Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Saturday, April 9, 2011

vodacom yamwaga madawati shule ya msingi darajani - zanzibar

Na Nafisa Madai, MAELEZO Zanzibar

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amani, imesema zaidi ya wanafunzi 30,000 Visiwani Zanzibar wanakaa chini darasani kutokana na ukosefu wa madawati.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 100 yaliyotolewa na Kampuni ya Vodacom kwa Shule ya Darajani Mjini Unguja, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mwanaid Saleh alisema idadi hiyo ni kubwa na juhudi zinachukuliwa kuondokana na tatizo hilo.

“Vijana wetu wengi bado wanakaa chini madarasani, hivi sasa kwa Zanzibar nzima tunahitaji madawati yasiyopungua thelathini elfu” Alisema Katibu Mkuu huyo na kuziomba Taasisi kusaidia.

Msaada huo wa madawati kutoka Vodacom wenye thamani ya shilingi milioni 10 umeelezwa umetolewa wakati muafaka ambapo shule nyingi zinakabiliwa na uhaba wa madawati.

Katibu Mkuu huyo alisema kwamba madawati yaliyotolewa yatatosheleza mahitaji ya Shule hiyo yenye wanafunzi

wasiopungua 2,100 ambapo wanafunzi 300 watafaidika na madawati hayo.

Aidha aliwataka wanafunzi kuhakikisha wanayatunza madawati hayo ili wadhamini hao na wengine wawe na moyo wa kusaidia zaidi.

Mkurugenzi wa huduma za jamii kutoka Vodacom, Mwamvita Makamba alisema kampuni yake inajali sana maendeleo ya jamii katika kila sekta na ndio maana imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii kwa faida itokanayo na Kampuni hiyo ikiwa ni mrejesho kwa wananchi.

Mwamvita alisikitishwa na hali duni ya Shule ya Darajani ya ukosefu wa madawati na vifaa vyengine ambapo alitoa ahadi ya jamii kuisadia.

“Tuliahidi kusaidia madawati 300, lakini kutoka na hali kuwa mbaya katika shule hii kama kampuni tumelazimika kuleta haya madawati 100 kwanza mpaka hali itakaporuhusu muda si mrefu tutakuja tena kumalizia madawati 200 yaliyobaki” Aliahidi Mkurugenzi huyo.

Katika risala ya walimu wa Shule hiyo iliyosomwa na Mwalimu Asha Abdallah alisema Shule ya Darajani inahitaji misaada ya vitabu na vifaa vya maabara.

Mwalimu Asha alisema kwa kuwa Shule ya Darajani ni ya Msingi na Sekondari, inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo wanafunzi kusoma katika mazingira magumu hasa somo la sayansi ambalo linahitaji vifaa vya kujifunzia kwa vitendo.

Shule ya Darajani ni moja ya Shule yenye historia ndefu katika Tasnia ya elimu Visiwani Zanzibar ambayo ilianza kutoa wanazuoni mapema zaidi.

Itakumbukwa kuwa nchi nyingi zimetakiwa ifikapo mwaka 2015 ziwe zimetimiza malengo ya milenia katika sekta ya elimu kuhakikisha kila mtoto aliyetimiza umri wa kwenda shule anapata haki ya elimu.

No comments: