Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Friday, January 15, 2016

WAKULIMA WA TUMBAKU WAOKOA MAMILIONI YA SHILINGI KWA KUJENGA DARAJA KWA NGUVU ZAO.




Mmoja wa Wanachama wa TAJATI Rashid Mkwinda akishiriki katika ujenzi la daraja la Mto Lupa ambalo wananchi wameokoa mamilioni ya fedha kwa kujitolea nguvu zao daraja ambalo limejengwa na wakulima wa Chama cha Msingi cha Igangwe Amcos katika Kata ya Mtanila wilayani Chunya.


Wanachama wa TAJATI  wakishiriki katika ujenzi la daraja la Mto Lupa wakishirikiana na  wakulima wa Chama cha Msingi cha Igangwe Amcos katika Kata ya Mtanila wilayani Chunya.

Wakulima wakivuka katika daraja la Mto Lupa baada ya ujenzi wake kukamilika

WanaTAJATI wakivuka katika daraja baada ya kushiriki ujenzi wake uliofanyika katika kijiji cha Igangwe Kata ya Mtanila Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya

Muonekano wa daraja baada ya ujenzi wake kukamilika

Daraja likiwa tayari kwa matumizi ya binadamu kwa ajili ya kuvushia Tumbaku baada ya mavuno

ILI kukabliana na vifo vinavyotokana na wananchi  kusombwa na maji katika wilaya ya Chunya, ufumbuzi umepatikana baada ya wakulima wa zao la tumbaku  wa Kijiji cha Igangwe Kata ya Mtanila kujitolea kujenga daraja kwa fedha zao na nguvu kazi ili kuepuka madhara makubwa waliyokuwa yakikabiliana nayo kipindi cha masika.

Wakulima hao kutoka chama cha Msingi cha Igangwe Amcos wamejenga daraja linalounganisha kijiji cha Igangwe na Vitongoji vya Shauri Moyo na Mtukula ili kurahisisha usafiri kwa wanafunzi na wakulima wa Tumbaku kuelekea kwenye mashamba yao.

Akizungumza na Waandishi wa Chama cha Waandishi wa habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania(TAJATI) waliotembelea kijijini hapo na kushiriki ujenzi huo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igangwe Lwitiko Mwambegele alisema kabla ya kujengwa kwa daraja hilo wakulima wengi wamepoteza maisha kutokana na kusombwa na maji wakiwemo wanafunzi.

Mwambegele alisema wakulima wengi hutumia usafiri wa baiskeli na pikipiki kwenda mashambani hivyo mara nyingi walikuwa wakipata ajali mara wavukapo mto Lupa na kupelekea kupoteza maisha jambo waliloona ni vema kuchangishana na kujenga daraja imara.

“Wakulima wengi wamepoteza maisha kwa kuangukua mtoni na kusombwa na maji na watoto wete wadogo ambao ni wanafunzi lakini tukaona hatuwezi kuisubiri serikali ije itujengee na tukaamua tuchangishane shilingi 20,000 kila mkulima ili kufanikisha zoezi hili ambalo hadi sasa tumekamilisha kwa asilimia 95.

Alisema jumla ya shilingi Milioni 2.5 zilipatikana ambazo zimesaidia kuchana mbao na kusomba kupeleka eneo la mradi pamoja na ununuaji wa misumari na nguvu za wananchi zimetumika kwa asilimia kubwa zaidi na vitendea kazi ambapo jumla ya mbao 313 zilichanwa na kutumika.

Kwa upande wao baadhi ya wakulima walioshiriki ujenzi huo walisema zoezi hilo limetumia muda wa mwezi mmoja kutokana na michango kusua sua lakini kazi iliyofanyika imeokoa fedha nyingi tofauti na serikali kama ingemuweka mkandarasi.

Makamu Mwenyekiti wa TAJATI, Christopher Nyenyembe aliwapongeza wananchi hao kwa kujitolea katika kazi za maendeleo na kwamba ni mfano wa kuigwa badala ya kuitegemea serikali kwa kila jambo hata kama wao wanauwezo nalo.

Alisema ni vema wakulima hao wakaendelea kuainisha maeneo mengine kwa kuyafanyia kazi ambapo Serikali itaona aibu na kuamua kuchangia na kusaidia nguvu za wananchi pindi wanapokwama kukamilisha miradi waliyoinza.

“Kwa kutazama ujenzi wa daraja hili lenye urefu zaidi ya mita 100 kama lingekuwa mikononi mwa mkandarasi nadhani zaidi ya Sh milioni 200 zingetumika,wananchi wamefanya kazi kubwa sana nay a ajabu” alisema Nyenyembe.

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Sophia Kumbuli, alionyesha kushangazwa na kitendo cha Wananchi hao kujenga daraja hilo na kuongeza kuwa wameisadia Serikali kwa kiwango kikubwa na kuokoa fedha nyingi ambazo makadirio ya wataalam mradi huo ungekuwa wa mamilioni ya fedha.

“Nawahakikishia lazima niende nikajionee daraja hilo mimi mwenyewe ikiwa ni pamoja na kuwaongezea nguvu kwani daraja naliona ni kubwa na kugharimu milioni mbili tu, hizo ni fedha ndogo kuna kadaraja mkandarasi amekajenda hapo jirani kamegharimu zaidi ya milioni 60 hivyo wameokoa mamilioni ya shilingi nawapongeza sana” alisema Mkurugenzi huyo.

No comments: