WALIMBWENDE wanaoshiriki vinyang’anyiro mbali
mbali hapa nchini na nje ya nchi wameaswa kulinda maadili na utamaduni wa
Tanzania ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanaheshimika.
Mwito huo ulitolewa na Mbunge wa Viti
maalumu Mkoa wa Mbeya kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Mary Mwanjelwa
alipokuwa akiongoza shughuli za usafi wa Mazingira zilizofanywa na walimbwende
30 walioko kwenye kambi ya kumtafuta Mwanamitindo wa Nyanda za Juu kusini.
Mwanjelwa aliongoza usafi huo kuanzia Stendi kuu
ya Mabasi yaendeyo Mikoani, Stendi ya Daladala ya Mwanjelwa na kuishia Stendi
kuu ya Daladala ya Kabwe Jijini Mbeya huku akiongozana na Walimbwende hao.
Mbunge huyo alisema lengo la kufanya usafi ni
kutokana na mtoto wa kike kuwa ndiye mwanaharakati anayetakiwa kuwa mfano
katika usafi wa mazingira ambayo husaidia kujenga afya nzuri na kuimarisha
uchumi wa eneo husika.
Alisema Mtoto wa kike ndiye anayetakiwa
kuwamstari wa mbele katika kuhakikisha anatengeneza mazingira masafi na mazuri
kwa ajili ya kujenga afya bora na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii.
Aidha aliwasihi walimbwende hao kuheshimu mila na
utamaduni wa Mtanzania pindi wanapokuwa wakishiriki mashindano hayo na siyo
kuiga tabia ambayo siyo nzuri na inayoitambulisha vibaya nchi ya Tanzania.
Alisema suala la ulimbwende ni suala la utamaduni
na sanaa hivyo linatakiwa kuungwa mkono na jamii yote na siyo kuwakatisha tama
waandaaji.
Kwa upande wake mwandaaji wa mashindano hayo
Bahati Mwakalinga alisema Jumla ya Walimbwende 30 watachuana jukwaani kumtafuta
Mwanamitindo wa Nyanda za Juu kusini katika mashindano yakayofanyika Machi 30,
Mwaka huu katika Ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya.
Alisema washiriki hao wametoka katika Mikoa ya
Mbeya, Katavi, Rukwa, Njombe, Iringa na Ruvuma ambapo alitaja viingilio kuwa ni
Shilingi 10,000/=, 25,000/= kwa Vip na 50,000/= kwa ajili ya meza yenye
watu watano.
Alisema mashindao hayo yameandaliwa na kampuni ya
Tanzania Youth Arise kutoka Dar Es Salaam ambayo imekuwa akiandaa mashindao
kama hayo kwa miaka mitano mfulululizo kwa mikoa ya Dar Es Salaam na Pwani
ambapo kwa kanda ya Nyanda za Juu Kusini ni mara ya kwanza.
Aliongeza kuwa washindi watano katika
kinyanyanyiro hicho wataenda kushiriki mashindano mengine ya dunia yaitwayo
Miss Universe pamoja na zawadi mbali mbali ambazo hakuweza kuzitaja.
Walimbwende hao kwa hivi sasa wameweka kambi
katika Hoteli ya Manyanya iliyoko Forest Mpya Jijini Mbeya.
|
No comments:
Post a Comment