BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya limepinga hatua ya wajumbe wa kamati inayohusika na masuala ya ukimwi kwenda mkoani Tanga kwa ziara ya kujifunza namna ya kupambana na maambukizi ya Virusi vya ukimwi kupitia kukutana kimwili kwa watu wa jinsia moja ya kiume yaani ushoga.
Kauli ya baraza juu ya ziara hiyo imetokana na maelezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 iliyokuwa ikijadiliwa katika kikao maalumu ambapo miongoni mwa vipengele vyake vimeonesha madiwani watatu na wataalamu wawili watapaswa kwenda mkoani Tanga kujifunza namna ya kupambana na maambukizi ya VVU kwa njia ya ushoga.
Baraza hilo liliipinga ziara hiyo likisema maambukizi ya VVU yanayotokea wilayani hapa ni kupitia kujamiiana kwa watu wa jinsia tofauti,matumizi ya kuchangia kwa vitu vilivyo na ncha kali pamoja na maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kamwe si ushoga. Mmoja wa madiwani wa baraza hilo Rhodes Mwaikambo alisema si jambo la busara kwa kamati husika kutumia kiasi cha shilingi 7,000,000 kwenda kujifunza namna ya maambukizi ya VVU utoka kwa mwanaume kwenda kwa mwanaume badala yake waendekejifunza kule walikofanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya kawaida. Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri hiyo Meckson Mwakipunga amesema kipaumbele cha elimu dhidi ya maambukizi ya Ukimwi kinapaswa kulenga kupunguza asilimia saba ya maambukizi yalioyopo wilayani hapa na si maambukizi kupitia ushoga. Ameitaka kamati husika kufanya utafiti upya na kubaini maaeneo kuliko na mafanikio makubwa katika kupunguza kiwango cha maambukizi ili wajumbe watakaporejea walete elimu itakayoisaidia wilaya. Akitetea hoja ya ziara hiyo,mratibu wa ukimwi wilayani hapa Tengamitumba Mululumilwa amesema ililenga halmashauri kujiandaa ili siku za usoni itakapokumbwa na matukio ya ushoga iwe na utayari wa kukabiliana na maambukizi ya aina hiyo.
Kwahisani ya Joachim Nyambo |
No comments:
Post a Comment