ASKARI wa Jeshi la Polisi na raia mmoja
wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Mbeya wakituhumiwa kwa makosa
mawili ambayo ni kula njama za kutenda kosa pamoja na wizi wa mtoto.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Mshtakiwa wa
kwanza aliyekuwa Ditektivu Constebo wa Polisi mwenye namba WP 5367 Prisca
Isaya (35) mwenyeji wa Ilala Dar es salaam ambaye hata hivyo alivuliwa vyeo na
kufukuzwa kazi kabla ya kupandishwa Mahakamani na Salehe Mwangosi (28)
mkazi wa Njisi wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya.
Akisoma mashtaka yanayowakabili
Mwendesha mashtaka wa Serikali, Juliana William, mbele ya Hakimu wa Wilaya ya
Mbeya, Maria Batulaine, alisema watuhumiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na
makosa mawili waliyoyatenda Aprili 4, Mwaka huu.
Alisema kosa la kwanza ni kula njama kwa
nia ya kutenda kosa la kuiba mtoto kinyume cha kifungu cha 384 (16) cha kanuni
ya adhabu kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002 walilofanya Aprili 4, Mwaka huu
katika eneo la Songwe wilayani Kyela.
Alitaja kosa la pili kuwa ni Wizi wa
mtoto kinyume cha kifungu cha 169 (1) (a) sura ya 16 ya kanuni ya adhabu
kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mwendesha mashtaka huyo aliiambia
Mahakama kuwa washtakiwa wote kwa pamoja mnamo Aprili 6, Mwaka huu katika eneo
la Zahanati ya Njisi Wilaya ya Kyela Mkoani hapa kwa maksudi waliiba mtoto
mwenye umri wa siku saba kutoka kwa mama yake mzazi Mboka Mwakikagile.
Washtakiwa wote kwa pamoja walikana
kuhusika na tukio hilo ambapo upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa shauri
hilo umekamilika na upo tayari kuwaleta mashahidi wake kwa ajili ya kuendelea
na usilizwaji wa kesi.
Kwa upande wake Hakimu aliahirisha kesi
hadi Mei 6, Mwaka huu na kwamba dhamana kwa washtakiwa iko wazi kama watakidhi
vigezo ambavyo ni kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye mali zisizo
hamishika zenye thamani ya shilingi Milioni 5, barua ya mtendaji na barua
kutoka kwa mwajiri kwa ajili ya mshtakiwa wa kwanza.
Hata hivyo walishindwa kuwa na wadhamini
waliokidhi vigezo vya mahakama na kuamliwa kurudishwa rumande hadi Mei 6, Mwaka
huu kesi itakapo kuja kwa ajili ya kusikilizwa.
Mwisho.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment