Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, April 28, 2016

MKUU WA MKOA WA MBEYA AMOS MAKALLA AZINDUA MRADI WA UIMARISHAJI WA MIFUMO YA SEKTA ZA UMMA(PS3)

Mkurugenzi wa Mradi wa PS3 Dk. Emmanuel Malangalila akitoa taarifa ya Mradi huo katika hafla ya uzinduzi wa Mradi iliyofanyika katika ukumbi wa Royal Tughimbe jijini Mbeya.

Mratibu wa Mradi wa PS3 Beatha Swai akieleza malengo na matarajio ya mradi huokwa Halmashauri za Mkoa wa Mbeya

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma uliozinduliwa kimkoa jijini Mbeya

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) Shanon Young akitoa neno katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa PS3 ambao umedhaminiwa na Serikali ya Marekani

Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja (aliyesimama) akitoa utambulisho wa wageni katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa PS3


Wakuu wa Idara na viongozi mbali mbali wakifuatilia shughuli za uzinduzi wa Mradi katika ukumbiwa Tughimbe Mafiati jijini Mbeya

Mkuu wa Wilaya ya  Mbeya, Nyerembe Munasa akitoa neno la shukrani baada ya hotuba ya mgeni rasmi

Viongozi wakiwa katika picha ya pamoja

Viongozi wakiagana

Washiriki wakiwa kwenye ukumbi wa Mikutano
 
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla amesema uimarishwaji wa mifumo ya sekta za Umma nchini utasaidia kuondoa tatizo sugu la watumishi hewa endapo utekelezaji wake utafanyika vizuri.
 
Makalla aliyasema hayo  alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Mradi wa Uimarishaji mifumo ya Sekta za Umma mkoani Mbeya uliofadhiliwa na shirika la Msaada la Marekani (USAID) katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Royal Tughimbe jijini Mbeya.
 
Mkuu huyo wa Mkoa alisema Mradi huo umekuja katika kipindi muafaka ambacho serikali ya awamu ya tano inajitahidi kuhakikisha inahimiza na kurekebisha iliyokuwepo katika Sekta za Umma ili kurahisisha utoaji huduma bora kwa wananchi.
 
Alisema Mradi huo utasaidia kuweka mfumo mzuri ambao utaondoa kabisa tatizo la watumishi hewa katika taasisi za umma na kuboresha mfumo wa utendaji kwa watumishi kutimiza wajibu wao kwa kiwango chenye ubora na wakati unaostahili.
 
Awali akisoma taarifa katika uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Mradi, Dk. Emmanuel Malangalila alisema mradi huo utahakikisha mifumo iliyopo katika ngazi ya Halmashauri inaimarishwa kupitia kitita cha afua zilizoundwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi wa Tanzania.
 
Dk. Malangalila alisema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka mitano kuanzia 2015 hadi 2020 ambapo mafanikio yanategemewa kutokea kwenye sekta ya Utawala bora na ushirikishwaji wa raia ambapo Rasilimali za taifa zitatumika kwa uwazi, kuwawezesha ushiriki wa wananchi katika kupanga, kufuatilia na kutoa matokeo katika kila sekta.
 
Alisema mafanikio mengine ni kuongezeka kwa usawa katika mgawanyo wa rasilimali watu kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwenye maeneo yenye uhitaji zaidi, kuimarisha mfumo wa ajira pamoja na kudumu kwa watumishi katika ajira serikalini.
 
Aliongeza kuwa mradi huo pia utasaidia ongezeko la pato la ndani kwa ajili ya huduma za umma, kuongezeka kwa ufanisi katika matumizi ya fedha za umma pamoja na kuongeza uwiano kati ya kiasi cha fedha kilichotumika na mali iliyonunuliwa jambo ambalo litapunguza hati chafu na zenye mashaka kwenye halmashauri.
 
Dk. Malangalila alisema kuimarishwa kwa mifumo ya utoaji taarifa iliyopo nchini pamoja na matumizi ya takwimu kwa wadau utasaidia kutokuwa na takwimu za kutengenezwa ambapo pia Mradi huo utasaidia katika tafiti tendaji zitakazosaidia mradi kujua changamoto na mikakati  ya kuzishughulikia changamoto hizo.
 
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi huo kutoka Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi, Beatha Swai alisema Mradi huo unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania Bara ambayo ni Iringa, Dodoma, Kagera, Kigoma,Lindi, Mara,Mbeya, Morogoro, Mtwara,Mwanza, Njombe, Rukwa na Shinyanga.
 
Alisema uzinduzi wa mradi huo umeshafanyika katika Mikoa ya Iringa, Shinyanga, Dodoma na Morogoro huku Mikoa ya Mtwara, Mwanza na Mbeya ikizindua kwa pamoja ambapo alisema mategemeo ya Wizara ni kuwa mradi huo utasaidia kuwajengea uwezo watumishi wa Halmashauri katika utekelezaji wa majukumu yao.
 

No comments: