Mchina katulia anasubiri oda ya chakula toka kwa mama ntilie wala hana wasiwasi na mgogoro huo
KAMPUNI ya wachina inayoendelea na ujenzi wa barabara za Jiji la Mbeya ( CICO), imedaiwa kuvamia eneo la wananchi na kuanza kuchimba vifusi vya udongo kinyume cha taratibu katika eneo la Machinjioni Kata ya Ilomba.
Imeelezwa kuwa Kampuni hiyo, imeingizwa mjini na watu wanaojitambulisha kwamba wao ni wamiliki halali wa ardhi hiyo hivyo kuingia mkataba feki ambao umesababisha kuwepo kwa mgogoro mkubwa na mmiliki halisi wa eneo hilo.
Kitendo cha kampuni hiyo kuingia kwenye ardhi hiyo na kuanza kufanya kazi kilipelekea wakazi wa eneo hilo kufanya vurugu zilizoambatana na kupiga mawe mitambo na magari ya wachina hao.
Akizungumza na Mbeya yetu Kenneth Mwang’amba ambaye ndiye anayedai kulimiliki eneo la kiwanja hicho chenye hati miliki yenye namba 2459, alisema kitendo walichofanya wachina hao kufanya shughuli za uchimbaji katika eneo lake ni ukiukwaji wa sheria.
“Hili eneo mimi nalimiliki kihalali licha ya kuwepo kwa mgogoro na skauti ambao awali walinyang’anywa eneo hili baada ya kushindwa kutimiza baadhi ya vigezo na kukabidhiwa kwangu,”alisema
Mwang’amba alisema eneo hilo limekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati yake na Skauti Mkoa wa Mbeya ambao walivamia eneo hilo bila kufuata taratibu huku mamlaka zinazohusika zimeshindwa kutoa ufafanuzi kuhusu nani ndiye mmiliki halali wa eneo hilo.
Alisema baada ya kukosa maelewano na skauti, Halmashauri ya Jiji iliamua eneo hilo lichukuliwe na Skauti ambapo pia walitakiwa kulipa fidia kwake baada ya makubaliano kutokana na uharibifu uliokuwa umetokana.
Aliongeza kuwa kutokana na Skauti kushindwa kulipa fidia hivyo hawakuwa na uhalali wowote wa kuendesha shughuli ya aina yoyote katika eneo hilo kutokana na Skauti kushindwa kulipa fedha walizokuwa wakidaiwa.
“ Kisheria hawa watu wa Skauti hawakutakiwa kufanya shughuli zozote katika kiwanja hiki kwa sababu mimi ndiye mmiliki halali wa eneo hili hadi hapo watakapokuwa wametimiza masharti hata kunilipa fidia kwa sababu awali kulikuwa na tofali ambazo ziliharibika kutokana na mgogoro ” Alisema.
Kwa upande wake Msemaji wa Skauti Mkoa wa Mbeya Uswege Kagubo Mwaitebele ambaye pia ni mkufunzi wa Skauti alisema waliwaruhusu wachina kuchimba eneo hilo kwa makubaliano ya kuwajengea kituo cha kufundishia skauti hivyo hawakuona sababu za kusubiri.
Kuhusu mgogoro uliopo kati ya Skauti na Mwang’amba, Mwaitebele alikiri kuwepo kwa mgogoro huo ambapo naye alisema eneo hilo linamilikiwa kihalali ingawa walishindwa kulipia fidia kama walivyokubaliana.
Pia alikiri kutofuata taratibu za kuruhusu uchimbaji wa vifusi pasipokuwa na kibali kutoka katika Halmashauri husika ambapo yeye alifanya hivyo bila kuwahusisha viongozi wenzie wa Skauti kwa madai kuwa yeye ni kiongozi wa Skauti wa kanda hivyo kama kanda haina ofisi nayeye amekuwa akijitolea kuhifadhi nyaraka za Skauti katika Ofisi yake.
Naye Afisa ardhi wa Jiji la Mbeya Ephraimu Mkumbo alikiri kuwepo kwa mgogoro wa eneo hilo huku akiwatupia lawama Skauti kwa kufanya shughuli zao kinyume na taratibu ambapo alisema wameshindwa kuonesha hata ofisi zao zilipo kwa ajili ya ufuatiliaji wa madai hayo.
Mkumbo alisema Halmashauri ya Jiji iliwaamuru Skauti kulipa fidia za eneo hilo kwa mhusika kama watahitaji kulimiliki kihalali ambapo alisema wamekuwa wakipiga chenga bila taarifa zozote hadi leo unapoibuka mgogoro mwingine.
“Ukweli ni kwamba mpaka sasa mmiliki halali wa eneo hili na Keneth Mwang’amba hivyo wachina hao wanapaswa kuondoka na kusitisha shughuli zao,”alisema
Hata hivyo, Kiongozi huyo alishangazwa na kitendo cha wachina hao kuchimba vifusi katika eneo hilo kwani walishapangiwa eneo la kuchimba vifusi eneo la Kawetere nje kidogo ya Jiji la Mbeya hivyo wamekiuka sheria na wanachofanya sasa ni uharibifu wa Mazingira.
No comments:
Post a Comment