Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
MATUMAINI yaliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kwamba makali ya mgawo wa umeme yangepungua kwa kiasi kikubwa kuanzia Septemba 7, mwaka huu yamekuwa kinyume chake kutokana na adha ya upatikanaji wa nishati hiyo kuongezeka.
Maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam hayana umeme yapata siku tatu sasa, huku mengine yakipata nishati hiyo mara moja katika muda wa saa 36 na 48.
Ngeleja alitoa ahadi kwamba kungekuwa na nafuu ya mgawo baada ya kuwashwa kwa mitambo ya umeme ya Kampuni ya Symbion na ile ya Aggreko ambayo kwa ujumla wake, ilitarajiwa kuzalisha megawati 137.5.
Hata hivyo, hadi jana jioni mitambo hiyo haikuwa imewashwa hivyo kusababisha maeneo mengi ya Dar es Salaam kuendelea kuwa gizani.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili jana umebaini kuwa baadhi ya maeneo ya yakiwamo Ubungo, Mwenge, Kimara, Temeke, Keko na Sinza makali ya mgawo wa umeme yamezidi huku Tabata kukiwa hakuna umeme kwa siku tatu mfululizo.
Mtendaji Mkuu wa Symbion, Stanley Munai alisema bado hawajaanza uzalishaji licha ua mafuta ya kuwashia mitambo kufika akisema kwanza wameyapeleka kuyapima ili kujua kama yanafaa ama la... “Tunasubiri majibu ili kuona kama yanafaa au hayafai.”
Alisema uamuzi wa kuyapima mafuta hayo umezingatia kwamba mtambo wao utakuwa ukiyatumia kwa mara ya kwanza, hivyo ni lazima yapimwe ili yasije kusababisha tatizo jingine.
“Ukiwasha bila kupima mafuta unaweza kuua mtambo, mafuta huwa tunachukulia katika kampuni ya kuuza mafuta ya BP,” alisema Munai.
Alipoulizwa ni lini mitambo hiyo itawashwa, Munai alisema: “ Muda wowote tu tukishapata majibu, mafuta huwa yanapimwa na kampuni ya SGS au Intertake.”
Alichoahidi Ngeleja Septemba 4
Septemba 4, mwaka huu alipotembelea mitambo hiyo iliyopo Ubungo, Ngeleja alisema makali ya umeme yangepungua kwa kiasi kikubwa akirejea ahadi aliyopewa na Symbion kwamba mitambo yao ingewashwa katika muda huo.
Ngeleja kwa kauli ya kujiamini alikwenda mbali zaidi huku akisisitiza kwamba mpaka kufikia Desemba mwaka huu, uzalishaji wa umeme utafikia megawati 572, hivyo kutamaliza kabisa mgawo wa umeme.
“Mitambo ya Symbion ina uwezo wa kuzalisha megawati 112 ambayo inatumia gesi na mafuta mepesi, mpaka sasa inazalisha megawati 75 tu, megawati nyingine 35.7 za mtambo huu zitaanza kuzalishwa kesho (Septemba 6) au keshokutwa (Septemba 7) baada ya kuwasili kwa mafuta mepesi” alisema Ngeleja.
Alisema kuwa mitambo ya Aggreko ambayo inazalisha megawati 100 utawashwa baada ya kukamilika kwa ufungaji wa baadhi ya vifaa zikiwemo transfoma.
Hii si mara ya kwanza kwa Ngeleja kutoa kauli kama hiyo kwani amekuwa akifanya hivyo na kutoa ahadi ambazo utekelezaji wake umekuwa mgumu.
Mapema mwaka huu, wakati akiapishwa kushika nafasi yake ya Waziri wa Nishati na Madini kwa kipindi kingine, aliutangazia umma kwamba mgawo wa umeme ungekuwa historia lakini wiki hiyo ya kwanza tangu kuapishwa kwake nchi ikatikiswa na mgawo mkubwa.
Alipotafutwa kwa ajili ya kuzungumzia ongezeko la makali ya mgawo, Meneja Uhusiano wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Badra Masoud hakupatikana kwani simu yake ilikuwa ikiita bila majibu ya kupokewa.
Hata hivyo, mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa si msemaji wa alisema Badra alikuwa msibani na kwamba hayupo ofisini mpaka Jumatatu ijayo.
“Badra amefiwa hayupo kwa sasa, ila kuhusu suala la mtambo wa Symbion ungekwenda kuzungumza na haohao Symbion kwa sababu wao wanawauzia umeme Tanesco,” alisema mfanyakazi huyo.
Kuhusu mitambo ya Aggreko alisema mitambo hiyo itawashwa mwezi huu baada ya kukamilika ufundi.
“Unajua kuna upungufu wa megawati 300 katika Gridi ya Taifa kwa hiyo hata zikiwashwa hizo megawati 37.5 za Symbion na megawati 100 za Aggreko bado kutakuwa na mgawo, Waziri Ngeleja alifafanua kuwa mpaka Desemba mwaka huu ndipo mgawo utakwisha kabisa,” alisema mtumishi huyo.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment