Silaha mbalimbali zilizo kamatwa katika tukio la kuuwawa kwa majambazi wilayani Chunya mkoani Mbeya Aprili 27 mwaka huu.
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya
limefanikiwa kuwaua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika
majibizano ya kurushiana risasi wakiwa katika majaribio ya kufanya uhalifu
kwenye duka la Bia la Jumla.
Akizungumza na waandishi wa
Habari ofisini kwake, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo,
alisema tukio hilo lillitokea juzi majira ya saa mbili usiku katika kijiji cha
Matundasi Wilaya ya Chunya Mkoani hapa.
Mwambelo alisema siku ya tukio
majambazi hao walikuwa watano na walibebana kwenye pikipiki mbili ambapo
majambazi watatu walipanda pikipiki moja huku wengine wawili wakiwa wamepanda
nyingine.
Alisema Jeshi la Polisi
lilipata taarifa ya kiinterensia na kufanikiwa kujipanga ili kukabiliana na
majambazi hao ambapo katika majibizano ya risasi jambazi mmoja aliyejulikana
kwa jina moja la Baraka anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 35 – 38 mkazi wa Makongolosi na fundi ujenzi aliuawa kwa kupigwa risasi tumboni na
mgiuuni.
Alisema marehemu baada ya kukaguliwa
alikutwa na silaha aina ya SMG yenye
namba 1996 AFU 1120 ikiwa na risasi 26 kwenye magazine,na kwamba majambazi
wengine wanne walifanikiwa kukimbia kuelekea Kijiji cha Matondo na ndipo askari
waliendesha msako kuwatafuta.
Alisema baada ya majambazi
kuwaona askari waliwasha pikipiki zao kwa nia ya kukimbia huku wakirusha risasi
ovyo ndipo Polisi walijibu mapigo na kufanikiwa kuwaua majambazi wawili na
kukamata pikipiki moja yenye namba za usajili MC 761 AFS aina ya Sanlg
iliyokuwa ikitumiwa na majambazi hao pamoja na Begi moja lenye tochi na Panga..
Alisema majambazi wengine
wawili walifanikiwa kukimbilia kusiko julikana ambapo Jeshi la Polisi
linaendelea na msako mkali likishirikiana na wananchi ili kuwakamata
waliotoroka na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya
ya Chunya.
Aliongeza kuwa majina ya miili
ya majambazi wawili hayajafahamika ambapo alitoa wito kwa wananchi kufika
katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kuwatambua ikiwa ni pamoja na kuchukua
miili yao baada ya kufuata utaratibu baada ya kuwatambua kwa ajili ya kuwazika
kutokana na Hospitali hiyo kukabiliana na changamoto ya Chumba cha kuhifadhia
maiti.
Aidha Kaimu Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Mbeya, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Butusyo Mwambelo anatoa wito kwa
wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri
ili kuzuia vitendo vya kihalifu mapema kabla ya kutokea.
|
No comments:
Post a Comment