Waziri wa ustawi wa jamii maendeleo ya vijana wanawake na watoto bi Zainab Omar Mohd |
Na Mwandishi Wetu,Zanzibar
Waziri wa ustawi wa jamii maendeleo ya vijana wanawake na watoto bi Zainab Omar Mohd amewaasa wazazi kutowanyanyasa watoto na kuwaomba waheshimu haki zao za msingi ili wawe wanafamilia na viongozi bora wa baadaye.
Waziri ameyasema hayo leo katika ukumbi wa bwawani mjini Zanzibar alipokuwa akizungumza katika warsha ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo kilele chake hufanyika kila Juni 16 duniani kote.
Katika kuazimisha siku hiyo ujumbe wa mwaka huu umetajwa kuwa ni “kwa pamoja tuchukue hatua za haraka ili kunusuru watoto wa mitaani” ambao wanaonekana kushamiri katika jamii ya Zanzibar.
Akielezea sababu ya ujumbe huo Bi zainab amesema inatokana na kuongezeka kwa watoto hao mitaani ambao chanzo chake kimetajwa kuwa ni pamoja na mifarakano ya ndoa katika jamii.
Aidha Bi Zainab ameipongeza bodi ya watoto hao kwa utendaji kazi wake pamoja na kuchangia shl. Mill.1 ambazo zitasaidia uendeshaji wa bodi hiyo.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo bw. Mshamu Abdallah khamis ameongezea kuwa watoto wana haki zao za msingi ambazo wanapaswa kupatiwa ili watakapokuwa wakubwa waweze kuzisimamia haki hizo kwa wengine.
Katika warsha hiyo ambayo ilihudhuriwa na wawakilishi wa watoto kutoka sehemu mbali za Zanzibar, watoto hao walipata fursa ya kutoa maoni yao kwa serikali ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti katika wizara ya ustawi wa jamii maendeleo ya vijana wanawake na watoto, ambapo wao ni wadau wa wizara hiyo.
Siku ya mtoto wa Afrika ambayo huazimishwa kila ifikapo Juni 16 iliasisiwa kutokana na mauaji ya watoto yaliyofanyika Afika ya kusini katika eneo la Soweto mwaka 1976 kutokana na kudai haki yao ya elimu.
Habari kwa Hisani ya Michuzi Blog
Habari kwa Hisani ya Michuzi Blog
No comments:
Post a Comment