Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Sunday, May 1, 2011

TANZANIA YAPIGIA DEBE MATUMIZI YA KISWAHILI UMOJA WA MATAIFA


Katibu Mkuu Msaidizi Bwa. Kiyo Akasaka anayeongoza Idara ya Habari na Mawasiliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa, akiwasilisha Taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuhusu shughuli na utendaji kazi wa Idara hiyo, wakati wa mkutano wa 33 wa Kamati ya Habari ya Umoja wa Mataifa. Kulia kwake ni Balozi wa Antonio Pedro Moteiro Lima, mwakilishi wa Cape Verde katika Umoja wa Mataifa. Katika Mkutano huo, Tanzania iliisitiza kuongezwa kwa idadi ya wafanyakazi katika Radio ya Idhaa ya Kiswahili ya UM, idhaa hiyo imeelezwa kuwa licha ya kuwa na wafanyakazi wachache lakini imekuwa chombo muhimu cha mawasiliano katika utoaji wa usambazaji wa taarifa zinazohusu Umoja wa Mataifa na imejipatia umaarufu umeongezeka

Tanzania imeitaka Idara ya Habari na Mawasilliano ya Umma ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa inaongeza idadi ya waandishi katika Idhaa ya Radio ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa ili iweze kutekeleza kwa ukamilifu majukumu yake ya ukusanyaji, utoaji na usambazaji wa taarifa zinazohusu shughuli za umoja huo.
Tanzania imetoa wito huo wakati wa mkutano wa 33 wa Kamati ya Habari ya Umoja wa Mataifa, ambapo pamoja na mambo mengine Kamati hiyo iliyoanzishwa mwaka 1978 ikiwa na wajumbe 113 kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, walipokea na kujadili taarifa ya katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, kuhusu utendaji wa Idara hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Afisa Ubalozi Mwandamizi, Bibi Maura Mwingira amesema katika mkutano huo, kwamba Tanzania inafarijika na kuridhishwa na namna ambavyo lugha ya Kiswahili kupitia Radio ya Kiswahili ya UM imeendelea kuwa kiungo mkuhimu cha mawasiliano, kupata umaarufu na kuongeza idadi ya watumiaji wa taarifa za idhaa hiyo licha ya kwamba ina wafanyakazi wachache.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa UM iliyowasilishwa kwa wajumbe na Katibu Mkuu Msaidizi anayeongoza Idara ya Habari, Bw. Akito Akasaka, imeonyesha kuwa , katika eneo la Radio ya Umoja wa Mataifa, Radio hiyo ambayo hutoa taarifa zake katika lugha sita rasmi za UM, na lugha mbili za Kiswahili na Kireno, imekuwa na mafanikio makubwa ambayo pia yamehusisha ongezeko la watumiaji wa taarifa zake.
Lugha rasmi za Umoja wa Mataifa ni, Kiingereza, Kifaransa, Kiaarabu, Kirusi, Kichina na Kihispania
Kwa upande wa Idhaa ya Kiswahili Bw. Kiyo Akasaka amesema, Radio hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2006, watumiaji wa taarifa za idhaa hiyo imepanda kutoka asilimia moja wakati wa kuanzishwa kwake hadi kufikia asilimia 21, ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa Radio Maarifa FM iliyoko Tanzania.
“ Haya si mafaniko madogo, ni mafanikio makubwa ambayo kila mmoja wetu anapashwa kujivunia na tunawapongeza wafanyakazi hao wawili kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya”. Akasisitiza Afisa Ubalozi.
Idhaa hiyo ambayo inawafanyakazi wawili tu, ikilinganishwa na idhaa nyingine ambazo zinawafanyakazi zaidi ya wanne.Inaongozwa na Mtanzania Bi Flora Nducha. Ni kutokana na uchache huo wa wafanyakazi, ndio maana Tanzania imeitaka sekretarieti ya Idara hiyo ya Habari ya Umoja wa Mataifa kuangalia uwezekano wa kuongeza wafanyakazi .
Tanzania imewaeleza wajumbe wa Mkutano huo kuwa Lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 katika eneo la Afrika ya Mashariki , Afrika ya Kati na nje mipaka ya ya maeneo hayo, imekuwa chombo na kiungo muhimu sana cha upashanaji wa habari hususani katika udhibiti wa migogoro na ujenzi wa amani.
Ni kutokana na umuhimu wa lugha hiyo, Tanzania imesema, ndio maana Umoja wa Afrika uliamua kwa makusudi kabisa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa kati ya lugha rasmi za Umoja huo.
Tanzania ikasisitiza kwa kusema kuwa kila mmoja anafahamu nvugu ya habari. Na kwa sababu hiyo,Kiswahili kina nafasi ya kutoa mchango mkubwa katika kufikisha ujumbe na kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja.
“Kiswahili ni lugha muhimu sana kama chombo cha mawasiliano katika Umoja wa Mataifa, na katika suala zima la ulinzi, usalama na ujenzi wa amani na maendeleo. Tunatambua changamoto ya ufinyu wa bajeti inayoikabili Idara ya Habari na Umoja wa Mataifa kwa ujumla wake. Lakini bado tunaamini kwamba mtafikiria suala la kuongeza idadi ya wafanyakazi katika idhaa hiyo hivi karibuni.” Akasisitiza Afisa Ubalozi Mwandamizi
Na kuoongeza kuwa Tanzania inaamini kuwa kwa kuongeza idadi ya waandishi katika idhaa hiyo, siyo tu kutaboresha kiwango na ubora wa habari zinazotolewa, kuwafikia watu wengi zaidi, lakini kitawapunguzia mzigo wa kazi wafanyakazi waliopo sasa.
IMETOLEWA NA UBALOZI WA TANZANIA KATIKA UMOJA WA MATAIFA
 Habari kwa Hisani ya Issa Michuzi


No comments: