MFUKO
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya watu
wa Ujerumani (KfW) imeunga mkono mkakati wa Kitaifa wa kupunguza vifo vya akina
mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano kwa kutoa vifaa tiba katika
vituo vya matibabu vinavyohudumia kundi hilo.
Msaada
huo unaohusisha mikoa ya Mbeya na Tanga wenye thamani ya shilingi milioni 989.1
umekabidhiwa leo na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid kwa
niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hussein Mwinyi kwa Waganga Wakuu
wa mikoa hiyo.
Akikabidhi msaada huo, Dk. Rashid
alisema kuwa msaada huo utaboresha huduma za akina mama wajawazito na kupunguza
vifo vitokanavyo na uzazi lakini pia ni fursa ya vyanzo vya mapato kwa
Halmashauri na watoa huduma.
“Sote
tunafahamu kuwa matibabu sahihi yanatokana na vipimo sahihi hivyo uwekezaji
unaofanywa kwa pamoja na NHIF & KfW kupitia mradi huu kwa lengo la
kuviwezesha vituo vya matibabu kupata vifaa tiba utasaidia sana kupunguza
tatizo la upatikanaji wa huduma ya vipimo kwa akina mama wajawazito na watoto,”
alisema Dk. Rashid.
Kutokana
na hali hiyo, Dk. Rashid aliwaagiza Waganga Wakuu ambao wamekabidhiwa vifaa
hivyo kuhakikisha vinatumika ipasavyo na kutunzwa kwa faida ya Taifa ili
vipumguze vifo vya akina mama hao na watoto.
“Ni
vyema walengwa wa mradi huu wakapata huduma bora na si bora huduma, msaada huu
uwe na matokeo mazuri kwa walengwa ili mradi uwe na manufaa kwa nchi yetu,”
alisema.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Hamisi Mdee alisema
Mfuko unatarajia mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo yatashawishi akina mama
wengi zaidi kutumia huduma za uzazi salama katika vituo vya matibabu lakini pia
wafadhili kupanua maeneo ya mradi katika mikoa wanayofadhili.
Aidha
alizitaka Halmashauri kuwasilisha kwa wakati madai yao baada ya kutoa huduma
kwa wanachama pamoja na maombi ya fedha za tele kwa tele ili kuboresha huduma
za matibabu katika vituo vyao.
Akizungumzia
mafanikio ya mradi, alisema kuwa hadi sasa umefikia walengwa 74,099 ambao ni
sawa na asilimia 105 na jumla ya shilingi 644,1118,912 zimelipwa kwa vituo vya
matibabu vya mikoa ya Mbeya na Tanga vilivyotoa huduma kwa akina mama hao
lakini pia shilingi milioni 400.4 zimetumika kulipia familia za akina hao
kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Picha na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment