Wakazi wa wilaya ya Chunya wapo hatarini kukumbwa na
magonjwa ya mlipuko kutokana na Halmashauri ya wilaya kushindwa kuzoa taka
katika ghuba la soko kuu wilayani humo.
Wakazi hao waliongea jinsi wanavyokerwa na hali hiyo
kufuatia kujaa kwa taka na kushindwa kuzolewa kwa muda mrefu takribani mwezi
mmoja licha ya kutozwa ushuru kila mwezi kati ya shilingi elfu tatu hadi elfu
sita.
Ghuba hilo hivi sasa linatumiwa pia na wananchi
wanaolizunguka soko hilo ingawa hawachangii tozo lolote na taka zimekuwa
zikizagaa kwenye makazi ya watu na hata kwenye migahawa inayozunguka ghuba
hilo.
Mwenyekiti wa soko hilo Bwana EMMANUEL MWAKAJUMBA alikataa
kulizungumzia suala hilo licha ya kukiri kuwepo kwa taka hizo kwa muda mrefu
sasa ingawa wafanyabiashara wamekuwa wakitozwa tozo ya usafi kila mwezi.
Aidha ujenzi wa soko hilo umeendelea baada ya kusimama kwa
muda mrefu kutokana na ukosefu wa pesa ambapo sasa kiasi cha shilingi milioni
sitini zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na awamu ya pili ya uezekajii wa
mabati baada ya kukamilika kwa lenta.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya CHAKUPEWA
MAKELELE Amesema kuwa nia ya Halmashauri yake ni kumaliza soko hilo kwa wakati
kadri wanavyopata pesa ili kuwaondolea adha wakazi wa wilaya hiyo lakini pia kuongeza
mapato ya Halmashauri.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Chunya DEODATUS KINAWIRO amesema nia ya serikali ni kuhakikisha
inaboresha kila maeneo ikiwa ni pamoja elimu ,afya,barabara kwa kutumia vyanzo
vya mapato ya ndani ili kuwaletea wananchi maendeleo yaliyokusudiwa.
Picha na Ezekiel Kamanga
Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment