Na Anna Nkinda – Malabo, Equatorial Guinea
01/07/2011 Muungano wa Wake wa Marais wa Afrika wa Kupambana na Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (OAFLA) umetakiwa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 vifo vya kina mama wajawazito na watoto vitakuwa vimepungua katika nchi zao.
Wito huo umetolewa jana na Kamishna wa masuala ya jamii wa Umoja wa Afrika (AU) Bience Gawanas wakati akiongea na wake wa marais wa Afrika katika mkutano mkuu wa kumi uliofanyika mjini Malabo nchini Equatorila Guinea.
Kamishna Gawanas alisema kuwa Afrika ni bara tajiri na limejaliwa kuwa rasilimali za kutosha lakini jambo la kujiuliza ni kwanini vifo vya wanawake wajawazito na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto vinaongezeka kila siku.
“Kwa nini kila siku tupoteze wanawake na watoto kutokana na matatizo haya nyie kama wake wa marais kupitia umoja wenu mnaweza kukabiliana na jambo hili kwa kuhakikisha kuwa hakuna mtoto atakayezaliwa akiwa na maambukizi ya VVU na hakuna mama atakayekufa wakati wa kujifungua.
“Nyie ni sauti ya wanawake na watoto katika jamii mnayotoka, mnauwezo wa kuhakikisha kuwa wako salama kwani kila siku wanazaliwa watoto wakiwa na maambukizi ya VVU huku wanawake wajawazito wakipoteza maisha wakati wa kujifungua”, alisema Kamishna Gawanas.
Aliendelea kusema kuwa ikiwa tatizo la vifo vya wanawake wajawazito na watoto litapungua wanawake watajivuna kuzaliwa katika bara la Afrika na hawatakuwa na fikra kuwa kuchagua kuzaliwa Afrika ni kama kuchagua kifo kwani litakuwa ni bara salama kwao.
Aliyekuwa Rais wa umoja huo mke wa waziri mkuu wa Ethiopia Mama Azeb Zenawi alisema kuwa wao ni sauti za wanawake katika jamii wanaweza kuondoa maambukizi ya VVU na kuhakikisha kuwa hakuna mtoto atakayezaliwa akiwa na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.
Mama Zenawi alisema kuwa wake wa maraisi wanaweza kuwa nguvu ya kupambana na ugonjwa wa Ukimwi kwa kuwawezesha wanawake kiuchumi kwani mwanamke akiwa na pesa ya kutosha ataweza kununua chakula na kupeleka watoto shule na hivyo kujiepusha na mazingira yanayoweza kupelekea kupata maambukizi .
“Moja ya sababu za maambuzi ya VVU ambayo wanawake wanayapata ni kutokuwa na kazi ya kufanya ila kama wanawake watawezeshwa kiuchumi na kuwa na kazi ya kufanya watajiepesha na mazingira hatarishi ya kuambukizwa ugonjwa wa UKIMWI.
Aliendelea kusema kuwa kazi wanayoifanya ni kuhamasisha watu wakiwemo wanawake wajawazito wakapime kwa hiari na kujua afya zao kwani kama mjamzito akijua amepata maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi ni rahisi kumkinga mtoto aliyepo tumboni na hivyo kuzaa mtoto aliye salama..
Wake hao wa marais pia walizindua mpango wa kuharakisha juhudi za kupunguza vifo vya kina mama vitokanavyo na uzazi nchini Equatorial Guinea ambapo hadi sasa katika kila wanawake laki moja wanaojifungua kwa mwaka wanaokufa ni mia tatu hamsini sababu zikiwa ni ugonjwa wa maralia, ukimwi na upungufu wa damu.
Katika mkutano huo pia ulifanyika uchaguzi wa Rais mpya wa umoja huo ambapo Mke wa Rais wa Jamuhuri ya Namibia Mama Penehupifo Pohamba alichaguliwa kuongoza kwa muda wa miaka mitatu.
Mkutano huo ambao ulimalizika jana ulihudhuriwa na wake wa marais kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika akiwemo Mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete.
No comments:
Post a Comment