Kama kawaida watoto hawakuwa nyuma kusikiliza mafunzo hayo
Shirika la Huduma Majumbani Mkoa wa
Mbeya(KIHUMBE) linalofadhiliwa na WRP Chini ya Shirika la HJFMRI la watu wa
Marekani limeendesha kampeni kwa jamii kuhusu sera zinazopinga ukatili wa
kijinsia.
Akizungumza wakati wa kufunga kampeni
hiyo Mratibu wa Mradi wa Kupinga ukatili wa kijinsia na ukatili wa Watoto
kutoka Kihumbe, Sonja Mnyani uliofanyika katika kata ya Bulyaga wilayani Rungwe
Mkoa wa Mbeya hivi karibuni alisema lengo ni kuijulisha jamii kujua sera
zinazohusu ukatili wa kijinsia na watoto.
Alisema Kampeni hiyo ililenga kuelimisha
jamii kuhusu sera zinazopinga ukatili wa kijinsia ili jamii ielewe haki zao za
msingi na maeneo wanayopaswa kukimbilia kupata msaada baada ya kukumbwa na
ukatili wa aina yoyote.
Alisema kampeni hiyo ililenga katika
Kata tano za Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ambazo ni kata za Bagamoyo,
Bulyaga, Malindo, Masoko na Mpuguso pamoja na kata moja katika
Halmashauri ya Busokelo ambayo ni kata ya Kambasegera.
Aliongeza kuwa Wanawake wengi pamoja na
watoto ndiyo wanaoathirika na ukatili wa kijinsia kutokana na maumbile yao
ingawa pia kuna wanaume wanaofanyiwa hivyo lakini wanashindwa kutoa taarifa.
Mratibu huyo aliongeza kuwa zoezi hilo
limelenga jinsi zote ili kuwakumbusha wanajamii kuchukua hatua za haraka pindi
wanapokumbwa na ukatili ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wanaume na wanawake
kuacha ukatili dhidi ya wenzie.
Alisema hakuna mfumo maalumu
unaomwelekeza mwathirika wa ukatili kwa kukimbilia ingawa kuna vituo vingi
vikiwemo dawati la Jinsia katika vituo vya Polisi, ofisi za ustawi wa jamii
katika ngazi za kata na Watendaji wa Kata.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika
Kampeni hiyo, Violeth Mwakatuma ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa kata ya Bulyaga
alilipongeza shirika la Kihumbe kwa kampeni hizo na kusisitiza jamii kuacha
vitendo hivyo.
Aliongeza kuwa ni vyema wanajamii
kutokaa na matukio hayo majumbani kwao bali wanapaswa kutoa taarifa katika
vyombo vya sheria ili wahusika wachukuliwe hatua inayostahili.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment