Mwenyekiti wa Umoja wa vijana UVCCM Mkoa wa Mbeya Amani Kajuna akiwa meza kuu wakipiga makofi pamoja na viongozi wengine.
Katibu Wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Mbeya, Bi Khadija akiwasalimia wananchi wa Kata ya Sogea katika mji mdogo wa Tunduma.
Mwenyekiti wa Umoja wa vijana UVCCM Mkoa wa Mbeya Amani Kajuna akihutubia wananchi wa Tunduma kwenye mkutano wa hadhara.
Awilo kidume cha Mbeya akitoa burudani.
Makhirikhiri wakitumbuiza.
Wakazi wa Tunduma wakisikiliza kwa makini.
Wakazi na wanachama wa ccm wakifuatilia kwa makini na kushangilia katika mkutano wa hadhara.
WAKAZI wa Mji mdogo wa Tunduma wilayani Momba Mkoa wa Mbeya
wametakiwa kuutunza mji huo kama kitovu cha biashara kwa Mkoa wa Mbeya na mpaka
unaotegemewa na nchi jirani.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Mkoa
wa Mbeya, Amani Kajuna alipokuwa akihutubia vijana na wananchi wa Mji wa
Tunduma katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa na Kata ya Sogea.
Kajuna alisema Wakazi wa Tunduma wamekuwa wakikubali kutumika
katika vurugu za kisiasa na kufanya maandamano ambayo yanapelekea kuvunjika kwa
amani katika mji huo na kusababisha kuyumba kwa uchumi na mzunguko wa
kibiashara kwa ujumla kwa Mkoa wa Mbeya na Taifa kwa jumla.
Alisema hivi sasa idadi ya magari na wafanyabiashara katika mji
huo inazidi kupungua siku hadi siku na kuhamia sehemu zingine kuwekeza kutokana
na vitendo vya vurugu ambazo husababishwa na wanasiasa bila kujali anayeumia ni
nani.
“Hivi sasa hakuna mzunguko mzuri wa fedha, wafanyabiashara wakubwa
wamekimbioa idadi ya magari yanayovuka katika huu mpaka imepungua kutokana na
vurugu zenu vijana ambao mnanyweshwa viloba na kuanza kuandamana mnaharibu mji
wenu wenyewe acheni” alisihi Kajuna.
Aliongeza kuwa Mpaka wa Tunduma ni mkubwa kuliko yote nchini na ni
kitovu cha uchumi cha Mkoa na Taifa hivyo kitendo cha kuendekeza
vurugu zisizo kuwa na msingi zinasababisha kudorora kwa shughuli za uzalishaji
na kupelekea wageni na wawekezaji kukimbia.
Kajuna alienda mbali zaidi na kuwataka Wakazi wa Tunduma kutumia
maandamano kuwashinikiza viongozi wa Serikali za Mitaa na Mbunge wao David
Silinde kuwasomea mapato na matumizi ya fedha wanazochangishwa kwa ajili ya
shughuli za maendeleo.
Alitoa kauli hiyo kufuatia Mbunge wa jimbo hilo kutuhumiwa
kukumbatia fedha za mfuko wa jimbo Milioni 46 bila kuzipeleka katika shughuli
za maendeleo ya wananchi na kutatua matatizo yao ikiwemo kero ya maji
inayoukabili mji huo kwa muda mrefu.
Alisema Umoja wa Vijana wa CCM unampa siku tatu Mbunge huyo awe
amefika Jimboni kwake na kuziwasilisha fedha hizo vinginevyo atachukuliwa hatua
za kisheria za kufuja fedha za maendeleo ya wananchi na kuzitumia kwa maslahi
binafsi ambapo pia Mbunge huyo inasemekana fedha hizo ametenga ili azitumie
kwenye kampeni katika uchaguzi mkuu ujao.
Mbali na tuhuma hizo Mbunge Silinde pia anatuhumiwa kumiliki
miradi ya maji ya wananchi na kugeuza kuwa mradi binafsi na kuwatoza fedha
pindi wanapotaka kupata huduma ya maji katika visima viwili vilivyochimbwa
mjini hapo.
Wakizungumza mbele ya Mwenyekiti huyo, Wakazi wa Mji wa Tunduma
walisema kutokana na kero ya maji ambayo inawakabili wakazi hao walikubaliana
kuitisha harambee na kuchanga ili kuchimba visima jambo ambalo lilifanikiwa na
kupata zaidi ya shilingi Milioni 21 ambazo alikabidhiwa Mbunge Silinde.
Walisema baada ya hapo Visima viwili vilichimbwa lakini katika
hali isiyokuwa ya kawaida visima hivyo vikaandikwa mradi binafsi wa mbunge
hivyo kusababisha watu wanaotaka huduma ya maji kuuziwa na fedha kuzichukua
yeye kwa shughuli zake binafsi.
Na Mbeya Yetu
No comments:
Post a Comment