kufungua mafunzo kwa mawakala wa usambazaji wa bidhaa za afya iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya
Paradise Soweto jijini Mbeya.
Ndutila alisema sababu ya kanda hiyo
kuongoza kwa maambukizi inatokana na kuwepo kwa shughuli kubwa za kiuchumi
pamoja na mashamba makubwa yanayokusanya watu wa aina mbali mbali.
Alisema sababu nyingine ni muingiliano wa
watu kutokana na utamaduni wa watu kutoka Mikoa hiyo kufanana pamoja na uwepo
wa barabara kuu iendayo nchi jirani hivyo kusababisha wageni wengi kuingia na
kutoka kwa shughuli mbali mbali hivyo kuchangia kuwepo kwa maambukizi mapya.
Aidha akizungumzia lengo la Semina hiyo
alisema ni kujadili changamoto wanazokabiliana nazo wasambazaji wa bidhaa za
PSI katika Mikoa yao ambao wengi wao ni wamiliki wa maduka makubwa ya madawa na
mawakala wa bidaa za kawaida.
Alisema mbali na changamoto hizo pia
mawakala watajadili malengo ya Mikoa iliyojiwekea kwa ajili ya kuhakikisha
inatimiza Sifuri tatu kwa kufikisha kwenye sifuri maambukizi, Vifo na
unyanyapaa.
Kwa upande wake Mgeni rasmi katika Semina
hiyo, Dk. Sewangi, ambaye pia ni mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Mbeya aliwataka
mawakala na wadau mbali mbali kushirikiana na serikali katika kupunguza hali ya
maambukizi katika Mikoa ya Kanda ya Kusini.
Alisema malengo hayo yanaweza kufikiwa
kutokana na serikali kushirikisha Sekta binafsi (PPP) katika kufikia malengo
yaliyowekwa ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya uzazi wa mama na Mtoto.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment