*Baba yake afukuzwa kijijini kwa tuhuma za wizi
*Marehemu alituhumiwa kuiteketeza kwa moto Mahakama ya mwanzo.
******
Habari na Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Mkazi mmoja wa Kijiji cha Igoma, Kata ya Igoma, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoani Mbeya Riziki Limbakisya (25), ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za wizi.
Tukio hilo limetokea Mei 15 mwaka huu majira ya saa 11:25 jioni katika eneo la msitu wa Shule ya Sekondari Igoma iliyopo wilayani humo, baada ya marehemu kukutwa akiwa na spika na deck mali ya Bwana Elias Mbwete na Musa Mchona, ambavyo viliibiwa katika nyakati tofauti kijijini hapo ambapo baada ya uchunguzi wahanga walimbaini mtuhumiwa wao.
Kutokana na kuchoshwa na vitendo vya wizi wa mara kwa mara kijijini hapo na mara baada ya kumkamata walimpiga na kumsababishia majeraha mbalimbali mwilini mwake, ambapo hasira zake ziliishia kwa kumteketeza baada ya kumzinga kwa shehena la kuni zilizowashwa kwa petroli huku wananchi hao wakiimba nyimbo za kejeli.
Baada ya tukio hilo uliitishwa mkutano wa hadhara uliokuwa ukijadili masuala ya maendeleo ya kijiji hicho, baada ya wananchi kumtaarifu Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Elias Mwaipopo ambapo wananchi wote walikimbilia eneo la tukio na kukuta mwili wa marehemu ukiendelea kuteketea.
Naye, Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Bwana Samwel Malesa, baada ya kufika eneo la tukio alitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ambao walifika eneo la kijiji na kukuta baadhi ya mwili wa marehemu ukiendelea kuteketea huku mikono yto ikiwa imeteketea kabisa.
Kwa upande wake Bwana Elias Mbwete alisema kuwa usiku wa Mei 14 mwaka huu Grocery yake ilivunjwa na kuibiwa TV, Deck, remote 2, simu moja na pesa taslimu shilingi 145,000, hivyo kufanya jumla ya mali zote zilizoibiwa kuwa na jumla ya thamani ya shilingi 675,000.
Hata hivyo Mchungaji Abel Mwakisyala wa Kanisa la Church Gospel International (COG) la kijiji hicho, amesikitishwa sana na kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi, lakini alivitaka vyombo vinavyosimamia sheria kufanya kazi kwa uadilifu kwani wananchi hao huchoshwa na vitendo vya kuwaona wahalifu mitaani pindi wanapokamatwa na makosa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment