Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, June 14, 2012

WANAUME KATA YA IJOMBE MBEYA WADAIWA KUNYANYASA WANAWAKE NA WATOTO WAKATI WA MAVUNO


Mwanaume mkazi wa Iwalanje kata ya Ijombe ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja akiuza kabichi ambazo alikuwa amezisogeza barabarani kusaka wateja kama alivyonaswa na kamera ya mtandao huu ,wanaume wa kata hiyo wanatuhumiwa na wanawake kuwa wanawanyanyasa kwa kuuza mazao na pesa kuongeza wanawake


kabichi zikipakiwa katika gari kwa ajili ya kwenda kuuzwa mjini shughuli iliyokuwa ikifanywa na wanaume watatu wa kijiji cha Iwalanje Mbeya


Mwanamke mkazi wa Iwalanje Mbeya akihudumia shamba la mazao ya biashara ambayo mwisho wa siku wanaume ndio wamekuwa wakinufaika zaidi huku wanawake na watoto wakiendelea kunyanyasika


Akina mama wajasiriamali wakazi wa kata ya Ijombe wakitafuta wateja wa nyanya baada ya kata hiyo kukosa soko


Kaloti zikioshwa katika mto Kijombe japo uoshaji huu si salama sana kwa uhifadhi wa mazingira


Mwanaume mkazi wa kata ya Ijombe mbeya akisafisha kaloti kwa ajili ya kuzisafirisha mjini kwa kuziuza ,wanaume wa kata hiyo wamekuwa wakilalamikiwa kwa kutelekeza familia kipindi cha mavuno kwa kuuza mazao na kutumia pesa vibaya


Na Francis Godwin  
UKOSEFU wa masoko katika kata ya Ijombe wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya umetajwa kuwa ni chanzo cha wanawake na watoto kuendelea kunyanyasika kutokana na badhi ya wanaume kutumia mwanya huo kusafirisha mazao mjini na fedha kutumia kwa anasa .
Wakizungumza wanahabari wanaharakati wa mtandao wa kijinsia Tanzania (TGNP) kijijini hapo leo baadhi ya wanawake wa kata hiyo ya Ijombe walisema kuwa , kukosekana kwa masoko katika kata hiyo ndiko kunapelekea wao na watoto kuendelea kunyanyasika katika mgawanyo wa kipato kinachotokana na mavuna wanayoyapata .
Zuwena Mwakyoma na Atuganile Mwasanga wakazi wa kata hiyo ya Ijombe walisema kuwa pamoja na kuwa wakati wa kuandaa mashamba kwa kulima na kutunza mazao hayo hadi yanafikia wakati wa kuvunwa ila ikifika wakati wa mavuno wanaonyanyasika zaidi ni wanawake na watoto huku wanaume wao wakitumia nafasi hiyo kujineemesha mijini .
Zuwena alisema kuwa wakati kata hiyo ya Ijombe ikiwa ni moja kati kata zinazoongoza kwa kuzalisha mazao mbali mbali ya kibiashara ila bado serikali haijaweza kuwakomboa wakulima hao kwa kujenga soko la mazao ambalo litawasaidia wakulima wa kata hiyo kuuza mazao yao na kunufaika na kilimo .
“Leo tumekuwa tukishuhudia jinsi ambavyo sisi wanawake na watoto tunavyonyanyasika na kilimo na kushuhudia baadhi ya wanawake wakinyanyasika kwa waume zao kuongeza wanawake wakati wa mavuno kutokana na wao kuwa wasimamizi wakuu wa mazao hayo ….wamekuwa wakiyasafirisha kwa usafiri wa mikokoteni hadi mjini na huku wakiuza pesa zote wanatumika katika pombe na kuhonga wanawake”
Hivyo alisema njia pekee ya wanamke na mtoto wa pembezoni mwa miji kuweza kukombolewa ni serikali kuweka utaratibu wa kujenga masoko katika kata hiyo na kata nyingine ambazo zipo pembezoni na miji .
Huku Atuganile akidai kuwa mbali ya baadhi ya wanaume wa kata hiyo kuendelea kuwanyanyasa wakati wa mavuno kwa kuwaongezea wanawake ama wapenzi katika nyumba zao ila bado hata madalali wamekuwa ni kikwazo kikubwa kwani wamekuwa wakifika na kununua mazao yakiwa mashambani .
Alisema kuwa madalali hao wamekuwa wakifika kununua mazao katika mashamba hayo hata kabla ya kuvunwa na sehemu kubwa ya wanaoathirika na mfumo huo wa madalali ni wanawake wajane ambao hawana uwezo wa kutafuta masoko wala kupata fedha za kusafirishia mazao hao na hivyo kukubali kuuza mazao yao kwa bei yeyote ile .
“Kuna baadhi ya kaya ambazo zinaongozwa na mama na baba mwenye moyo wa upendo katika familia yake zimekuwa zikinufaika na kilimo kutokana na kuuza mazao kwa ushirikiano na pesa hutumika kwa matumizi mazuri ila baadhi ya kaya suala la masoko ni kilimo endelevu”
Pia alisema suala la ushuru limeendelea kuwa kero kutokana na serikali ya wilaya kuwatoza ushuru mara mbili mazao yakiwa shambani na pindi yanapopelekwa sokoni Uyole .
Deus Mwambaje mkazi wa kijiji cha Iwalanje kata hiyo ya Ijombe akijibu madai ya wanawake hao alisema kuwa si wanaume wote ambao wamekuwa wakinyanyasa wake zao wakati wa mazao na kuwa badhi ya kaya zimekuwa na ushirikiano kwa kulima pamoja na kuuza kwa utaratibu mzuri ila badhi ya kaya zimekuwa zikiongoza kwa migogoro na kesi wakati wa mavuno kutokana na wasimamizi wa familia hiyo ambao ni wanaume kuwa na mfumo dume kwa kuuza mazao na pesa kuhonga wanawake mjini.
Hata hivyo alidai kuwa pamoja na kuwa kata hiyo inaongoza kwa kulima nyanya, njegere ,viazi ,karoti na vitunguu pamoja na mazao mengine mengi ya biashara ila hakuna soko hata moja.
Afisa biashara wa wilaya ya Mbeya Castro Temihanga alithibitisha madai ya wanawake hao wa kata ya Ijombe kuwa ni kweli kata hiyo mbali ya kuongoza kwa uzalishaji ila hakuna soko na kuwa jitihada za Halmashauri kuzungumza na watu wa SIDO ili kusaidia kujenga soko eneo hilo zinafanyika.

No comments: