USHAHIDI wa kesi inayowakabili Askari
Polisi mmoja na Askari Magereza pamoja na Raia wengine watatu wanaotuhumiwa kwa
unyang’anyi wa kutumia nguvu umeendelea kutolewa katika Mahakama ya Wilaya ya
Mbeya.
Katika Kesi hiyo, Mhakama iliweza
kusikiliza ushahidi wa Shahidi mmoja tofauti na Mashahidi Sita kama upande wa
Waendesha mashtaka ulivyodai mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Mbeya chini ya
Hakimu Mfawidhi, Michael Mteite.
Shahidi huyo ambaye ni shahidi namba
mbili kwa mujibu wa Mahakama, Kitinkwi Mtatiro ambaye ni Mkaguzi msaidizi wa
Polisi na Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi (O-CID) Wilaya ya Mbeya, ambaye
aliiambia Mahakama kuwa siku ya ambayo ni Januari 3, Mwaka huu alikuwa kwenye
majukumu yake ya kazi ya kila Siku.
Shahidi huyo ambaye alikuwa akiongozwa na
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Basilius Namkambe, alisema majukumu yake ya
kila siku ni pamoja na kuangalia nidhamu ya Askari waliochini yake, kufuatilia
makosa makubwa pamoja na kufanya kazi za upekuzi maeneo mbali mbali.
Alisema siku ya tukio alimuaga bosi wake
ambaye ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya kuwa anaenda kufuatilia tukio la
uhalifu maeneo ya Soweto ambapo baada ya kufika huko muda mfupi tu alipokea
simu kutoka kwa Bosi wake huyo huyo akimweleza kuwa amepata taarifa kutoka kwa
msamaria mwema kuwa kuna tukio la uporaji eneo la Kawetere.
Shahidi huyo aliendelea kuieleza
Mahakama kuwa baada ya kupokea maelezo hayo aliwasiliana na Msaidizi wake
aliyemtaja kwa jina la Philibert Matoo ambaye alienda eneo la tukio huku
wakiendelea kuwasiliana kupitia Simu ya upepo(Redio call).
Alisema wakati akisikia maelekezo
kupitia simu ya upepo alisikia Msaidizi wake akiomba msaada wa nguvu kisha
mawasiliano yakakatika na kumlazimu yeye mwenyewe kuacha kazi aliyokuwa
akiifanya na kuamua kuelekea eneo la tukio.
Alisema alipokuwa njiani kuelekea eneo
la tukio akiwa Isanga tankini alikutana na msafara wa magari matano yakiwa
yanakimbia ambapo aliweza kuligundua gari la polisi aina ya Landcruser ndipo
alipoamua kuunga msafara ulioishia katika kituo cha Polisi cha Kati.
Alisema baada ya kufikia eneo hilo
alipewa maelekezo kutoka kwa msaidizi wake ambapo baada ya hapo aliandaa hati
ya dharula ya kupekua mali wazokuwa nazo kwenye magari mawili yaliyokuwa
yakimikiwa na watuhumiwa.
Alisema kwenye gari ya Kwanza yenye
namba za Chesesi GX 6011832 Aina ya Grand Mark II, iliyokuwa ikiendeshwa
na mtuhumiwa namba moja ambaye ni PC James mwenye namba F8302 akiwa na
mtuhumiwa namba tatu,walikuta mabegi mawili ya nguo, Laptop Mbili, Chaji ya
Simu,Simu mbili za Mkononi pamoja na Pingu moja.
Aliongeza kuwa katika upekuzi katika
Gari ya pili aina ya Toyota Cresta yenye namba T 182 BEU Mali ya mtuhumiwa
namba mbili Elinazi Mshana na kukuta Mablanketi mawili yakiwa kwenye mifuko
yake.
Hata hivyo Mwendesha Mashtaka wa Serikali
aliiomba Mahakama kupokea maelezo ya upekuzi kama vielelezo vitakavyotumiwa na
mahakama jambo amblo lilipingwa vikali na upande wa utetezi ukiongozwa na
Wakili Ladislaus Lwekaza ambaye alidai kuwa maelezo hayo hayakuandikwa katika
katatasi maalumu kwa mujibu wa kifungu cha 38.
Akijibu pingamizi hilo, Namkambe alisema
Shahidi wake alisema alifanya upekuzi katika mazingira ya dharula kwa mujibu wa
kifungu cha 42 na siyo anavyodai wakili wa utetezi.
Kutokana na majibizano hayo Mahakama
ilipokea maelezo hayo kama kielelezo P2 ambapo pia Mahakama ililazimika kuhamia
Nje kwa ajili ya Shahidi kutambua magari waliyokutwa nayo watuhumiwa ambapo
baada ya kutambuliwa pamoja na vitu vilivyokutwa yalipokelewa kama vielelezo
kama P3 na P4.
Awali Mwendesha mashtaka wa Serikali
Basilius Namkambe alisema washtakiwa wote kwa pamoja wanatuhumiwa kwa
kosa moja la unyang’anyi kinyume cha Sheria kifungu cha 287 sura ya 16
kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Namkambe aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni Mshitakiwa namba moja ambaye ni Askari Polisi PC James
mwenye namba F8302 wa Wilaya ya Mbeya ambaye kabla ya kufikishwa mahakamani
alivuliwa Uaskari baada ya kuhukumiwa kijeshi.
Aliwataja wengine kuwa ni mshtakiwa
namba mbili kuwa ni Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya, Askari
Magereza mwenye namba B 500 Sajenti Juma Mussa(37) wa Gereza la Ruanda
Mbeya,Mbaruku Hamis(29) Mkazi wa Iyela na Amri Kihenya(38) Mkazi wa Iyela.
Akisoma mashtaka yao Mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, Namkambe alisema watuhumiwa hao
walitenda kosa hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo la
Mlima Kawetere barabara ya Mbeya Chunya.
Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja
walitenda kosa hilo kwa kulizuia gari aina ya Pick Up lililokuwa likiendeshwa
na Ezekia Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye alikuwa na mtu
aliyekuwa akifahamika kwa jina la Sreedhar Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia
wakitumia magari madogo mawili ambayo ni GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari
linguine ambalo lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 AINA YA Grand Mark II.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho kwa
mashahidi wengine kuendelea kutoa ushahidi wao, huku Mahakama hiyo ikiendelea
kusisitiza kuwa itahakikisha kuwa kesi hiyo itaisha muda mfupi kama ilivyopangwa.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment