Hakimu
Mwakalinga siku alipohukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe. Leo amehukumiwa tena
kunyongwa mpaka kufa katika mauaji ya mlemavu wa ngozi Henry Mwakajila.
MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Mbeya leo hii imewahukumu kunyongwa mpaka kufa watu wanne
kati ya watano waliomuua Henry Mwakajila (17) ambaye ni mlemavu wa ngozi
(albino).
Waliohukumiwa
kunyongwa mpaka kufa ni Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au
Mwakatoga na Gerard Korosso Kalonge (wakazi wa Kijiji cha Mbembati
wilayani Ileje), na Leonard Msalage Mwakisole na Hakimu Mselem
Mwakalinga (wakazi wa Kiwira wilayani Rungwe).
Mshtakiwa
wa nne, Mawazo Philemon Figomole, ameachiliwa huru na mahakama hiyo
baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasi na
shaka kwamba alihusika katika mauaji hayo.
Akisoma
hukumu ya kesi hiyo ya mauaji yenye kumbukumbu Namb. KIW/IR/49/2008 na
PI 5/2013, Jaji wa Mahakama Kuu Dk. Revila, amesema mahakama
imejiridhisha pasi na shaka na ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba
washtakiwa hao wanne walitenda kosa hilo na hivyo wanastahili adhabu
hiyo.
Hii ni
kesi ya saba ya mauaji ya albino kutolewa hukumu ambapo mpaka sasa jumla
ya watuhumiwa 15 wamehukumiwa kunyongwa mpaka kufa. Ililezwa mahakamani
hapo kwamba, mnamo Februari 5, 2008 majira ya saa 12:00 na saa 1:00
jioni huko katika Kijiji cha Ilolo, Kata ya Kiwira, tarafa ya Ukukwe,
wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya, washtakiwa hao walimteka nyara
kijana Henry Mwakajila, ambaye ni mlemavu wa ngozi aliyekuwa akisoma
kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ukukwe na kisha kumuua.
Wakati wa
mwenendo wa kesi, ilielezwa na mashahidi wa upande wa mashtaka kwamba
mshtakiwa wa kwanza Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga
ambaye ni mganga wa jadi, mkazi wa Kijiji cha Mbembati, Wilaya ya
Ileje, alikutwa na utumbo unaodhaniwa kuwa wa binadamu na ulipopelekwa
kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ukathibitika kwamba ni utumbo wa marehemu
Henry.(VICTOR)
Mshtakiwa
wa pili, Gerard Korosso Kalonge wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje
alikutwa na vidole vinne na mifupa kumi (10) vyote vinavyodhaniwa kuwa
vya binadamu na baada ya uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali ilibainika
kwamba ni viungo vya marehemu Henry Mwakajila.
Ilielezwa
pia kwamba, washtakiwa Leonard Msalage Mwakisole, Mawazo Philemon
Figomole na Hakimu Mselem Mwakalinga ndio waliodaiwa kumteka nyara mtoto
huyo na kumuua, kisha kupeleka viungo kwa mganga wa kienyeji
Asangalwisye Kayuni.
Mshtakiwa
wa tano, Hakimu Mselem Mwakalinga, tayari alikwishahukumiwa kunyongwa
katika kesi nyingine ya mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya
Rungwe, John Mwankenja, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani
kwake. Hukumu ya kesi hiyo namba 131/2012 ilitolewa Novemba 13, 2013
ambapo inaelezwa kwamba watuhumiwa walitenda kosa hilo Mei 19, 2011
katika kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani
Mbeya.
Ingawa
watuhumiwa walikuwa wanne, lakini Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya chini ya
Jaji Samwel Karua iliwahukumu kunyongwa mpaka kufa mshtakiwa wa kwanza
Hakimu Mwakalinga na mshtakiwa wa pili Daudi Mwasipasa kwa maelezo
kwamba walihusika moja kwa moja na mauaji hayo ya kukusudia.
Mshtakiwa
namba tatu Obote Mwanyingili yeye alitiwa hatiani kutokana na kosa la
kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji wakati
mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela alitiwa hatiani kutokana na kuhifadhi
silaha iliyotumika katika mauaji hayo ingawa hakusika na kitendo hicho
moja kwa moja, hivyo wote wawili walihukumiwa kifungo cha miaka saba
jela.
Hata hivyo, Myovela tayari alikwishahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa na silaha kinyume cha sheria.
Inadaiwa
kwamba, chanzo cha mauaji hayo ya John Mwankenja, ambaye pia alikuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Rungwe, kilitokana na
kiongozi huyo kufahamu kwamba hao ndio waliomuua mlemavu wa ngozi Henry
Mwakajila, hivyo aliuawa ili kupoteza ushahidi
CHANZO:www.brotherdanny.com
1 comment:
SAAAFI SANA HUYO HAKIMU ANAYETOA HIZI HUKUMU<NINGEWEZA NINGEMPA HATA ZAWADI<ILIMRADI USHAHIDI UPO WA KUTOSHAHAINA HAJA YA KUWAFUNGA NA KUPOTEZA PESA ZA WALIPA KODI KUWALISHA HUKO JELA NA WAO WAONJE UCHUNGU WAKE, NA IWE FUNDISHO KWA YEYOTE ANAYESHURIKI VITENDO HIVI VYA KINYAMA
Post a Comment