Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Sunday, August 7, 2011

Mama Nkurunziza awataka wanawake nchini kuheshimiana

Na Anna Nkinda – Maelezo
07/08/2011 Wanawake nchini wametakiwa kuheshimiana na kupendana huku wakiondoa tofauti zao za elimu na uwezo walionao kwani kila mtu anamuhitaji mwenzake katika utendaji wake wa kazi.
Wito huo umetolea hivi karibuni na Mke wa Rais wa Burundi Dk. Denise Nkurunziza wakati akiongea na wanawake viongozi, wake wa viongozi na wanawake wajasiliamali katika viwanja vya Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza kukagua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa  na wanawake wajasiliamali.

Dk. Nkurunziza ambaye pia ni Mchungaji wa kanisa la juu ya Mwamba aliwapongeza wanawake hao kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwasisitiza kutokudharauliana baina yao kwani kila mtua anauwezo wa kufanya kitu fulani ambacho mwenzake hawezi kukifanya.
“Kila mtu anauwezo wa kufanya kitu fulani, wasomi wanauwezo wa kufanya kitu ambacho yule ambaye hajasoma hawezi kufanya,  ambao hawajasoma nao kuna mambo wanayoyafanya ambayo yule ambaye amesoma hawezi kuyafanya hivyo basi wasomi wanahitaji wale ambao hawajasoma ili waweze kuwasaidia yale ambayo hawayawezi na wale ambao hawajasoma wanahitaji walio na elimu ili wawasaidie katika mambo wasiyoweza kuyafanya”.
“Kazi mnazozifanya ni nzuri na zimenionyesha mamlaka na uwezo wa mwanamke, ninampenda sana mwanamke si kama nampenda kwa kuwa mimi ni mwanamke hapana bali ninajua  kuwa mwanamke anauwezo wa kufanya mambo mengi hakika  nimejinza mambo mengi kwa muda mchache niliokuwa naangalia bidhaa zenu ”, alisema Dk. Nkurunziza.
Aliendelea kusema kuwa ni jambo la muhimu sana kutumia vitu vya asili kwani kuna vitu ambavyo vinapotea kwa kutupwa, vitu ambavyo vingeweza kutengeneza bidhaa mbalimbali na kuahidi kwenda kuonyesha vitu alivyopewa nchini Burundi ili nao waje kununua bidhaa hizo nchini Tanzania.
Akimkaribisha Dk. Nkurunziza ili aweze kuongea na wanawake hao Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alisema kuwa wanawake wa Tanzania ni wazuri sana na si wazuri katika sura pekee bali ni wazuri katika pande zote, wanaupendo na wanajali familia zao, wametengeneza maisha yao na kuyafanya maisha kuwa mazuri zaidi.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alisema kuwa wanawake hao  siyo wanawake waliokaa na kusubiri wanaume zao wawaletee chakula na kulisha familia zao bali ni wanawake wanaojituma na kufanya kazi kwa bidii katika kujiletea maendeleo na kujikwamua na hali ngumu ya umaskini.
“Leo umeona bidhaa nzuri zinazotegenezwa na wanawake wajasiliamali lakini pia wapo wanawake ambao wameshika nafasi mbalimbali za uongozi hapa nchini na nje ya nchi hii ni kuonyesha kuwa wanawake wakipewa nafasi ya kuongoza wanaweza kufanya hivyo”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema kuwa bidhaa zinazozalishwa na wanawake hao ni nzuri na anaamini kuwa zinahitajika nchini Burundi  na kumuomba Mama Nkurunziza aweze kuwatafutia soko la bidhaa hizo kwa kuonyesha vitu ambavyo anakwenda navyo kwa kufanya hivyo atakuwa  balozi tosha kwa kinamama hao.
Alimalizia kwa kusema kuwa hivi sasa kina mama wanatengeneza mifuko ambayo ni rafiki wa mazingira kwa kiasi kikubwa wameachana na tabia ya kutumia mifuko ya plastiki, wanatumia vikapu ambavyo vimetengenezwa na mimea ya asili ambacho kikiharibika na kutupwa  kinakuwa mbolea.
Mama Nkurunziza amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku tano leo ambapo pamoja na kazi mbalimbali za kijamii alizozifanya alishiriki hafla za futari ziliyoandaliwa na Mke wa Rais Mama Kikwete na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamema Shein pia akiwa mjini Zanzibar alitembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria.

No comments: