IMEELEZWA kuwa njia rahisi ya kupunguza
umaskini kwa jamii ya Watanzania ni kuwahamasisha wananchi kujikita katika
miradi ya ufugaji wa kuku, kwa kile kilichodaiwa kutokuwa na gharama kubwa.
Hayo yalibainishwa na Afisa Kilimo na
Mifugo wa Halmashauri ya Busokelo,Gidion Mapunda wakati wa uzinduzi wa Mradi wa
ufugaji Kuku wa Kikundi cha Mshikamano katika sherehe zilizofanyika juzi katika
viwanja vya ofisi za kikundi hicho zilizopo kata ya Lufilyo Wilayani Rungwe
Mkoa wa Mbeya.
Mapunda alisema mradi wa kuku ni rahisi
sana kuendeshwa na kila mwananchi endapo atahamasishwa kufuga kuku kwa kutumia
rasilimali zinazomzunguka kwa kujengea mabanda ya kawaida ambayo yanaweza
kumkomboa kiuchumi na hatimaye kupunguza wimbi la umaskini miongoni mwa jamii.
“ kila mtu aanze kufuga kuku nyumbani kwake
na siyo lazima kujenga mabanda ya kisasa tumieni rasilimali zinazowazunguka
ambazo ni rahisi kuzipata bila gharama yoyote lakini matunda yake yatakuwa
makubwa baada ya kuanza kuvuna mayai” alisema Afisa huyo.
Aliongeza kuwa mbali na mradi wa ufugaji
kuku kuwa rahisi kuendeshwa na kila mtu pia kunachangamoto ya upatikanaji wa
madawa ya kinga ya mifugo inayotokana na kufungwa kwa kiwanda kilichokuwepo
Nchini hivyo kutegemea madawa kutoka nje ya nchi ambayo ni gharama kuhifadhi.
Alisema ili kuepukana na magonjwa
nyemelezi kwa mifugo ni bora wananchi na wafugaji wakazingatia usafi wa mabanda
wa mara kwa mara hali itakayosaidia kuepusha magonjwa yasiyokuwa ya lazima kwa
mifugo hususani Kuku wanaoathirika zaidi na ugonjwa wa kideli.
Awali akisoma Risala mbele ya
mgeni rasmi na wageni waalikwa, Katibu wa Kikundi cha Mshikamano, Nikutusya
Sakujonga alisema kikundi kilianzishwa Mwaka 2011 na sasa kina kuku wapatao 100
ambao wameanza kutaga hivyo kikundi hukusanya mayai zaidi ya 70 kwa siku.
Alisema wakati kikundi kinaanzishwa
kilikuwa na wananchama 20 lakini hadi sasa wamebakia 10 kutokana na wengine
kuhama makazi katika kata hiyo na kuhamia maeneo mengine ambapo Wanaume
wako watano na wanawake wako watano ambao wanawakilishwa vitongoji tofauti.
Aliongeza kuwa kikundi kilianza na mtaji
wa shilingi 100,000/= lakini sasa mtaji unazidi kukua na kufikia shilingi
Milion 4,500,000/= pamoja na kujiunga na chama cha kuweka na kukopa Saccos.
Katibu huyo alisema chama kinamatarajio
mengi sana ambapo aliyataja moja wapo kuwa ni kununua mashine ya kukoboa na
kusaga nafaka ambayo itasaidia upatikanaji wa chakula cha kuku, kununua mashine
ya kutotoreshea vifaranga, kusomesha watoto yatima na kumwezesha kila
mwanakikundi kuwa na mradi wake binafsi.
Aidha alitoa shukrani kwa Serikali ya
Mkoa wa Mbeya kwa kukipatia kkikundi hicho mizinga 10 ya Nyuki pamoja na
Asasi ya Elimisha ambayo ndiyo iliyotoa elimu kwa wananchi wa Kata ya Lufilyo
kujiunga katika makundi na kufungua miradi elimu ambayo imezaa matunda kwa kuanzishwa
kwa kikundi cha Mshikamano na kuwa na mradi mkubwa wa ufugaji wa kuku.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment