Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, August 30, 2013

MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII(TASAF) WAZINDUA AWAMU YA TATU WILAYANI MBARALI.

 Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulam Hussein Kiffu kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro, akifungua warsha hiyo

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali, Mhandisi Venant Komba akisoma taarifa kwenye warsha hiyo


Picha ya pamoja

MFUMO mpya wa utekelezaji wa Mfuko wa maendeleo ya jamii(TASAF) wa awamu ya tatu wa mpango wa kunusuru kaya maskini zilizo katika mazingira hatarishi nchini, umepokelewa kwa mwitikio mkubwa na wadau wa maendeleo wilayani hapa.

Aidha baadhi ya wadau hao pia wameipongeza Serikali ya awamu ya nne kwa kutengeneza miradi ambayo humnufaisha mwananchi moja kwa moja kwa kupitia wawakilishi wao ambao ndiyo wanaotakiwa kuchagua na kupendekeza miradi ya kutekelezwa.

Hayo yalibainshwa wakati wa Washa ya kuwajengea uwezo Wakuu wa Idara na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya kuhusu mradi wa awamu ya tatu wa Mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF) iliyofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya maji uliopo katika mji mdogo wa Rujewa Wilayani hapa.

Walisema mpango wa kunusuru kaya maskini ni mzuri kutokana na kuwalena wananchi moja kwa moja katika ngazi za vijiji na mitaa wanayoishi baada ya kukidhi vgezo vitakavyokuwa vimewekwa na TASAF pamoja na uwezeshwaji uliotolewa kwa Madiwani ambao ni wawakilishi wa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kenneth Ndingo alisema utekelezaji wa mradi wa awamu ya tatu utafanikiwa zaidi tofauti na miradi iliyopita kutokana na wahusika kufika jirani na maeneo ambayo miradi itatekelezwa.

Aliongeza kuwa mpango wa kupunguza umaskini ni mzuri na utaleta manufaa makubwa kwa maendeleo ya nchi baada ya wananchi wa hali za chini kuwezeshwa kiuchumi baada ya kupatiwa misaada na kufundishwa namna ya kujishughulisha na ujasiliamali.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbarali, Mhandisi Venant Komba  Mradi wa awamu ya Tatu utafanikiwa endapo changamoto zilizoonekana katika awamu ya pili zitaondolewa mapema kabla ya mradi kuanza.

Alizitaja baadhi ya changamoto zilizojitokeza katika awamu ya pili kuwa ni pamoja na gharama kubwa za kuendeshea miradi kuwa tofauti na fedha halali zinazotolewa na Tasaf hivyo kuzifanya Halmashauri kutafuta fedha kutoka katika vyanzo vingine vya mapato.

Alisema changamoto nyingine ilikuwa ni elimu kwa wananchi ambao ndiyo walengwa wakubwa kutokuwa na mwitikio wa kuchangia baadhi ya michango ambayo walipaswa kuchangia kama mradi ulivyokuwa umeainishwa.

Alisema katika awamu ya pili jumla ya miradi 87 katika Kata 10 na vijiji 50 ilitekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5 ambapo  wananchi walichangia shilingi Milion 234,797, 450 katika kufanikisha miradi hiyo ambayo imekamilika yote kwa asilimia mia moja isipokuwa mradi mmoja ambao fedha zake zilichelewa kufika.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Taifa, Mhandisi Elisifa Kinasha,ambaye pia ni Meneja miradi wa Mfuko huo alisema mpango wa awamu ya tatu umelenga kunusuru kaya maskini kutokana na athari za umaskini na kuziwezesha kupata mahitaji ya msingi, kulinda rasilimali zao na kuwekeza kwa maendeleo yao.

Alisema mradi huo umegawanywa katika sehemu kuu nne ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kwa awamu ya miaka mitano mitano ambapo alizitaja sehemu hizo kuwa ni pamoja na Kunusuru kaya maskini na zilizo katika mazingira hatarishi.

Sehemu nyingine ni kuinua hali ya maisha na kuongeza kipato kwa kutoa msaada kwa watu wenye kuonyesha jitihada katika kuboresha kipato na kuinua hali za maisha kwa kuweka akiba.

Alisema sehemu nyingine itakuwa ni ujenzi wa miundombinu katika vijiji ambavyo havina miundombinu au huduma kuwa mbali ili kuwasaidia walengwa kuweza kutimiza masharti ya mpango huo.

Alesma sehemu ya mwisho ya mradi huo itakuwa ni kujenga uwezo kwa kutoa mafunzo kwa wadau katika ngazi zote za taifa, Mkoa, Wilaya, Kata, Vijiji na Shehia ambapo mafunzo yatatolewa ili utekelezaji wa mpango ufanyike kwa mujibu wa utaratibu na hivyo kufanikisha malengo yaliyowekwa.

Mhandisi Kinasha aliongeza kuwa katika mradi wa awamu ya tatu jumla ya kaya 275000 zitanufaika kwa nchi nzima ambapo kwa kuanzia mradi utaanza katika Halmashauri 14 ikiwemo Wilaya ya Mbarali iliyoteuliwa katika Mikoa ya Rukwa na Mbeya kutokana na utafiti uliyofanyika mwaka 2011.

Aidha katika Washa hiyo ilifunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gulam Hussein Kiffu kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro, ambapo alisema mradi huu ili ufanikiwe ni lazima ushirikishwaji wa wadau uzingatiwe.

Aliongeza kuwa mradi huu ulizinduliwa na Raisi Kikwete Agosti 15, mwaka jana Mkoani Dodoma baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa awamu ya kwanza na awamu ya pili.

Alisema wadau waliopatiwa mafunzi ni vema wakatekeleze kile walichofundishwa kwa kuwafikia walengwa na kutoa elimu kuhusu mradi huo ili isiwe na vikwazo wakati wa utekelezaji wake.

Hata hivyo Washa hiyo itafanyika kwa siku tano kwa kuwajengea uwezo Madiwani, Wakuu wa Idara na wataalamu wa Halmashauri ili kuwawezesha kutoa elimu kwa wananchi ambao watafikiwa na mradi ili kurahisisha utekelezaji wake.

Na Mbeya yetu

No comments: