Mkurugenzi wa Msama Auction Mart anayemiliki pia Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana na kuwalaumu baadhi ya wasanii nchini na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), kwa kutotoa ushirikiano katika vita dhidi ya wanyonyaji wa kazi za wasanii nchini.
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Msama Auction Mart, imewalaumu baadhi ya wasanii nchini na Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA), kwa kutotoa ushirikiano katika vita dhidi ya wanyonyaji wa kazi za wasanii nchini.
Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Msama Auction Mart anayemiliki pia Kampuni ya Msama Promotions, Alex Msama alisema anawashangaa wadau hao kwa kuziba plasta mdomoni kwa kutolizungumzia suala hilo.
Alisema aliamini kutokana na kufanikiwa kuwakamata baadhi ya wanyonyaji na mitambo yao, wangejitokeza kumuunga mkono, lakini hawajafanya hivyo.
'Hakuna hata msanii mmoja anayeniunga mkono, zaidi ya ushirikiano wa dhati ninaopata kutoka kwa Jeshi la Polisi, lakini naamini nitafanikiwa, atakayeutambua mchango wangu atakuja kunishukuru,' alisema Msama.
Msama alieleza kuwa amesambaza zaidi ya vijana 50 nchini kushughulikia tatizo hilo, ambapo sasa wanakamata wanyonyaji wa aina zote za muziki bila kujali maudhui yake.
Aliwataja baadhi ya wanyonyaji waliokwishakamatwa kuwa ni Fred Jumbe, Martin Mkinga, Abdalah Kijemi, Abdallah Salum,Yahya Salum, Razaro John, Amir Kasim, Faraj Amir, Rashid Juma na Mustafa Rashid.
Mpaka sasa kampuni hiyo imefanikiwa kukamata CD feki zenye thamani ya mamilioni ya fedha kutoka kwa wanyonyaji wa kazi za wasanii nchini, hatua iliyokuja baada ya kuwekwa mitego mbalimbali ya kuwakamata wezi hao.
Msama alisema mbali ya kukamata fedha hizo, lakini pia wamefanikiwa kukamata fedha taslimu zaidi ya sh. milioni 10 kutoka kwa wahalifu hao.
Alisema kampuni yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, imefanikiwa kuwatia nguvuni wanyonyaji na wasambazaji wakubwa wa kazi za wasanii zaidi ya wanane, na tayari baadhi yao wamefikishwa mahakamani.
Mbali ya kuwakamata wahusika lakini pia imefanikiwa kukatama mitambo miwili mikubwa ya kudurufu CD yenye uwezo wa kuzalisha CD feki zaidi ya 300 ndani ya dakika 20.
Alisema anaamini kazi ya kulitokomeza tatizo hilo inahitaji ushirikiano wa wadau wote wa muziki, lakini kutokana na kutopata ushirikiano atahakikisha anapambana.
'Ni kazi nzito kuifanya mwenyewe, lakini naamini nitafanikiwa tu, dawa yao nimeshaipata, nitahakikisha napunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa au kulimaliza kabisa,' alisema.
No comments:
Post a Comment