Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Tuesday, January 21, 2014

SHULE mbalimbali za msingi katika mji wa Tunduma wilaya ya Momba Mkoani Mbeya zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa watoto madarasani kutokana na ukosefu wa madawati na madarasa

Katibu wa CCM kata ya Tunduma, Hemed Stephen alipotembelea baadhi ya shule katika kata hiyo Januari,mwaka huu akiambatana na kamati ya siasa na uchumi.
SHULE mbalimbali za msingi katika mji wa Tunduma wilaya ya Momba Mkoani Mbeya zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa watoto madarasani kutokana na ukosefu wa madawati na madarasa.

Hayo yamebainika katika ziara ya Katibu wa CCM kata ya Tunduma, Hemed Stephen alipotembelea baadhi ya shule katika kata hiyo Januari 15,mwaka huu akiambatana na kamati ya siasa na uchumi.

Katika ziara hiyo ambayo aliongozana na Afisa Elimu wa mji wa Tunduma  Franco Ngonya ilimpelekea kutembelea shule za Manga Mwaka na Mkombozi ambapo alishuhudia changamoto hizo.

Alisema katika shule ya msingi Mwaka yenye jumla ya wanafunzi 1727 ikiwa na walimu 22 tu huku ikiwa na vyumba 11 vya madarasa ambapo ina upungufu wa vyumba 19 hali inayolazimu walimu kufundisha kwa awamu mbili asubuhi na mchana ili kila mtoto aweze kusoma.

Alisema  walimu wanakabiliwa na ukosefu wa ofisi ya walimu na samani ambapo mwalimu mkuu wa shule ya Manga iliyopo Mwaka Betina Timoth alimweleza Katibu kuwa shule yake inakabiliwa na upungufu wa madawati 268 na walimu 59 hivyo hulazimika kufundisha watoto zaidi ya mia katika kila darasa badala ya 45 kama ulivyo utaratibu.

Kutokana na upungufu wa vifaa vya ofisi ya Walimu Katibu huyo  alitoa viti vitano kwa ajili ya ofisi ya walimu.

Katibu aliendelea na ziara yake katika shule ya Mkombozi ambapo alishuhudia darasa moja likiwa na watoto 350 huku baadhi ya watoto wakiwa wameeti chini kwa ukosefu wa madawati na vyumba vya madarasa na kujionea madarasa yaliyokwama kuezekwa kutokana na ukosefu wa fedha baada ya wazazi kujenga hadi mtambaa panya.

Pia alisomewa risala na mwalimu mkuu  Simika Hakton ambaye alimwambia katibu na ujumbe wake kuwa wanakabiliwa na changamoto ya samani za walimu hali inayowafanya walimu kufanya kazi katika mazingira magumu.

Hata hivyo Katbu alimtaka Afisa Elimu kutoa kipaumbele kwa shule hiyo kuezekwa kwa madarasa ambapo alikiri kutengwa shilingi milioni 45 zitakazogawanywa shilingi Milioni 10 kila moja kwa shule za Mwaka,Mkombozi,Uhuru na Migombani ili kupunguza msongamano madarasani.

Alihitimisha ziara yake shuleni hapo kwa kutoa mchango wa shilingi 232,000/- kwa ajili ya kupunguza kero ya samani shuleni hapo ambapo mwalimu Simika alimshukuru Katibu kwa moyo wa uzalendo na kuahidi kuzitumia kwa malengo yalikusudiwa.

Mwisho.
 Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu

1 comment:

Anonymous said...

IDADI HIYO YA WANAFUNZI NDANI YA DARASA MOJA HAIKUBALIKI NA NDIYO CHANZO CHA ELIMU KUPOROMOKA.