Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, June 2, 2011

Breaking Nuzz.......RAIS WA UTPC AKEMEA JESHI LA POLISI KUMKAMATA MWANDISHI FRANCIS GODWIN

Bloga  Francis Godwin ni mzee wa Matukio Daima

RAIS  wa muungano  wa vyama  vya  waandishi  wa habari nchini (UPTC) Keneth Simbaya amelaani kitendo cha  jeshi la   polisi mkoani Iringa kumkamata mwandishi  wa habari wa gazeti la Tanzania  daima mkoani Iringa Francis Godwin  (pichani)na wakati akifuatilia sakata la mgomo  wa  wanafunzi  wa  shule ya  Sekondari Tosamaganga  wilaya ya Iringa mkoani Iringa.


Simbaya alisema kuwa hatua ya  jeshi la  polisi kumkamata mwandishi  huyo ni   sawa na  kuzuia  uhuru  wa vyombo vya habari nchini katika kuihudumia jamii na  kuwa kitendo cha  polisi  kumkamata mwandishi  huyo kimepokelewa kwa masikitiko makubwa na wanahabari kote nchini.

Alisema  kuwa waandishi  wa habari na jeshi la  polisi ni watu ambao  wanapaswa kufanya kazi  kwa kushirikiano kwani  wote  wapo kwa ajili ya  kuihudumia jamii na Taifa kwa ujumla  hivyo iwapo vyombo  hivyo viwili  vikaingia katika migongano kama  hiyo ni hatua mbaya ambayo haitakuwa na tija  kwa Taifa.

Rais  huyo alitaka  waandishi  wa habari  kuendelea kufanya kazi yao kwa uhuru  zaidi na ushirikiano mkubwa  kutoka kwa vyombo vyote za serikali na  vyombo vya dola bila kubagua  wala kuwepo kwa vitendo vya vitisho kama hivyo.

“..Mwandishi  wa habari yupo kwa ajili ya jamii nzima na ni mdau  wa vyombo  vyote hata  polisi  ... UTPC  kama chombo ambacho kinawaunganisha  waandishi  wa habari kote nchini kupitia vyama vyao tunaendelea  kuomba vyombo vya dola   kuendelea  kujenga mahusiano mema na  kutoa ushirikiano kwa wanahabari badala ya  kujengeana chuki zaidi....UPTC inatoa pole  sana kwa mwanahabari Francis Godwin kwa misukosuko iliyomkuta ila tunamwomba asikate tamaa katika  kuendelea  kuitumikia jamii”

Simbaya alisema  kuwa  UTPC imekuwa  ikipokea taarifa mbali mbali  dhidi ya wanahabari mbali mbali kuendelea  kukamatwa na  jeshi la  polisi mfano mkoani Tarime ,Mbeya ,Kilimanjaro ,Iringa na maeneo mengine jambo ambali ni hatari katika  kutekeleza wajibu  wao na kufanya kazi kwa uhuru  zaidi .

Mwanahabari Godwin alisema  kuwa siku moja kabla ya kukamatwa  kwake akiwa na mwanahabari mwenzake wa kituo cha Radio Ebony Fm walizuiwa na mkuu wa  polisi  wilaya ya Iringa kuendelea  kufuatilia sakata la  FFU  kuwapiga mabomu  wa  wanafunzi  wa sekondari ya Tosamaganga   bila  kuwa na kibali cha  polisi .

Alisema  kuwa kutokana na kiongozi  huyo  wa  polisi wilaya  kuwataka  kuomba kuifanya kazi  hiyo  walilazimika  kuondoka na kwenda kuripoti tukio  la  wanafunzi hao kugoma  katika vyombo vyao .

“ Kabla ya  kuondoka eneo la tukio kijiji cha Mseke mpakani mwa Iringa vijijini na mjini ambako wanafunzi hao  zaidi ya 1000 walitawanywa na FFU kwa mabomu tulipata  kumuuliza mkuu  huyo wa Polisi aina ya vibali ambavyo vinatolewa na  jeshi la polisi kwa  waandishi wa habari  wanapotakiwa  kufuatilia tukio “

Hata  hivyo alisema  siku ya pili ambayo ni jumanne Mai 31 majira ya saa 7.45 akiwa katika  shule ya  sekondari Tosamaganga kufuatilia hali ya mgomo  huo ghafla  alizingirwa na  polisi wa upelelezi ambao  waliziba barabara  na kumshusha katika gari ambayo  ilikuwa na  wanahabari  wengine kwa kudai  kuwa mwandishi  huyo amewachongea askari hao  kwa wanafunzi  hao  zaidi ya 1000 pindi  wakiwa maeneo ya  shule  hiyo majira ya saa 6.30 mchana na kuwa  wamenusurika  kuuwawa na wanafunzi hao jambo ambalo si kweli kutokana na wanafunzi kwa kipindi  hicho walikuwa ndani ya ukumbi na viongozi wa elimu  wakipatanishwa na  walimu  wao.

“Pamoja na madai hayo nilishangazwa  hatua ya askari mmoja ambaye anaitwa Mrisho kwa kuanza  kunitukana matusi ya  nguoni  na kudai kuwa mimi nimejifanya mjuaji na kupitia gazeti la Tanzania  Daima na blogu ya Francis Godwin nimeonyesha tukio la  wao  kuwapiga mabomu  wanafunzi hao na tukio jingine  alilonihusisha ni lile la madai ya  polisi  kudaiwa kumpiga kwa risasi mwanamke mmoja mkazi  wa Don Bosco “

Godwin alisema  kuwa pamoja na askari  huyo Mrisho kutishia kuwa angempiga sana ila hakuweza kufanya  hivyo baada ya  kuwasiliana na wakuu  wake ambao  wamemtaka asinipige wala  kunitesa kwa namna yeyote ile.

Pia alisema baada ya  kukamatwa akiwa eneo la shule  hiyo alipelekwa  kituo  kidogo cha polisi Tosamaganga na baadae kupakizwa katika gari iliyokuwa na askari wa FFU zaidi ya 10 huku wakipiga king’ora  mfano njia nzima na kumfikisha  kituo cha polisi mfano  wa jambazi  sugu amekamatwa  na baada ya kufika mkuu  wao aliagiza mwandishi  huyo kuwekwa mahabusu bila maelezo kwa zaidi ya masaa mawili.

Majira ya saa 12.49 ndipo mwandishi wa habari  za Chanel Ten mkoa  wa Iringa Daud Mwangosi na mwandishi  wa gazeti la Majira mkoa wa Iringa Eliasa Ally  walifika kituoni hapo kwa ajili ya kumwekea dhamana na ndipo mwandishi huyo alipotoa maelezo yake kuelezea mazingira ya kukamatwa japo katika maelezo hayo sehemu ya kosa haikujazwa chochote zaidi ya askari aliyokuwa akichukua maelezo kudai  kuwa kosa ni kuwaonyesha  wanafunzi hao zaidi ya 1000 askari wawili wa upelelezi.

“Nikiwa ndani ya gari ya FFU baadhi ya askari  walikuwa  wakinihoji  ili kujua kama ni mfuasi wa Chadema na  kuwa  wao  walielezwa kuwa nimetumwa na Chadema katika  shule  hiyo huku wengine  wakitoa vitisho  kuwa yaliyompata Jerry Muro na Said Kubenea ndio wanayotaka  kunifanyia mimi”

Godwin alisema kuwa maelezo ya polisi na yale ya kamanda  wa  polisi mkoa kwa vyombo vya habari yalionyesha  kutofautiana baada ya polisi kudaiwa  kuwaonyesha wanafunzi askari  wa upelelezi na kuhatarisha maisha yao huku kamanda  wa  polisi akidai kuwa sababu ya kushikiliwa na polisi ni kuchochea mgomo wa wanafunzi.

