Ndugu zangu,
NIONAVYO, kuna upepo mgumu wa kisiasa unaovuma sasa kwenye nchi yetu. Ndio, upepo mwingine ni mgumu wenye kutingisha matawi ya miti na hata makoti tuyavaayo. Kamata-kamata hii ya sasa na matumizi ya nguvu ni ishara za upepo mgumu wa kisiasa unaovuma.
Hii ni nchi yetu. Tunaipenda nchi yetu tuliyozaliwa na ndio maana ya kuyaandika haya. Na naamini, kuwa msingi wa haya tunayoyaona ni mapambano ya vyama na makundi katika kuwania kushika mamlaka za dola.
Na katika upepo huu mgumu wa kisiasa uvumao sasa, ni vema tukaongozwa na busara badala ya kuruhusu kuongozwa na hisia zetu. Tufanye hivyo kama kweli tuna mapenzi ya dhati kwa nchi yetu tuliyozaliwa. Maana, tukionacho sasa ni kazi ifanywayo na baadhi ya wanasiasa ya kupandikiza chuki miongoni mwetu.
Na tusiombe chuki hii ikaachwa ikomae, maana, sote, kwa njia moja au nyingine, tutalipa gharama ya ujinga huu wa wanasiasa wa kutanguliza maslahi yao binafsi, ya vyama na makundi yao badala ya yale ya nchi yetu tuliyozaliwa.
Na katikati ya upepo huu mgumu wa kisiasa uvumao sasa tunauona mpambano mkali baina ya chama tawala – CCM na chama kikuu cha upinzani – Chadema. Siasa sasa inafanywa kuwa uhasama badala ya kuwa nyenzo ya kidemokrasia katika kuiendeleza nchi yetu. Katika nchi zetu hizi, na katika upepo huu wa mabadiliko, Serikali ya chama tawala Afrika haina maana ya Serikali inayoongozwa na watendaji wote walio wanachama au wafuasi wa chama tawala.
Hivyo basi, katika mpambano huu, tunaona, kuwa chama tawala, kwa namna moja au nyingine kinapotumia dola katika kuikabili Chadema kinaongeza nyufa za kiuongozi. Huu ni mkakati wa kimakosa na wa hatari sana. Na Mwana-CCM yule Fredrick Sumaye aliyesomea masuala ya Utawala kule Havard Marekani alipata kukitahadharisha chama chake, kuwa kisitumie Serikali kwa maana ya dola kujibu hoja za Chadema, badala yake, CCM ipambane na Chadema kwa hoja za kisiasa majukwaani. Sumaye alikuwa na hoja ya msingi, sina hakika kama wenzake kwenye CCM walimwelewa ipasavyo.
Ndio, tuko sasa kwenye mapambano ya kisiasa ya vyama yenye ushabiki mkubwa bila misingi ya hoja za kisiasa na kutanguliza maslahi ya nchi. Na Afrika ukikuta jogoo wawili wanagombana, basi, hapo hapakosi mashabiki. Na kila shabiki aliyesimama kutazama mpambano wa majogoo hao, ujue, kuwa ana jogoo wake anayemshabikia. Na jogoo anayemshabikia akishindwa pambano, shabiki ataondoka akisononeka. Kuna ambao watakosa hata hamu ya chakula siku hiyo. Kisa? Jogoo wake kagalagazwa!
Na kama jogoo mmoja ni mnene na mwingine ni mwembamba, ujue, kuwa jogoo mwembamba ana mashabiki wengi. Lakini mie ni mmoja kati ya wachache, ambao, kwenye pambano kama hilo, hujitahidi kusimama katikati, hata kama ni kazi ngumu. Nawasilisha.
Maggid,
Dar es Salaam, Juni 9, 2011.
No comments:
Post a Comment