Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Wednesday, June 29, 2011

Vigogo wanane kortini kwa ufisadi

Wafanyakazi wa Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi na pamoja na watumishi wa Manispaa ya Kinondoni wanaotuhumiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka na kutoa taarifa za uongo wakishuka kwenye gari kwenye mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam jana,wakituhumiwa kwa makosa 45.Picha na Michael Jamson.
Waandishi Wetu
VIGOGO wanane wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka 45 tofauti.


Mashtaka ya watendaji hao wa Manispaa ya Kinondoni yamegawanyika katika sehemu kuu mbili ikiwemo kutumia madaraka vibaya pamoja na kutoa taarifa za uongo kwa mkurugenzi wa Manispaa hiyo.
Washtakiwa hao ambao walifikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ni pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Ardhi Manispaa ya Kinondoni, Hamidu Mgaya, Ofisa Mtendaji Kilongawima Mbezi, Wanura Maranda, Mwenyekiti wa mtaa Kilongawima Mbezi, Francis Woiso na Diwani wa kata ya Kunduchi, Patrick Makoyola.

Watuhumiwa hao kwa pamoja walisomewa mashtaka hayo na Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Leonard Swai, ambaye aliieleza mahakama kuwa watuhumiwa hao wamevunja kifungu namba 31 cha kuzuia na kupambana na rushwa kwa kutumia madaraka yao vibaya pamoja na kutoa taarifa za uongo kwa waajiri wao.
Swai alidai mbele ya Hakimu Yohana Yongolo wa mahakama hiyo kuwa, mnamo mwezi Juni na Julai mwaka 2008, watendaji wa hao walitoa taarifa za uongo kwa mkurugenzi wao zikionyesha kuwa eneo ambalo lililopo katika michoro ya mipango miji namba TR.DRG. 1/12/8001 kuwa linamilikiwa na Athumani Mahimbo ambapo walimsajili kwa namba ya eneo 2466 Block L Mbezi.

Swai alidai kuwa watuhumiwa hao walifanya jambo hilo huku wakijua kuwa ni kosa na kwamba mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni asingelikubali hilo endapo angepewa maelezo sahihi.
Wengine waliofikishwa mahakamani hapo na Takukuru ni Anna Macha ambaye ni Ofisa Mipango Miji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mapambano Baseka (Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Kinondoni), Said Waligwah (Ofisa Mtafiti wa ardhi Manispaa ya Kinondoni) na Hamidu Mgaya (Ofisa ardhi manispaa ya Kinondoni).

Swai alidai kuwa watuhumiwa hao walitumia madaraka yao vibaya na kuvunja kifungu cha sheria namba 12(1) cha mwaka 1999 namba nne katika sheria ya michoro ya mipango miji kwa kummilikisha Kheri Mabira eneo walilolisajili kwa namba 2473 lililoko Block L Mbezi.
Swai alidai eneo hilo ni la wazi ambalo lilitengwa na serikali kwa matumizi ya umma.

Watuhumiwa wote walikana na mashtaka hayo na walipata dhamana baada ya wadhamini kukubaliana na masharti waliosomewa na hakimu.
Hata hivyo, watuhumiwa saba kati ya nane ndiyo walifika mahakamani hapo huku Patrick Makoyola akikosekana, ambapo mahakama iliamuru atafutwe na polisi na kufikishwa mahakamani hapo.

Hata hivyo, Hakimu Yongolo alisema kesi hiyo itasomwa tena Julai 26 mwaka huu.

Ugawaji Kinyerezi wapigwa stop
Katika hatua nyingine, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imeiamuru Manispaa ya Ilala kusitisha utaratibu wa ugawaji wa viwanja katika eneo la Kinyerezi hadi hapo itakapotoa uamuzi kuhusu shauri la mgogoro huo lililoko mahakamani hapo.

Amri hiyo ilitolewa jana na Jaji Augustino Shangwa kufuatia ombi lililowasilishwa na wakazi wa Kata ya Kinyerezi ambao ni walalamikaji katika shauri la msingi, kupitia kwa wakili wao, Mathias Kisegu.

Katika shauri lao hoja yao ya msingi ni kwamba hawakushirikishwa katika mchakato wa kupima viwanja hivyo kwenye maeneo wanaodai kuwa ni yao hivyo hakuna makubaliano bali manispaa inatumia ubabe tu.

Akitoa amri hiyo Jaji Shangwa alisema kuwa Manispaa ya Ilala inapaswa kusitisha ugawaji wa viwanja hivyo hadi hapo pande zote mbili zitakaposikilizwa na kutolea uamuzi shauri la msingi.
Hata hivyo, shauri hilo lililotolewa mbele ya upande mmoja wa walalamikaji pekee, baada ya mwakilishi wa upande unaolalamikiwa kutokufika mahakamani hapo.

Kabla ya mahakama kutoa amri hiyo kwa manispaa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kutetea Ardhi ya Wakazi wa Kata ya Kinyerezi Dk Silas Kishaluli alieleza kuwa wameamua kuitumia mahakama baada ya kushindwa kuafikiana na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.
Alidai kuwa juhudi zao za kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kwa lengo la kufikia muafaka wa kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa njia ya majadiliano zilishindikana.

Alisema kuwa kutokana na sababu hiyo wanaiomba mahakama itoe tafsiri sahihi kuhusu hatua zinazokusudiwa kuchukuliwa na mkurugenzi huyo bila ya kuzingatia ridhaa zao na sheria za nchi.


Jaji Shangwa aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 8 mwaka huu ambapo itawakilishwa kwa ajili ya kutajwa. 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala alitangaza mpango wa kupima viwanja katika eneo la Kinyerezi akidai kuwa ni sehemu ya mradi wa viwanja 20,000 vilivyotangazwa na serikali miaka mingi iliyopita kwa lengo la kupunguza uhaba wa viwanja vya makazi katika jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo mpango huo uliibua mgogoro baina yake na wakazi wa eneo hilo kiasi cha kufikia hatua ya kufungua kesi mahakamani wakipinga mpango wa manispaa hiyo kwa madai kuwa hauzingatii taratibu na sheria ya Ardhi.

Imeandaliwa na Felix Mwagara, David Mtewele na James Magai

Mwananchi

No comments: