Na Nova Kambota,
Hakuna ubishi kuwa kauli yenye utata ya mwenyekiti wa CCM JakayaKikwete ya kukitaka chama chake kufanya kile kinachoitwa ‘kujivua gamba’ inazidi kukibomoa chama hiko kikongwe zaidi nchini, naaita kauli yenye utata kufuatia tafsiri isiyoeleweka ya kauli hiyo ambayo kwa wachambuzi wengi wa kisiasa wanadai kuwa iwe kwa kutoelewa au kwa kudhamiria watu mbalimbali ndani ya chama hiko wanaataka kuitumia kauli hiyo kupakanaa matope kama sio kufanyiana michezo ya kimafia ya siasa za majitaka.
Baada ya kauli hiyo ilifuatiwa na tamko la UVCCM mkoa wa Pwani ambapo kati ya mambo yalitamkwa ni kuwa viongozi wastaafu yaani Sumaye na Lowassa waache rafu zao za kuutaka urais, akisoma tamko hilo Abdalah Ulega hakusita kkubainisha kuwa vigogo hao wasahau ndoto ya urais kwa madai kuwa tayari Kikwete ana jina la mrithi wake, baada ya hilo Umoja wa vijana taifa chini ya Benno Malissa nao ukakaa na kupigilia msumari kwenye lakini katika hiko kikao tunaelezwa kuwa mjumbe mmoja kutoka Arusha Bw Mrisho Gumbo aliweka wazi kuwa ni lazima wale wote wanaohusika na tuhuma za ufisadi wang’olewe kwenye chama.
Ndani ya mbilinge hii pia akaibuka Fredrick Sumaye akajibu mapigo akiwataka vijana hao kuacha kutumiwa, wakati huhuo huko Tabora lingine likazuka la Robert Kamoga mwenyekiti wa UVCCM mkoani humo kumng’oa mlezi wao Bw Samwel Sitta lakini wenzake wakajitokeza na kupinga uamuzi huo, kabla hali ya mambo haijakaa sawa UVCCM Arusha wakatangaza kumwondoa Mrisho Gumbo ambaye na yeye hata hivyo ameongea kwa msisitizo kuwa UVCCM Arusha hawana ubavu huo na huko Iringa nako kumeibuka kundi lingine la UVCCM linalotaka viongozi wa umoja huo taifa wang’olewe kwa madai kuwa hawana mwelekeo na hawana msaada kwa chama chao., hii ndio hali ya UVCCM kwa sasa.
Hii ina maana gani katika zama hizi za CCM kujivua gamba? Hakika ni vigumu hata kubaini haswa gamba analozungumzia mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete ni lipi? Ndani ya CCM kuna makundi yanasigana huku moja likiwa linapinga ufisadi na lingine ingawa halijatamka wazi kuwa linaunga mkono ufisadi lakini kwa jinsi lisivyokemea ufisadi tafsiri yake ni kuwa linaunga mkono ufisadi. Kwa mantiki hii sasa ni kuwa Kikwete anaposema kujivua gamba kila kundi linatafsiri yake, kwa kila kundi linaamini kuwa kundi pinzani ndio gamba linalotakiwa kuvuliwa nah ii ndio imepelekea vuguvugu hili kuikumba hata UVCCM nah ii ni lele tu ngoma yenyewe inakuja kwani kuna kila dalili kuwa hali hii itavamia hata umoja wa wanawake wa chama hiko na pia jumuia ya wazazi wa chama hiko nko huko kote hali inatajwa kuwa si punde itakuwa ni mwendo wa kujivua gamba kama ilivyo UVCCM.
Kwangu mimi na imani kuwa ni vigumu kusema gamba ni nani ndani ya chama hiko? Kama ni mafisadi sasa mbona hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi ni wanachama watiifu wa CCM? Tena baadhi yao wapo kwenye kamati kuu ya chama hiko? Na kama ni wapinga ufisadi mbona baadhi yao ni mawaziri? Tena nao ni wajumbe wa kamati kuu? Kwa muktadha huu ni sahihi kusema kuwa gamba limeshikamana na ngozi je wataweza kujivua? Lakini tukigeukia upande wa pili ambao ni UVCCM nao kwa mbali naona kuwa wamejiingiza kwenye mgogoro usiowahusu, kwangu mimi UVCCM ni sehemu muhimu ya CCM, tofauti na wachambuzi wengine wanaodai kuwa UVCCM haina chochote ni jumuia tu naomba nitofautiane nao ni kweli UVCCM ni jumuia tu lakini sio huko walipotoka kina Kikwete au Sumaye enzi hizo ikiitwa TANU youth League? Kwa maana nyingine UVCCM ni chombo na kiungo muhimu kwa uhai wa CCM na ndio maana hata wanaotaka kuupata urais wameanza na UVCCM kabla ya jumuia nyingine ndani ya chama hiko.
Lakini swali la msingi ni je UVCCM ni gamba au ngozi? Kama gamba basi ivuliwe na kama ngozi itunzwe, pia ni vigumu kusema moja kwa moja kuwa UVCCM ni ngozi au gamba. CCM wakifumba macho na harakaharaka tu wakadai kuwa UVCCM ni gamba basi ivuliwe naomba niwape angalizo kuwa sio kila anayevaa shati la kijani anakipenda chama hiko na sio kila mwanaUVCCM kweli yupo tayari kudhalilika kwa hoja ya uamuzi wa chama wasije kujidanganya kwa kuifuta jumuia hiyo kirahisirahisi,napenda kuwaonya kuwa baadhi yao vijana hao watageuka wapinzani wakubwa wa CCM hakuna ubishi kuwa hata Makamba na Kikwete wanafahamu siri nzito za chama walizonazo vijana hao kwenye mioyo yake na bila shaka kwa mantiki hii CCM wanaweza kukisia athari za vijana hao kugeuka wapinzani na hata mkurugenzi wa propaganda wa CCM Tambwe Hizza anaweza kubashiri kitakachowapata chama chake 2015 kama vijana hao watageuka wapinzani!
Na iwapo CCM wakajifanya kufumba macho kwa kulea kinachoendelea ndani ya UVCCM na kuifananisha jumuia hiyo na ngozi hivyo kuitunza tu bila shaka watakuwa wanajidanganya, itakuwa ni kama kujipalia makaa ya moto kwani hakuna ubishi kuwa UVCCM haijui majukumu yake na haijui ifanye nini, imechoshwa na makundi na minyukano ya kisiasa, imepigwa ikapigika sasa imeamua kuishi kwa mwongozo wa vigogo na sio kwa katiba inayoongoza jumuia hiyo kwa maana nyingine haileleki hata kidogo kwa mazingira ya sasa hivyo si sahihi pia kuiita ngozi basi UVCCM ni nini?
Kwa jinsi hali ilivyo na ikizingatiwa umuhimu mkubwa wa jumuia hiyo kama nilivyoeleza hapo awali basi ni sahihi sasa kusema kuwa UVCCM sio ngozi bali ngozi yenye chunusi na mabaka, sasa nini kifanyike ili kutibu chunusi na mabaka haya kuifanya ngozi hiyo kuwa nzuri, jibu ni rahisi ila kutimiza mahitaji ya jibu si jambo rahisi, CCM haipaswi kukaa kimya katika timbwili hili ni laziima ionyeshe ubaba wake na ni lazima ionyeshe kuwa UVCCM ipo chini ya CCM na siyo CCM chini ya UVCCM lakini hili sifanyike kwa nia ya kuonyeshana ubabe bali lifanyike kwa busara kubwa tena kwa uadilifu ili lizae matunda hakuna ubishi kuwa imefika wakati sasa viongozi wote wa UVCCM waliotekwa na makundi wapigwe chini ! na kuwekwa vijana wanaojua jukumu lao kubwa ni kuisaidia CCM kwa mema siyo kwa mabaya kama kuunga mkono ufisadi, imefika sehemu ya kufumba macho na kuinua panga kukata kidole kilichoanza kuoza maana kikiachwa mkono wote utaoza.
Na hili halipaswi kuishia ndani ya UVCCM bali liende mpaka huko CCM kwenyewe kwa maana haiingii akilini kuona UVCCM inasafishwa halafu CCM inaendelea na mwenendo wake ambao si salama hata kidogo, CCM inapaswa ijipambanue iwapo inaunga mkono ufisadi kwa maana hao ndio wenye hela wanaweza kuwa wafadhili wazuri na wakubwa au pia ijipambanue kuwa inapinga ufisadi na kwa hapa kabla hawajaamua niwakumbushe kuwa wananchi wanapinga ufisadi na zaidi wananchi ndio wapiga kura hivyo kwangu mimi naona ni busara na salama kwa chama hiko kujipambanua kimaneno na kimatendo kuwa kinapinga ufisadi kwa kuwaengua kabisa wahusika wote wa ufisadi na hapo ndio haswa CCM itakuwa imejivua gamba kinyume na hili ni porojo na makidamakida tu….Tafakari!
1 comment:
Nikitumia usemi ambao Makwaiya wa Kuhenga hupenda kutumia ni " HAYA MANENO NI MAZITO SANA" na kama hao wanaojiita viongozi wa nchi hawatatafakari vya kutosha na kuyafanyia kazi basi watalipa gharama ya kutofanya hivyo siku si nyingi zijazo.Nova Kambota, nikupongeze sana kwa kuelimisha UMMA nami nasema "Mwenye sikio na asikie neno hili ambalo UMMA unawaambia Viongozi hasa wale MAFISADI". Nachelea kusema kuwa Wasomi wa nchi hii tuna kazi kubwa ya kufanya kwa UMMA wa Watanzania.Ni vyema tukaiendeleza kazi hii ambayo Kambota ameonyesha kwa kiasi.Lazima tuikomboe nchi yetu toka mikononi mwa hawa wezi ambao wanaiba bila huruma hali wakijua hapa ndipo walipoazaliwa na waathirika ni ndugu zao. Wakoloni wasingekuwa na Huruma kwani hawakuwa na hisa zozote lakini hawa ambao ni wazawa na bado wanafanya mambo ya ajabu kiasi hiki ni vyema tukawaondosha mapema madarakani kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Mungu Ibariki Tanzania.
Post a Comment