WATU watatu wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa
kutenda kosa la kumuua kwa kukusudia aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha kuweka
na Kukopa (Saccoss), Mbeya
Akisoma mashtaka hayo, Mwendesha Mashtaka wa
Serikali Hebel Kihaka mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya
Venance Mlingi alidai Watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa la mauaji kwa
maksudi kinyume cha Sheria ya Makosa ya Jinai kifungu cha 196 sura ya 16 kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Jailo Rashid
(30), Niza Hamis (24) na Medi Keya(33) ambao kwa pamoja walimuua kwa maksudi,
Ambrose Shayo(45) aliyekuwa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Saccos Taifa na Tazara
Saccos ya Jijini Mbeya.
Alisema watuhumiwa hao kwa pamoja walitenda kosa
hilo April 20, Mwaka huu majira ya saa 3 usiku katika Kijiji cha Itagano
Kawatere Jijini Mbeya ambapo Marehemu alivamiwa na watu hao kisha kumuua.
Kwa upande wake Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo
Venance Mlingi alisema Kwa mujibu wa Sheria watuhumiwa hawaruhusiwi kujibu
chochote kutokana na Mahakama yake kutokuwa na uwezo wa kusikiliza Shauri la
Mauaji.
Aliongeza kuwa Shauri hilo limeletwa kwa ajili ya
hatua za awali ambapo baada ya upelelezi kukamilika litapelekwa Mahakama kuu
kwa ajili ya taratibu za kusikiliza, pia aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 3,
Mwaka huu itakapotajwa tena.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment