Wednesday, June 8, 2016
MBEYA KUKAMILISHA MADAWATI JUNI 20 MWAKA HUU.
MKUU WA Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema zoezi la utengenezaji wa madawati kwa Mkoa wa Mbeya litakamilika Juni 20 mwaka huu badala ya Juni 30 iliyowekwa na Rais Dk. John Magufuli kutokana na kasi nzuri inayoendelea.
Makalla alisema hayo katika ziara ya kukagua na kukabidhi Madawati yanayotengenezwa na Karakana ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ambapo alisema licha ya Rais kutoa muda hadi Juni 30 lakini kama Mkoa lazima umalize mapema na kuwa Mkoa wa Kwanza kumaliza tatizo la madawati.
Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mbarali, Makalla alisema pamoja na zoezi la utengenezaji kwenda vizuri lakini madawati wanayotengenezwa yako kwenye viwango vya juu na imara hivyo kuwa mfano kwa Halmashauri zingine.
“Mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, nimeridhishwa na kiwango cha ubora wa madawati yenu, huyu mkandarasi wenu anafaa hata kufanya kazi zinazohusu Mkoa madawati yake ni imara namazuri hivyo jitahidi kuongeza kasi kabla ya Juni 20 yawe tayari” alisema Mkuu wa Mkoa.
Aidha katika ukaguzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla alikabidhi madawati 62 kwa Shule ya Msingi Jangurutu iliyopo katika Kata ya Rujewa ambayo ilikuwa na upungufu wa madawati 62 hivyo kuondokana na tatizo hilo kabisa.
Akikabidhi madawati hayo, Makalla alitoa wito kwa Wanafunzi kuyatunza ili kuepuka kuwa na madawati mabovu na kwamba kama kunatokea mahitaji mengine yatokane na ongezeko la Wanafunzi na sio kuwa mabovu.
Alisema ni vema kila dawati likaandikwa kulingana na darasa lake ili kuepuka kuhamisha hamisha madawati kutoka darasa moja kwenda lingine jambo linaloweza kuchangia uharibifu wa madawati.
Awali akisoma taarifa ya utengenezaji wa Madawati kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Kaimu Afisa Mipango wa Wilaya, Edmund Kishimbo alisema hadi sasa ni madawati 2987 yako katika hatua mbali mbali za ukamilishaji na usambazaji kwenye shule tofauti ambapo tayari madawati 1022 yamepelekwa mashuleni.
Aliongeza kuwa Halmashauri ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa madawati 5010 lakini juhudi mbali mbali zimefanywa ili kuhakikisha idadi hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa ambapo Mkandarasi Luka Edward kutoka kampuni ya Mkwawa woodwork anafanya kazi kwa saa 24.
Aliongeza kuwa Mkandarasi ameongeza muda wa kufanya kazi katika Karakana ya Halmashauri kutoka saa 12 hadi 24 na hivyo kuongeza uzalishaji wa madawati kutoka 90 hadi 180 kwa siku kutokana na uwepo wa Jenereta kubwa la kufua umeme ili kukabiliana na changamoto ya kukatika katika kwa umeme.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment