VIONGOZI na
Watumishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya wametakiwa kufanya kazi
kwa ushirikiano na vyama vya siasa vya upinzani ili kuwaletea maendeleo
wananchi.
Hayo yamesemwa na
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Dk. Norman Sigalla ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya
Mbeya wakati akifungua warsha juu ya Demokrasia na Stadi za uongozi inayotolewa
kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi pamoja na Madiwani wa Mkoa wa Mbeya.
Dk. Sigalla alisema
Chama cha Mapinduzi ni mlango wa kuingilia ili kupata uongozi ili kuwahudumia
wananchi lakini siyo sababu ya kuwachukia viongozi wa vyama vya upinzani.
" Si sahihi
kugombana na na kiongozi wa chama kingine bali shirikianeni ili muwaletee
maendeleo wananchi ambapo mtakapokuwa na ushirikiano na upendo ndipo watakapo
watamani na kuhamia kwenye chama chenu" alisema Mkuu huyo.
Aliongeza kuwa
Warsha zinazotolewa kwa viongozi zinasaidia kuwakumbusha wajibu wao kwa chama
na kwa wananchi ili wasijisahau katika utendaji kazi wa kila siku ikiwa ni
pamoja na kutekeleza Ilani za Chama.
Alisema kazi ya
kiongozi wa Chama ni kujibu hoja za wananchi na siyo kiongozi kujifanyia mambo
ambayo wananchi hawayahitaji na ambayo yanasababisha kuwachukia viongozi.
Kaimu Mkuu wa Mkoa
huyo alisema ili Chama kiendelee kubaki madarakani ni wajibu wa Viongozi
waliopewa dhamana na wananchi kuyatendea kazi madai yao ambayo yataepusha
migogoro isiyokuwa na sababu.
Kwa upande wake
Mwaandaaji wa Mafunzo hayo Dk. Marry Mwanjelwa Mbunge wa Viti maalumu Mkoa wa
Mbeya alisema mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya
mkutano mkuu wa wajumbe wa CCM Taifa walioagizwa kuwajengea uwezoviongozi wa
Chama.
Alisema lengo la
kutoa mafunzo hayo ni kuwakumbusha viongozi waliokuwepo madarakani kuhusu
uwajibikaji pamoja na kuwajengea uwezo viongozi wapya walioingia madarakani
hivi karibuni.
Naye mfadhili wa
Mafunzo hayo Dk. Stefan Chrobot ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa shirika la Fes-
Tanzania kutoka Ujerumani alisema wameamua kufadhili mafunzo hayo kutokana na
shirika hilo kuwa na ushirikiano na Chama cha Mapinduzi.
Alisema kazi ya
Shirika hilo ni kukuza demokrasia na utawala katika jamii, kuinua haki za
binadamu za kupata huduma muhimu za kijamii na namna ya kuepukana na rushwa.
Na Mbeya yetu
|
No comments:
Post a Comment