Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, September 29, 2011

VYAMA VYA SIASA IRINGA VYAMLILIA WAKILI MWAKINGWE KAMPENI ZA NCCR MAGEUZI ZASIMAMA

Na blogu ya  Francis Godwin
WAKATI vyama vya  siasa  katika wilaya ya Iringa mjini  vikiendelea kukamiana katika kampeni za lala  salama kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa diwani  wa  kata  Gangilonga na Kitanzini katika  jimbo la Iringa mjini  hapo  jumapili wiki  hii chama  cha NCCR- Mageuzi  kimelazimika  kusimamisha kampeni  zake kwa muda  usiojulikana  kutokana na  kifo  cha ghafla  cha wakili maarufu wa  kujitegemea mkoa  wa Iringa Nelson Thomas Mwakingwe (pichani) ambaye  pia alikuwa ni mme  mwekahazina  wa Taifa wa chama  hicho Mariam Mwakingwe.

Huku  chama cha mapinduzi (CCM) na  chama cha  Demokrasia na maendeleo (Chadema ) vikituma  salam  za rambirambi pamoja na  kuungana na  NCCR-Mageuzi katika  kusitisha kampeni kwa muda.

Mwenyekiti  wa NCCR - Mageuzi   wilaya ya Iringa mjini  Nasra Mwampeta ambaye  pia ni mgombea  udiwani  wa kata ya Kitanzini alimweleza  mwandishi  wa habari  hizi jana  kuwa  chama chake  kimelazimika  kusitisha kampeni  hizo  kutokana na msiba  huo mkubwa  kwa  wakazi  wa mji  wa Iringa.

Alisema  kuwa  kifo cha  ghafla cha wakili  huyo  kimewashitua  wakazi  wa mji  wa Iringa hivyo  NCCR- Mageuzi kutokana na msiba  huo  kimelazimika  kusimamisha  shughuli  zote za kampeni  katika kata  ya Gangilonga na Kitanzini ili kupisha maombolezo  kwa  wananchi  wa mji  wa Iringa.

Mwampeta ambaye  pia ni mgombea  wa kata ya Kitanzini aliwaomba  radhi  wananchi  wa kata  hiyo  ya kitanzini kwa  kutoendelea  kupata  sera  za NCCR-Mageuzi kabla ya uchaguzi mkuu japo aliomba siku ya kupiga kura  kuchagua  chama hicho kwa kata ya Gangilonga  kumpigia  kura  Karimu  Masasi (NCCR-Mageuzi).

Mbali ya  kuwa  wakili Mwakingwe  pia  alipata  kuwa  diwani  wa kata ya Gangilonga kupitia NCCR-Mageuzi kati ya mwaka 1995 hadi 2000.

Kwa  upande  wake  katibu  wa chama  cha mapinduzi (CCM)  wilaya ya Iringa mjini Lusiana Mbosa alisema  kifo cha  wakili  Mwakingwe ni pigo  kubwa  kwa  wananchi  wa manispaa ya Iringa  bila  kujali itikadi  zao  za vyama kwani marehemu enzi  za uhai  wake  alikuwa  msaada mkubwa  kwa  wananchi katika masuala ya  sheria.

Mbosaa alisema  kuwa CCM kwa  siku ya jana  ililazimika   kusitisha  shughuli za kampeni  kwa ajili ya  kuungana na wafiwa katika  kuomboleza msiba  huo mzito na  kuwa katika kata ya Gangilonga CCM pia imepata kusimamisha mgombea wake Nicolina  Lulandala  huku Kitanzini  ikimsimamisha Jasca Msambatavangu.

Mwenyekiti  wa Chama cha  Demokrasia na maendeleo (Chadema)  wilaya ya Iringa mjini Mchungaji  Peter Msigwa  mbali ya  kutoa  pole kwa  wafiwa bado  alisema  kuwa  Chadema Iringa  imepokea  kwa masikitiko  kifo cha  wakili  huyo na kuwa itaungana na  wafiwa na  wakazi wa mji  wa Iringa siku ya jumamosi  katika mazishi.

Msigwa ambaye  pia ni mbunge  wa jimbo la Iringa mjini  alisema  kuwa Chadema imemsimamisha Edwin  Sambala kwa kata ya Gangilonga na Kitanzini  Gervas kalolo na  kuomba  wananchi  kutumia haki yao kuchagua viongozi  wa Chadema bila  kutishwa na mtu.


Wakili  Mwakingwe alifariki ghafla  dunia usiku wa kuamkia  jana akiwa katika  hospital ya mkoa  wa  Iringa kabla ya  kifo  chake Mwakingwe  alikuwa  akisumbuliwa na tatizo la kisukari
Wakili  Mwakingwe atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa aliopata kuutoa katika jamii ya wakazi wa mkoa wa Iringa ikiwa ni pamoja na kusaidia wanyonge kupata haki zao kwa kuwatetea akiwa kama wakili .

Pia alikuwwa ni mmoja kati ya mawakili waliopenda kujichanganya na jamii zaidi na kuwa jirani na wananchi na ni wakili pekee aliyepata kuingia katika ulingo wa siasa.

Kifo cha wakili Mwakingwe si pigo tu kwa familia bali ni pigo kwa Taifa zima kutokana na kupunguza idadi ya mawakili wa kujitegemea hapa nchini na kifo hiki ni pigo kwa chama cha NCCR Mageuzi kutokana na marehemu alipata kuwa diwani wa chama hicho japo kwa upande mwingine kifo cha wakili Mwakingwe kinakwamisha kampeni za uchaguzi mdogo kwa kata ya Gangilonga na Kitanzini kwa chama cha NCCR Mageuzi kutokana na mke wa Marehemu Bi Mariam kuwa ni mratibu mkuu wa kampeni hizo na ndiye nguzo ya NCCR kwa mkoa wa Iringa.

Kifo chake kimepokelewa kwa majonzi makuwa na wakazi wa mji wa Iringa ambao kwa nyakati tofauti wamepata kueleza masikitiko yao.

Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi wa CCM Iringa mjini Eliud Mvella Wamahanji anasema kuwa marehemu alikuwa ni shemeji yake na kuwa amepata taarifa ya msiba huo akiwa safarini kurejea Iringa na kuwa kifo hicho ni pigo kubwa ndani ya familia .

Deus Kalinga ni mkazi wa Gangilonga anasema kuwa kwa upande wake bado haamini kama kweli wakili huyo amefariki dunia na kueleza kuwa Mwakingwe ni mmoja kati ya mawakili waliokuwa wazalendo na kusaidia watu wenye shida.

No comments: