Wanawake wa kijiji cha Ifiga kata ya Ijombe wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya wakiwa katika foleni ya maji kwenye kisima ambacho maji yake si safi na salama na wanadai maji hayo huwasababishia ugonjwa wa kichocho
Na Francis Godwin
WANAWAKE wa kijiji cha Ifiga kata ya Ijombe wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya wamedai kuwa tatizo la maji katika kijiji hicho limeendelea kuwa sugu na kupelekea kutumia maji ya kisima ambayo si safi na salama na kujikuta wakiendelea kukumbwa na tatizo la ugonjwa wa kichocho .
Wakizungumza na timu ya wanahabari wanaharakati wa mtandao wa jinsia Tanzania (TGNP) waliotembelea kijijini hapo leo wanawake hao walisema kuwa kijiji hicho kutokana na ukosefu wa huduma hiyo ya maji wamekuwa wakilazimika kuchota maji katika kisima kimoja kilichoppo kijijini hapo ambacho maji yake si lazima kwa afya za binadamu.
Alisema Sophia John kuwa kisima hicho kimekuwa kikitumia na wakazi zaidi ya 2000 wa kijiji hicho na kuwa pamoja na kuwa maji hayo si salama baadhi ya watu hasa watoto wamekuwa wakiyanywa pasipo kuchemcha hali inayochangia kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wa kichocho katika kijiji hicho.
John alisema kuwa mbali ya watoto wa kijiji hicho kukumbwa na tatizo la ugonjwa wa kichocho kutokana na huduma hiyo ya maji wanayoitumia kuwa si salama bado wamekuwa wakichangia mradi wakiiomba serikali kusaidia kutatua tatizo hilo bila mafanikio .
Kwani alisema wanananchi wa eneo hilo hasa wanawake na watoto wamekuwa wakiathirika zaidi na tatizo la ukosefu wa maji kutokana na kisima hicho kuwa mbali na makazi yao hivyo wakati mwingine kutumia muda wa masaa manee hadi 6 kwenda kufuata huduma hiyo ya maji Kisimani .
Alisema kuwa tatizo hilo limepelekea kasi ya wanawake kuzalisha kupungua zaidi na kulazimika kuachiwa majukumu zaidi ya kulea familia kwa kufanya kazi ya kusaka maji pamoja na shughuli nyingine za shamba huku baadhi ya wanaume wao wakishinda katika vijiwe wakisubiri kuhudumiwa na mwanamke.
Kwa upande wake Anna Mbalawala alisema kuwa tatizo hilo la maji limeanza kujitokeza kati ya mwaka 2007 baada ya uongozi wa Halmashauri ya mji wa Mbeya kuanza mchakato wa kuwa jiji na hivyo kulazimika kuchukua mradi wa maji ambao ulichangiwa na wananchi wa kijiji hicho pia kwa kuchimba mtaro wa maji kutoka kijijini hapo na maji hayo kwenda kutumiwa na wakazi wa jiji la Mbeya.
“Hapa kijijini tulikuwa na maradi wa maji ambao tulikuiwa tukiutumia kupitia shirika la DANIDA ila toka mwaka 2007 mradi huo ulichukuliwa na jiji la Mbeya japo sisi wakazi wa kijiji hiki ndio tupo jirani na chanzo cha maji na tulishiriki kuchimba mtaro ….sasa hivi maji safi na salama tunapata kwa wiki mara moja na siku nyingine zote tumekuwa tukitumia maji ya kisima”
Frola Mlowezi (34) anadai kuwa kutokana na wananchi wa kijiji hicho kutumia maji ya kisima ambayo si salama watoto wake wawili wamekuwa wakitibiwa ugonjwa wa kichocho kutokana na kutumia maji hayo ya kisima.
Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya maji kijijini hapo Molis Selema alisema kuwa kabla ya mradi huo kuchukuliwa na jiji mwaka 2007 kulikuwa na kamati ya watumiaji maji ambayo kwa sasa ilivunjwa baada ya jiji kuchukua maradi huo.
Alisema kuwa kabla ya mradi huo kuchukuliwa kata zinazozunguka mradi huo zaidi ya tano zilipiga kura na kuonekana kata mbili za Idaba na Ijombe kushindwa kutetea mradi huo hivyo kuchukuliwa na jiji na wananchi wa kijiji cha Ifiga ambao ndio walikuwa wakitegemea mradi huo kuendelea kukosa huduma hiyo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Ifiga Raphael Syejele alithibitisha kuwepo kwa tatizo hilo la maji kijijini hapo na kuwa ugonjwa huo wa kichocho unachangiwa na huduma mbaya ya maji wanayotumia wananchi wake .
Alisema kuwa kijiji hicho kina idadi ya watu 1175 wakiwemo watoto 748 na wazee 127 ambao pia apo hatarini kukumbwa na ugonjwa huo wa kichocho kutokana na kunywa maji hayo.
Hata hivyo alisema kati ya wakazi wa kijiji hicho 636 ni wanawake ambao ndio wamekuwa wakitegemewa zaidi katika familia kwa kutumia kutafuta huduma hiyo ya maji.
Afisa afya wa kito cha afya Ifiga hakuweza kupatikana ili kueleza ukubwa wa tatizo hilo la ugonjwa wa kichocho katika kijiji hicho,huku kwa upande wake mhadisi wa maji wilaya ya Mbeya Bahati Haule alisema kuwa bado serikali haina mpango wowote katika kijiji hicho kwa sasa katika kutatua kero ya maji wakati baadhi ya vijiji kama Iwalanje mkakati wa kutatua kero ya maji unafanyika.
Alisema kuwa hali ya upatikanaji wa maji safi kwa sasa katika Halmashauri ya Mbeya ni chini ya aslimia 50 japo alisema ipo mipango mbali mbali ya kutatua tatizo hilo baadhi ya maeneo huku akidai kuwa mbali ya kijiji cha Ifiga kutumia maji ya kisima bado kijiji cha Iwalanje pia wanatumia maji ya kisima.
Alisema tayari Halmashauri imepokea fedha kutoka benki ya Dunia kiasi cha shilingi milioni 800 kwa ajili ya kutatua kero ya maji kijiji cha Iwalanje huku akidai kwa Ifiga bado wanasubiri wahisani.
No comments:
Post a Comment