Mwenyekiti wa Shirikisho la Wasomi Mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu kiongozi anayekubalika katika jamii. |
Viongozi wa Mashirikisho wakiwa kwenye mkutano na waandishi wa habari. |
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa kwenye mkutano na wenyeviti wa Mashirikisho Mkoa wa Mbeya. |
ZIKIWA zimebaki siku mbili kuelekea uchaguzi mkuu wa
Tanzania, Shirikisho la Vyama vya siasa na Shirikisho la Wasomi Mkoa wa Mbeya
kwa pamoja wamesema wanamuunga mkono mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha
Mapinduzi (CCM) Dk. John Magufuli kwa madai kuwa ni mtendaji mzuri.
Wakizungumza katika mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Mbeya Peak, Viongozi
wa mashirikisho hayo walisema Dk. Magufuli anakipaji cha utendaji sio wa
kufundishwa ni tofauti na wagombea wengine.
Mwenyekiti wa Shirikisho la
Wasomi Mkoa wa Mbeya, Prince Mwaihojo, alisema Dk. Magufuli anaweza kukemea
jambo baya linapotokea na sio mtu wa kusubiri maovu yakatendeka na kwamba
utendaji wake amezaliwa nao.
Alisema Wagombea wengine
wanahubiri siasa za mitaani ambazo haziwezi kuwasaidia watanzania kwa ujumla
kwani wamejikita zaidi kwenye kundi la Boda boda lengo lao likiwa ni kuwatumia
katika vurugu kwani wanajua hawawezi kushinda katika uchaguzi huo.
Alisema hivi sasa Watanzania
wanapaswa kumuangalia mtu anayeweza kuwaongoza na sio kuangalia Chama
anachotoka ndiyo maana Shirikisho hilo limeanzisha msemo wa “Mbeya kwanza vyama baadaye” ili kumpata kiongozi anayefaa bila
kujali itikadi yake.
“Sisi Wasomi wa Mkoa wa Mbeya
tumeona tusimamie kwenye mtu anayefaa kwa maslahi ya Watanzania wote bila
kujali chama anachotokea hivyo tunamuunga Mkono Dk. Magufuli kwa kuwa ni
mtendaji mzuri mwenye kipaji na mwenye uwezo wa kutatua changamoto katika jamii”
alisema Mwaihojo.
Alisema wagombea wengine
wanashindwa kusimamia kauli wanazotoa badala yake wamekuwa vigeu geu kwa
kushindwa kukumbuka kile walichokiongea mbele ya hadhara na badala yake
wamekuwa wakitoa kauli zinazokinzana.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Shirikisho la Vyama vya siasa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti wa APPT Maendeleo Mkoa wa Mbeya, Godfrey
Mwandulusya, ametoa wito kwa vijana kutokubali kutumiwa vibaya na baadhi ya
viongozi wa siasa katika kulinda kura jambo ambalo ni kinyume cha sheria za
uchaguzi.
Alisema kitendo hicho kinaashiria vurugu na
kuharibu taswira ya uchaguzi na kwamba maagizo ya Tume ya uchaguzi ya kuwataka
wapiga kura kusimama mita 200 yako sahihi kwa
kuwa sheria mama inatamka wazi kuwa kusanyiko lolote la kuanzia watu
watatu ni kosa kisheria.
Alisema ni vema wakazi wa Mbeya
wakaheshimu maagizo ya Tume kwa kupiga kura kasha kurudi nyumbani kwa kuwa
vyama vya siasa vitaweka mawakala wao ambao jukumu lao ni kulinda kura wakati
wa uchaguzi.
Aliongeza kuwa vurugu
zinazotokea Mkoa wa Mbeya zinakosesha fursa za ajira na kukimbia kwa wawekezaji
kwenye sekta za viwanda hivyo ni vema vijana wakakataa kutumiwa na baadhi ya
viongozi kwa manufaa yao binafsi.
“ Shirikisho la vyama vya siasa
Mkoa wa Mbeya nje ya Ukawa inawataka vijana kupiga kura na kurudi nyumbani, hao
wagombea wanaowataka walinde kura wao watakuwa wapi kuzilinda hizo kura zao
hadi wawaachie vijana? Hawaoni kama wanawatumia kutaka kuleta vurugu” alihoji
Mwandulusya.
No comments:
Post a Comment