Waumini wa kanisa la Wadventista wa
Sabato Jimbo la Nyanda za juu kusini mkoani Mbeya limetoa msaada wa vitu
mbali mbali kwa wafungwa wa gereza la Ruanda jijini hapa.
Akizungumza na waandishi wa Habari
katika Hafla ya kukabidhi zawadi hizo kwa niaba ya Askofu Joseph Mngwabi,
Mkurugenzi wa Afya na Mawasiliano Jimbo la Nyanda za juu kusini wa Kanisa la
Sabato, Mchungaji Haruni Kikiwa, amesema ni sehemu ya kutimiza neno la Mungu.
Amesema msaada huo umetolewa na kanisa
pamoja na waumini waishio ndani na nje ya nchi ambao wametoa zawadi mbali mbali
ambazo zitanufaisha Gereza zima zenye thamani ya zaidi ya shilingi Milioni 3.7.
Amezitaja zawadi hizo kuwa ni pamoja na
vyakula na matunda vyenye thamani ya shilingi Milioni 2,027,000 Nguo shilingi
240,000 na vitabu vya dini 525 vyenye thamani ya shilingi million 1.3
ambavyo vilikabidhiwa gerezani hapo na kufuatiwa na ibada ya kawaida.
Kwa upande wake Mchungaji Eliot Kiswaga
ambaye ni mkufunzi wa dini Gerezani hapo amesema ni vema taasisi zingine za
kidini na mashirika binafsi yakajitoa kwa ajili watu wenye mahitaji kama
wafungwa kwa kutoa misaada mbali mbali ili kuwatambua kama jamii ya kawaida.
Naye muumini wa Kanisa hilo, Tully
Musyani, amesema kama waumini wa Kanisa la Wadventista wa sabato wanaguswa sana
na binadamu wenzao wanaotumikia vifungo magerezani hivyo njia ya kuwafariji
katika shida hizo ni kutoa misaada ya hali na mali.
Amesema kanisa kupitia kwa waumini wao
na marafiki wanaoishi nje na ndani ya Nchi wameitikia wito wa kutoa vitu mbali
mbali ili kuwafariji wafungwa gerezani pamoja na kutoa pongezi kwa Wahitimu wa
mafunzo ya neno la Mungu yaliyotolewa na Chuo cha Sauti ya unabii chenye makao
makuu mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo yamewanufaisha Wafungwa 262
na Askari 20 wa Jeshi la Magereza wa Gereza la Ruanda mkoani Mbeya wamehitimu
mafunzo ya Biblia yaliyotolewa na Chuo cha sauti ya unabii kinachomilikiwa na
Kanisa la Wadventista wa Sabato nchini.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment