Saturday, April 9, 2011
Hoja ya Mdau kuhusu tiba ya jero kile kwa Babu Ambilikile
Tangu kuibuka kwa Babu wa Loliondo na dawa yake ya 'maajabu', ambayo inatibu ugonjwa wowote na ambayo haina gharama kubwa zaidi ya ya kusimama muda mrefu kwenye foleni ukisubiri zamu yako ya kupata kikombe, nimekuwa nikipata wakati mgumu sana mtu anaponiuliza iwapo dawa hiyo inatibu au la. Nimekuwa nikipata wakati mgumu kwa sababu awali ya yote dawa hiyo haijafanyiwa utafiti wa kisayansi lakini pia hakuna sayansi iliyo juu ya miujiza ya Mungu. Babu wa Loliondo ameoteshwa juu ya dawa hii kwa hivyo siwezi kusema kwa hakika iwapo inaponya ama la. Pia hajatokea mtu ambaye naweza kuthibitisha kwa asilimia 100 kwamba amepona.
Lakini swali kubwa kabisa ambalo nimekuwa nikijiuliza ni hili, "Kama dawa hii si dawa mbona watu wameelekea Lolindo kwa makumi ya maelfu?" Wakati swali hili likiendelea kuzungukazunguka ubongoni mwangu nikagongana na makala hii kwenye mtandao, "Placebos Work - Even if Patients are in On the Secret". Tafsiri rahisi ya kichwa hiki cha habari ni hii, "Dawa Bandia Zinafanya Kazi - Hata Mgonjwa anapoambiwa kwamba Anapatiwa Dawa Bandia".
Makala hii iliandaliwa na Maureen Salmo wa gazeti la News Day. Maureen anasema alipofanya uchunguzi wake kuhusu nguvu ya madawa bandia kutibu magonjwa aligundua kwamba hata mgonjwa alipokuwa akielezwa kwamba anachopatiwa ni dawa bandia mgonjwa huyo bado alionesha kupata nafuu kubwa baada ya kutumia dawa hizo bandia, wapo waliopona kabisa.
Akipitia utafiti ambao ulijumuisha wagonjwa 80 waliokuwa wakisumbukiwa na vidonda vya tumbo aliona kwamba wagonjwa wahawa waligawanywa katika maundi mawili. Kundi la kwanza wakaelezwa wazi kwamba walichokuwa wakipatiwa kama tiba hakikuwa dawa halisi ya kutibu ugonjwa wao na lili kundi lingine halikupatiwa tiba kabisa. Baada ya majuma matatu kundi lile liliopatiwa dawa bandia walisema wamekuwa wakijisikia nafuu kubwa tofauti na wale ambao hawakutibiwa kabisa.
Maureen pia alithibitishiwa na Dr. Ted Kaptuchuk wa Chuo Kikuu cha Utabibu cha Havard, ambaye aliendesha utafiti huu, kwamba wale waliopatiwa dawa bandia sio tu kwamba walikuwa wakijisikia nafuu lakini vipimo vya hospitali vilionesha kwamba ugonjwa wao ulikuwa unatoweka kama vile ambavyo ungetoweshwa na dawa halisi.
Utafiti huu uliofanyika mwaka 2008 ulionesha kwamba nchini Marekani karibu asilimia 50 ya madaktari, kwa siri, huwapatia wagonjwa wao, wasiofahamu, dawa bandia.
Dr. Kaptuchuk anasema uchunguzi wake ulidhamiria zaidi kutazama nguvu ya dawa bandia kwa wagonjwa ambao wanaelezwa awali kwamba wanapatiwa dawa bandia, na sio kuwapatia dawa hizo kwa siri. Tafiti nyingi kabla ya huu wa daktari huyu zimethibitisha kwamba dawa bandia zimekuwa zikitibu magonjwa ya wagonjwa wasiofahamu kwamba wanapatiwa dawa bandia. Kufanya kazi kwa dawa hizi kunaitwa kwa kimombo, "Placebo Effect".
"Tulipokuwa tukifanya utafiti huu hatukutegemea matokeo haya. Tulitegemea kwa sababu wagonjwa wetu wanafahamu kwamba wanapatiwa dawa bandia basi hali zao zingekuwa mbovu zaidi. Lakini imekuwa kinyume, imetushangaza sana." Anasema Dr. Kaptuchuk.
Daktari huyu anaendelea kufafanua kwamba kabla ya kuwapatia wagonjwa wao dawa hizo bandi (Placebo) waliketi nao na kuwaeleza kinagaubaga kwamba dawa wanazokwenda kuwapatia hazina hata chembe moja ya kemikali, na hawakuishia hapo, hata chupa iliyokuwa imebeba vidonge hivyo iliandikwa kwa herufi kubwa (PALCEBO), pia waliwafahamisha wagonjwa kwamba dawa hizo zina nafasi kubwa ya kutoleta tofauti yeyote kwa ugonjwa wao.
"Baadhi ya wagonjwa waliona kama tunapoteza muda wao, wako waliofurahia majario haya, lakini mwisho wa siku wote walifurahia matokeo ya utafiti wetu. Walijiona kama watu waliojaa miujiza ndani yao" Anasema Kaptchuk.
Mwisho wa utafiti wake Dr. Kaptchuk akaja na dhana kwamba kitendo cha mgonjwa kupatiwa na kumeza kidonge - hata kile cha bandia - kunafungua vimelea katika ubongo wake ambavyo vinakwenda kupambana na pale anapodhani kuna maradhi.
"Suluhu za matatizo yote yanayotukabili binadamu, yawe ya ndani au nje ya miili yetu, ziko kwenye ubongo wetu" Anasema Kaptchuk, "Hisia zetu mbaya kama vile wivu wa kupindukia, huzuni zetu, woga wetu, ndio hasa chimubuko la karibu kila ugonjwa unaoufahamu huku duniani".
Kwa hivyo, kila tunapotazama watu kama Babu wa Loliondo au Dada wa Tabora, au yule dogo wa kule Mbea, ambao wote wanasema wameoteshwa na Mungu kutupatia tiba za vikombe, huenda watu hawa wamepata elimu juu ya PALCEBO bila wenyewe kujua, na pengine kwa sababu hawana muda wa kutueleza kwa kina au kutuaminisha kwamba dawa zao zinatibu nadhani ni vyema kuwapa muda ili tuone kwanza matokeo ya tiba zao kabla ya kuwahukumu kwa ama dawa zao hazifanyi kazi au zinafanya. Huu ni mtazamo wangu.
Wikiendi Njema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment