Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, January 17, 2014

HAKIMU Mkazi wa Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Michael Mteite amewagiza wakili kuhakikisha anampeleka mtuhumiwa mahakamani hata kwa machela.

Wanaotuhumiwa kwa ujambazi wa kutumia siraha
Ulinzi mkali uliimarishwa mahakamani hapo



HAKIMU Mkazi wa Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Michael Mteite amewagiza wakili kuhakikisha anampeleka mtuhumiwa mahakamani hata kwa machela.

Hakimu Mteite alilazimika kutoa kauli hiyo  wakati akisikiliza kesi inayowakabili Askari wawili wa jeshi la Polisi na Magereza pamoja na watu watatu ambao ni raia wa kawaida  wanaotuhumiwa kwa ujambazi wa kutumia silaha.

Kauli ya Hakimu ilikuja kufuatia mmoja kati ya washtakiwa wote watano kushindwa kuhudhuria mahakamani wakati kesi yao ilipangwa kuendelea na ushahidi baada ya Wakili wa Serikali  Archiles Mulisa kuhoji Mhakamani kuwa Mshtakiwa namba mbili Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya hajafika huku upande wa jamhuri ukiwa hauna taarifa.

Kutokana na hoja hiyo ndipo aliposimama Wakili wa Utetezi ambaye anawasimamia watuhumiwa wote wato, Ladislaus Lwekaza na kuiambia Mahakama kuwa Mshtakiwa namba mbili ameshindwa kuhudhuria kesi yake kutokana na kuwa majeruhi yaliyotokana na kupigwa risasi sehemu ya paja hivyo kumfanya kuwa na maumivu makali anayougulia akiwa gerezani.

Lwekaza alidai kuwa kutokana na mteja wake huyo kuwa majeruhi aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi hapo mtuhumiwa huyo hali yake itakapotengemaa na kuongeza kuwa pia hawataweza kuendelea na kesi kutokana na washtakiwa wote kutopewa hati za mashtaka na maelezo ya mlalamikaji ili wajiandae na utetezi.

Hata hivyo Wakili wa Serikali Mulisa alisimama na kumuuliza Wakili wa utetezi kuwa anapaswa kuiambia mahakama kifungu alichotumia kudai hati ya mashtaka pamoja na maelezo ya mlalamikaji sambamba na majeraha aliyopata mtuhumiwa kuwa aliyapata wakati gani na lini.

Kwa upande wake Hakimu Mteite aliiambia Mahakama kuwa kutokana na ubishani wa pande zote mbili ameona aingilie na kuwashauri kuwa madai ya upande wa utetezi kuhusu hati ni haki ya kikatiba kupewa mshtakiwa.

Mteite aliongeza kuwa madai ya majeruhi ya Mshtakiwa namba mbili ni mbinu za kuchelewesha kesi ambazo mara nyingi hufanyika ili mahakama ishindwe kuendelea na kesi na kuongeza kuwa yeye binafsi pamoja na mahakama hakubaliani na suala hilo.

Alisema kama taarifa za ugonjwa huo zingikuwa za kweli Jeshi la Magereza linajua taratibu ambapo mgonjwa hupelekwa Hospitali ambapo mahakama ikitambua huhamishia kesi zake hospitali.

Alisema Wakili wa utetezi anapaswa kutambua kuwa mwenendo wa Mahakama wa siku hizo tofauti na zamani ambapo kesi moja ilikuwa ikichukua hadi zaidi ya miaka mitatu lakini sasa wamejipanga kumaliza kesi mapema kabisa.

Kutokana na hali hiyo Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 20 Mwaka huu na kumwagiza Wakili wa Utetezi Lwekaza kuhakikisha inampeleka Mtuhumiwa siku ya kesi kwa njia yoyote hata kama ni mgonjwa namna gani ikiwa ni pamoja na kumbeba kwa machela au gari la wagonjwa.

Pia alimwagiza mwendesha mashtaka wa Serikali kuhakikisha anawapatia washtakiwa madai yao ambayo ni kupatiwa hati za mashtaka, nakala ya maelezo ya mlalamikaji pamoja na mwenendo wa awali wa kesi.

Awali Mwendesha mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa akisaidiwa na Basilius Namkambe alisema washtakiwa wote kwa pamoja  wanatuhumiwa kwa kosa moja la unyang’anyi wa kutumia Silaha kinyume cha Sheria kifungu cha 287 sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

 Mulisa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mshitakiwa namba moja ambaye ni Askari Polisi PC James mwenye namba F8302 wa Wilaya ya Mbeya ambaye kabla ya kufikishwa mahakamani alivuliwa Uaskari baada ya kuhukumiwa kijeshi.

Aliwataja wengine kuwa ni mshtakiwa namba mbili kuwa ni Elinanzi Mshana(22)Mkazi wa Iyela Jijini Mbeya, Askari Magereza mwenye namba B 500 Sajenti Juma Mussa(37) wa Gereza la Ruanda Mbeya,Mbaruku Hamis(29) Mkazi wa Iyela na Amri Kihenya(38) Mkazi wa Iyela.

Akisoma mashtaka yao Mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Michael Mteite, Mulisa alisema watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Januari 3, Mwaka huu majira ya saa 11 jioni katika eneo la Mlima Kawetere barabara ya Mbeya Chunya.

Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kulizuia gari aina ya Pick Up lililokuwa likiendeshwa na Ezekia Matatira (34) Mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye alikuwa na mtu aliyekuwa akifahamika kwa jina la Sreedhar Pasupelet(38) mwenye asili ya Kiasia wakitumia magari madogo mawili ambayo ni GX 100 Toyota Cresta T 782 BEU na Gari linguine ambalo lilikuwa na namba za Chesesi GX 6011832 AINA YA Grand Mark II.

Na mbeya yetu

No comments: