Bloga Francis Godwin ni mzee wa Matukio Daima
RAIS wa muungano wa vyama vya waandishi wa habari nchini (UPTC) Keneth Simbaya amelaani kitendo cha jeshi la polisi mkoani Iringa kumkamata mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania daima mkoani Iringa Francis Godwin (pichani)na wakati akifuatilia sakata la mgomo wa wanafunzi wa shule ya Sekondari Tosamaganga wilaya ya Iringa mkoani Iringa.
Simbaya alisema kuwa hatua ya jeshi la polisi kumkamata mwandishi huyo ni sawa na kuzuia uhuru wa vyombo vya habari nchini katika kuihudumia jamii na kuwa kitendo cha polisi kumkamata mwandishi huyo kimepokelewa kwa masikitiko makubwa na wanahabari kote nchini.
Alisema kuwa waandishi wa habari na jeshi la polisi ni watu ambao wanapaswa kufanya kazi kwa kushirikiano kwani wote wapo kwa ajili ya kuihudumia jamii na Taifa kwa ujumla hivyo iwapo vyombo hivyo viwili vikaingia katika migongano kama hiyo ni hatua mbaya ambayo haitakuwa na tija kwa Taifa.
Rais huyo alitaka waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi yao kwa uhuru zaidi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa vyombo vyote za serikali na vyombo vya dola bila kubagua wala kuwepo kwa vitendo vya vitisho kama hivyo.
“..Mwandishi wa habari yupo kwa ajili ya jamii nzima na ni mdau wa vyombo vyote hata polisi ... UTPC kama chombo ambacho kinawaunganisha waandishi wa habari kote nchini kupitia vyama vyao tunaendelea kuomba vyombo vya dola kuendelea kujenga mahusiano mema na kutoa ushirikiano kwa wanahabari badala ya kujengeana chuki zaidi....UPTC inatoa pole sana kwa mwanahabari Francis Godwin kwa misukosuko iliyomkuta ila tunamwomba asikate tamaa katika kuendelea kuitumikia jamii”
Simbaya alisema kuwa UTPC imekuwa ikipokea taarifa mbali mbali dhidi ya wanahabari mbali mbali kuendelea kukamatwa na jeshi la polisi mfano mkoani Tarime ,Mbeya ,Kilimanjaro ,Iringa na maeneo mengine jambo ambali ni hatari katika kutekeleza wajibu wao na kufanya kazi kwa uhuru zaidi .
Mwanahabari Godwin alisema kuwa siku moja kabla ya kukamatwa kwake akiwa na mwanahabari mwenzake wa kituo cha Radio Ebony Fm walizuiwa na mkuu wa polisi wilaya ya Iringa kuendelea kufuatilia sakata la FFU kuwapiga mabomu wa wanafunzi wa sekondari ya Tosamaganga bila kuwa na kibali cha polisi .
Alisema kuwa kutokana na kiongozi huyo wa polisi wilaya kuwataka kuomba kuifanya kazi hiyo walilazimika kuondoka na kwenda kuripoti tukio la wanafunzi hao kugoma katika vyombo vyao .
“ Kabla ya kuondoka eneo la tukio kijiji cha Mseke mpakani mwa Iringa vijijini na mjini ambako wanafunzi hao zaidi ya 1000 walitawanywa na FFU kwa mabomu tulipata kumuuliza mkuu huyo wa Polisi aina ya vibali ambavyo vinatolewa na jeshi la polisi kwa waandishi wa habari wanapotakiwa kufuatilia tukio “
Hata hivyo alisema siku ya pili ambayo ni jumanne Mai 31 majira ya saa 7.45 akiwa katika shule ya sekondari Tosamaganga kufuatilia hali ya mgomo huo ghafla alizingirwa na polisi wa upelelezi ambao waliziba barabara na kumshusha katika gari ambayo ilikuwa na wanahabari wengine kwa kudai kuwa mwandishi huyo amewachongea askari hao kwa wanafunzi hao zaidi ya 1000 pindi wakiwa maeneo ya shule hiyo majira ya saa 6.30 mchana na kuwa wamenusurika kuuwawa na wanafunzi hao jambo ambalo si kweli kutokana na wanafunzi kwa kipindi hicho walikuwa ndani ya ukumbi na viongozi wa elimu wakipatanishwa na walimu wao.
“Pamoja na madai hayo nilishangazwa hatua ya askari mmoja ambaye anaitwa Mrisho kwa kuanza kunitukana matusi ya nguoni na kudai kuwa mimi nimejifanya mjuaji na kupitia gazeti la Tanzania Daima na blogu ya Francis Godwin nimeonyesha tukio la wao kuwapiga mabomu wanafunzi hao na tukio jingine alilonihusisha ni lile la madai ya polisi kudaiwa kumpiga kwa risasi mwanamke mmoja mkazi wa Don Bosco “
Godwin alisema kuwa pamoja na askari huyo Mrisho kutishia kuwa angempiga sana ila hakuweza kufanya hivyo baada ya kuwasiliana na wakuu wake ambao wamemtaka asinipige wala kunitesa kwa namna yeyote ile.
Pia alisema baada ya kukamatwa akiwa eneo la shule hiyo alipelekwa kituo kidogo cha polisi Tosamaganga na baadae kupakizwa katika gari iliyokuwa na askari wa FFU zaidi ya 10 huku wakipiga king’ora mfano njia nzima na kumfikisha kituo cha polisi mfano wa jambazi sugu amekamatwa na baada ya kufika mkuu wao aliagiza mwandishi huyo kuwekwa mahabusu bila maelezo kwa zaidi ya masaa mawili.
Majira ya saa 12.49 ndipo mwandishi wa habari za Chanel Ten mkoa wa Iringa Daud Mwangosi na mwandishi wa gazeti la Majira mkoa wa Iringa Eliasa Ally walifika kituoni hapo kwa ajili ya kumwekea dhamana na ndipo mwandishi huyo alipotoa maelezo yake kuelezea mazingira ya kukamatwa japo katika maelezo hayo sehemu ya kosa haikujazwa chochote zaidi ya askari aliyokuwa akichukua maelezo kudai kuwa kosa ni kuwaonyesha wanafunzi hao zaidi ya 1000 askari wawili wa upelelezi.
“Nikiwa ndani ya gari ya FFU baadhi ya askari walikuwa wakinihoji ili kujua kama ni mfuasi wa Chadema na kuwa wao walielezwa kuwa nimetumwa na Chadema katika shule hiyo huku wengine wakitoa vitisho kuwa yaliyompata Jerry Muro na Said Kubenea ndio wanayotaka kunifanyia mimi”
Godwin alisema kuwa maelezo ya polisi na yale ya kamanda wa polisi mkoa kwa vyombo vya habari yalionyesha kutofautiana baada ya polisi kudaiwa kuwaonyesha wanafunzi askari wa upelelezi na kuhatarisha maisha yao huku kamanda wa polisi akidai kuwa sababu ya kushikiliwa na polisi ni kuchochea mgomo wa wanafunzi.
“Hata hivyo nawashukuru wanahabari ndani ya mkoa wa Iringa kwa kulishughulikia suala hilo kwa uzito wake pamoja ....pia namshukuru mkuu wa polisi wilaya (OCD) Semunyu kwa kuniachia huru na kunitaka kuendelea na kazi yangu kwa amani”
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kamanda wa polisi wa mkoa wa Iringa Evarist Mangalla alisema kuwa mwandishi huyo alikamatwa kwa tuhuma za kuchochea mgomo wa wanafunzi wa shule hiyo ya sekondari Tosamaganga.
1 comment:
Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Mkoa wa Iringa (IPC) na Rais wa Muungano wa Vyama vya Waandishi wa Habari Nchini (UPTC), Keneth Simbaya, amelaani kitendo cha jeshi la polisi mkoani Iringa kumkamata mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima mkoani Iringa Francis Godwin wakati akifuatilia sakata la mgomo wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tosamaganga iliyo mkoani Iringa.
Hatua ya jeshi la polisi kumkamata mwandishi huyo ni sawa na kuzuia uhuru wa vyombo vya habari nchini katika kuihudumia jamii na kuwa kitendo cha polisi kumkamata mwandishi huyo kimepokelewa kwa masikitiko makubwa na wanahabari kote nchini.
Waandishi wa habari na jeshi la polisi ni watu ambao wanapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana kwani wote wapo kwa ajili ya kuihudumia jamii na taifa kwa ujumla hivyo iwapo vyombo hivyo viwili vikaingia katika migongano kama hiyo ni hatua mbaya ambayo haitakuwa na tija kwa taifa.
Waandishi wa habari wanapaswa kuendelea kufanya kazi yao kwa uhuru zaidi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa vyombo vyote za serikali na vyombo vya dola bila kubagua wala kuwepo kwa vitendo vya vitisho kama hivyo.
IPC na UPTC inatoa pole sana kwa mwanahabari Francis Godwin kwa misukosuko iliyomkuta ila tunamwomba asikate tamaa katika kuendelea kuitumikia jamii.
Wanachama wa IPC na wanahabari wote wanaofanya kazi zao mkoani Iringa wanapaswa kuonesha mshikamano wao dhidi ya vitendo vya udhalilishaji vinavyofanywa na vyombo vya dola dhidi yao.
Katika kuonesha mshikamano huo, wanahabari hao wataonekana hawana busara kama wataanza kuwanyoshea vidole wanahabari wengine katika kulishughulikia suala la Francis Godwin. Kila mmoja ili mradi yuko katika tasnia hii, huku akitambua kwamba misukosuko kutoka katika dola aliyopata Francis Godwin na wengine wengi akiwemo Raymond Francis wa Ebony FM mwaka jana, inaweza pia kumpata mwanahabari mwingine yoyote yule, anatakiwa kuonesha kwa vitendo jinsi alivyokerwa na suala hili.
Moja ya mambo ambayo wanahabari wanapaswa kuonesha ushiriki wao wa viwango katika mchakato wa uandikwaji wa Katiba Mpya ni kuhusu sheria mpya ya habari, kwasababu kwa kuwa na sheria hiyo wanahabari wanaweza wakawa wamepiga hatua muhimu katika kufanya kazi zao bila kuingiliwa na mamlaka zingine na hasa vyombo vya dola. Kinachotakiwa ni kwa wanahabari kuipitia sheria inayolalamikiwa na ile iliyopendekezwa na wadau ili wazifahamu vizuri kabla ya kushiriki katika mchakato huo wa KATIBA MPYA.
IPC inapeleka pongeza za dhati kabisa kwa Eliasa Alli na Daudi Mwangosi kwa kujitoa kumuwekea dhamana ndugu yetu Francis na wengine wote waliojitoa muhanga kulishughulikia suala hili. Mshikamano kama huu unahitaji kuendelezwa kwa nguvu zetu zote pale maslai yetu ya kikazi yanapoelekea kuhatarishwa kwa makusudi na watu wasioitakia mema tasnia ya habari.
Tunawatakia kazi njema wakati tukiweka mikakati ya kushikamana zaidi.
Asanteni
Nawatakia kila la kheri na kazi njema.
Post a Comment