“Hata  hivyo nawashukuru wanahabari ndani ya mkoa  wa Iringa kwa  kulishughulikia suala  hilo kwa uzito  wake  pamoja ....pia namshukuru mkuu  wa  polisi wilaya (OCD) Semunyu kwa kuniachia huru na kunitaka  kuendelea na kazi yangu kwa amani”
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kamanda  wa  polisi  wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla alisema  kuwa mwandishi  huyo alikamatwa kwa tuhuma za kuchochea mgomo  wa  wanafunzi  wa shule  hiyo ya  sekondari Tosamaganga.


1 comment:

IPC said...

Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Mkoa wa Iringa (IPC) na Rais wa Muungano wa Vyama vya Waandishi wa Habari Nchini (UPTC), Keneth Simbaya, amelaani kitendo cha jeshi la polisi mkoani Iringa kumkamata mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima mkoani Iringa Francis Godwin wakati akifuatilia sakata la mgomo wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tosamaganga iliyo mkoani Iringa.

Hatua ya jeshi la polisi kumkamata mwandishi huyo ni sawa na kuzuia uhuru wa vyombo vya habari nchini katika kuihudumia jamii na kuwa kitendo cha polisi kumkamata mwandishi huyo kimepokelewa kwa masikitiko makubwa na wanahabari kote nchini.


Waandishi wa habari na jeshi la polisi ni watu ambao wanapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana kwani wote wapo kwa ajili ya kuihudumia jamii na taifa kwa ujumla hivyo iwapo vyombo hivyo viwili vikaingia katika migongano kama hiyo ni hatua mbaya ambayo haitakuwa na tija kwa taifa.


Waandishi wa habari wanapaswa kuendelea kufanya kazi yao kwa uhuru zaidi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa vyombo vyote za serikali na vyombo vya dola bila kubagua wala kuwepo kwa vitendo vya vitisho kama hivyo.


IPC na UPTC inatoa pole sana kwa mwanahabari Francis Godwin kwa misukosuko iliyomkuta ila tunamwomba asikate tamaa katika kuendelea kuitumikia jamii.


Wanachama wa IPC na wanahabari wote wanaofanya kazi zao mkoani Iringa wanapaswa kuonesha mshikamano wao dhidi ya vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa na vyombo vya dola dhidi yao.


Katika kuonesha mshikamano huo, wanahabari hao wataonekana hawana busara kama wataanza kuwanyoshea vidole wanahabari wengine katika kulishughulikia suala la Francis Godwin. Kila mmoja ili mradi yuko katika tasnia hii, huku akitambua kwamba misukosuko kutoka katika dola aliyopata Francis Godwin na wengine wengi akiwemo Raymond Francis wa Ebony FM mwaka jana, inaweza pia kumpata mwanahabari mwingine yoyote yule, anatakiwa kuonesha kwa vitendo jinsi alivyokerwa na suala hili.


Moja ya mambo ambayo wanahabari wanapaswa kuonesha ushiriki wao wa viwango katika mchakato wa uandikwaji wa Katiba Mpya ni kuhusu sheria mpya ya habari, kwasababu kwa kuwa na sheria hiyo wanahabari wanaweza wakawa wamepiga hatua muhimu katika kufanya kazi zao bila kuingiliwa na mamlaka zingine na hasa vyombo vya dola. Kinachotakiwa ni kwa wanahabari kuipitia sheria inayolalamikiwa na ile iliyopendekezwa na wadau ili wazifahamu vizuri kabla ya kushiriki katika mchakato huo wa KATIBA MPYA.


IPC inapeleka pongeza za dhati kabisa kwa Eliasa Alli na Daudi Mwangosi kwa kujitoa kumuwekea dhamana ndugu yetu Francis na wengine wote waliojitoa muhanga kulishughulikia suala hili. Mshikamano kama huu unahitaji kuendelezwa kwa nguvu zetu zote pale maslai yetu ya kikazi yanapoelekea kuhatarishwa kwa makusudi na watu wasioitakia mema tasnia ya habari.


Tunawatakia kazi njema wakati tukiweka mikakati ya kushikamana zaidi.


Asanteni


Nawatakia kila la kheri na kazi njema.