WAFANYAKAZI wa halmashauri nchini, wametakiwa kuhakikisha wanathibitishwa kazini, ili wanapopata matatizo haki zao za msingi ziweze kupatikana kutoka kwa waajiri wao.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu chama cha wafanyakazi wa serikali za mitaa Taifa (TALGWU) Sudi Madega wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya viongozi wapya wa chama hicho kutoka mikoa ya Iringa, Rukwa na Mbeya.
Alisema, mbali na uthibitisho huo pia wanatakiwa kutunza kumbukumbu zao zote za kazini ambazo ni muhimu, zikiwemo barua za ajira, ili wanapostaafu waweze kupata mafao yao , bila ya usumbufu wowote.
Alisema, baadhi ya watumishi wamekuwa hawatunzi kumbukumbu zao na hivyo pindi wanapostaafu taratibu za kupata mafao yao yote inakuwa ni ngumu, na kwamba hata maafisa utumishi ni wazembe wa kutunza kumbuku za wafanyakazi wao.
Aidha. Alisema kuwa baadhi ya wakurugenzi wamekuwa wakikaa na nyaraka za wafanyakazi kwa muda mrefu bila ya kuzifikisha mahala husika jambo alilosema kuwa ni kuwanyima haki zao za msingi.
Pia aliwataka viongozi hao wapya kuhakikisha wanajadili na kuyawekea mikakati mambo mbalimbali watakayozungumza ili yawasaidie miaka mitano ijayo.
“Kazi kubwa inayokikabili chama hiki ni kutoa elimu kwa wanachama na waajiri ili kufahamu umuhimu wa chama, pamoja na kujitangaza kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari,”alisema
No comments:
Post a Comment