Pombe hizo ambazo zipo kwenye makaratasi ya
plastiki, zimezagaa kila kona ya wilaya ya Kyela, Rungwe, Mbeya mjini, Mbeya
Vijijini, Mbarali, Mbozi na Momba huku zikiuzwa bei ya kati ya Sh.100-300 bei
gharama ambazo vijana wengi wanaimudu na wanapokunywa wengi huzidiwa na kuanza
kutokwa na jasho.
Hali hiyo imejidhihilisha baada ya Mwandishi
wa habari hizi kutembelea wilaya ya Kyela iliyopo mkoani Mbeya na kukuta vijana
wengi wakinywa pombe hizo ambazo wamekiri kuwa zinaathari kwa Afya zao.
Wakiongea kwa ombi la kutoandikwa majina yao,
vijana wa eneo la Kasumulu, Kyela Mjini na Ipinda walisema kuwa wengi
wanaotumia pombe hizo hugeuka vituko na wale wanaotumia vyombo vya moto hasa
pikipiki huishia kugonga watu na baadhi yao kupoteza maisha.
’’Pombe hizi ni nzuri kwa bei lakini zina
madhara makubwa kwasababu wengi tumewaona wakitumia pombe hizi huanza kutokwa
jasho jingi katika miili yao jambo ambalo linaonesha kuwa pombe hizi zinakausha
maji mwilini lakini vijana wanashindwa kuiacha kutokana na bei ni ndogo na
hazikatazwi na Serikali’’ alisema mmoja wa vijana waliohojiwa.
Sanjari na hilo walibainisha moja ya athari
iliyowahi kutokea kuwa ni kifo cha kijana mwenzao John Mwakapisye
kilichotokea Julai 20,2010 baada ya kijana huyo kunywa pombe hizo kisha
kuendesha pikipiki na baadaye kupinduka na kujisababishia kifo.
Waliongeza kuwa uwepo wa pombe hizo ambazo
zinatengenezwa na kiwanda cha Bwenda Group Limited kilichopo mjini Lilongwe
nchini Malawi kumetokana na kuadimika kwa pombe iliyojulikana kwa jina la
Kadansana kutoka huko huko nchini Malawi.
Wakielezea kwa kina uwepo wa uholela wa pombe
hizo ambazo wamekiri kuwa huingizwa nchini kwa njia za magendo, walisema kuwa
pombe aina ya Kandasana nayo pia ilikuwa na madhara kwa watumiaji ambapo wengi
wao hasa wanaume walikuwa wakiishiwa nguvu za kiume baada ya kunywa pombe hiyo.
’’Unashangaa hizi Mowa wa Mafumu na Rider!
Mwanzo kulikuwa na pombe ilikuwa inaitwa Kadansana ambayo ilikuwa na athari
kubwa zaidi kwasababu wanywaji hasa wanaume walikuwa wakiishiwa nguvu za
kiume’’ alieleza mmoja wa vijana mjini Kyela.
Uwepo wa pombe hizo hapa nchini ni mwendelezo
wa udhibiti mdogo wa dawa na vyakula hapa nchini hususani mkoa wa Mbeya ambapo
hivi karibuni tuliweka wazi matumizi mabaya ya vidonge vya Crolofenical
kutumika katika pombe za kienyeji huku Mamlaka ya udhibiti wa dawa na chakalu
TFDA wakisema kuwa hawajui lolote.
Kwa upande wake mkaguzi wa TFDA nyanda za juu
kusini Rodney O. Atananga, alisema utaratibu wa kukamata bidhaa
zilizopigwa marufuku nchini na ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu
huhusisha pia Jeshi la polisi na idara ya afya.
Alisema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa mara kwa
mara ili kubaini ubora wa bidhaa zilizoko sokoni ili kubaini usalama wake na
kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu.
Atananga alisema watu wanaokamatwa na bidhaa
hizo wanafikisha mahakamani kwa sababu ni kinyume na sheria ya chakula na dawa
ya mwaka 2003 ambayo inakataza kuuza na kusambaza bidhaa ambazo
hazijasajiliwa na kupigwa marufuku.
Alisema baadhi ya bidhaa zilizopigwa marufuku
ni vipodozi vyenye viambato vyenye sumu pamoja na vinavyoingia nchini bila
kibali au kusajiliwa.
Aliongeza kuwa bidhaa zenye viambapo vyenye
sumu zinakatazwa kwa sababu zinamadhara kwa mwili wa binadamu ambapo alisema
madara yake hutokea baada ya muda mfupi na mengine huchukua muda mrefu
kujitokeza.
Alisema baadhi ya madhara hayo ni kansa ya
ngozi na damu ambayo hujitokeza baada ya muda mrefu lakini madhara ya muda
mfupi ni uharibifu wa ngozi na wajawazito kuharibu uzio wa ubongo wa mtoto
akiwa tumboni pamoja na kuumwa kichwa.
Kwa sasa pombe kali zilizozagaa mkoani Mbeya
ni pamoja na Zed pineapple spirit, double punch,Assorted sarit, Power na Rider
can.
No comments:
Post a Comment