Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Monday, March 2, 2015

WASOMI VYUO VIKUU WAILILIA TUME YA UCHAGUZI, WAITAKA IWAPENDELEE WAKATI WA KUPIGA KURA.

  Afisa  Elimu ya mpiga kura na Elimu kwa umma kutoka tume ya Uchaguzi(NEC), Salvatory Alute akitoa mada kwenye mdahalo wa Vyuo vikuu Mbeya.

Joseph Mallya kutoka Idara ya daftari la kudumu la mpiga kura akiwasilisha mada yake kwenye mdahalo wa wanafunzi kutoka vyuo vikuu Mbeya uliofanyika katika ukumbi wa TEKU.

Baadhi ya waratibu wa mdahalo huo wakichukua dondoo.

Walimu wa TEKU wakifuatilia hoja mbali mbali katika mdahalo.


Washiriki wa mdahalo huo kutoka vyuo mbali mbali vya Mkoa wa Mbeya wakifuatilia kwa makini.





WAKATI zoezi la uandikishaji wa Wapiga kura katika daftari la Kudumu likiwa limeanza Makambako  Mkoani Njombe, Wasomi wa Vyuo vikuu Mkoa wa Mbeya wameonesha hofu ya kushiriki uchaguzi mkuu ujao.

Wakizungumza na kwenye mdahalo wa vyuo vikuu uliofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Chuo kikuu cha Teofilo Kisanji(TEKU) ulioandaliwa na Chama cha walimu wanaofundisha masomo ya Siasa(CETA), walisema ratiba ya uchaguzi si rafiki kwa wanafunzi.

Nurdin Makoni, Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa  TEKU alisema masharti yaliyowekwa na Tume ya uchaguzi kwamba ni lazima kila mtu apige kura katika eneo alilojiandikishia linawabagua wanafunzi kutokana na muda wa uchaguzi kuwa eneo tofauti na alipojiandikishia.

Alisema asilimia kubwa ya wanafunzi hujiandikisha aidha akiwa chuoni ama nyumbani lakini siku ya uchaguzi huenda akawa sehemu tofauti na alipojiandikishia jambo ambalo linamnyima haki yake ya kupiga kura na kuchagua viongozi.

Frank David mwanafunzi wa Chuo kikuu Mzumbe alisema miaka mingi ya uchaguzi idadi ya wapiga kura inakuwa hairidhishi kutokana na kuwabagua vijana kwa sababu ya ratiba ambayo si rafiki kwa wanafunzi walioko vyuoni ambao ndiyo wengi zaidi kuliko watu wengine.

Alisema Tume inapaswa kuwa wazi kwa vijana  na wanafunzi walioko mashuleni ili wawe huru kuchagua viongozi wao kwa kuweka ratiba na maeneo ambayo wanapaswa kupigia kura katika uchaguzi mkuu ujao na kutopoteza haki yao.

Naye Frida Kitika kutoka Chuo cha Maendeleo ya Jamii alisema ni vema wanafunzi wakapewa uhuru wa kupiga kura sehemu yoyote watakapo kuwepo ili wasiwanyime haki ya kuchagua viongozi wao kutokana na mazingira wanayoishi kuwa si ya kudumu.

Alisema Changamoto nyingine inatokana na wengi wao kutofikisha umri wa miaka 18 kabla ya kuanza chuo lakini hufanikiwa kufikisha miaka inayotakiwa tayari akiwa ameanza masomo hivyo kusababisha kukosa sifa ya kuchagua viongozi wake.

Wanafunzi hao walishauri kuwa endapo tume itaendelea kusimamia msimamo wake ni bora wanafunzi wakawekewa utaratibu wa kumchagua Rais kwa kuwa ni kiongozi wa kitaifa tofauti na Wabunge na madiwani ambao wanapaswa kuchaguliwa na wakazi wa eneo husika.

Kwa upande wake Afisa Elimu ya mpiga kura  na elimu kwa umma kutoka tume ya uchaguzi, Salvatory Alute,alisema ni vema vijana wakajitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu bila kuhofia ni wapi watakapokuwepo siku ya uchagfuzi.

Alisema zoezi la kujiandikisha ni muhimu kutokana na kutolewa vitambulisho vipya tofauti na ambavyo tayari vipo kwa walioandikishwa zamani na kushiriki chaguzi zilizopita.

Alisema Tume imejipanga kuhakikisha zoezi la uandikishaji linafanyika katika kipindi kifupi kutokana na vituo kuongezwa kutoka vituo 23000 hadi vituo 40000 smbsvyo vitakuwepo kila kijiji ili kurahisisha wananchi wengi kujiandikisha.

Alisema Serikali imetoa vifaa zaidi ya 8000 ambavyo Tume itakuwa ikivitumia ambapo itafanya mtindo wa kuhama kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine na kutoruhusi zoezi hilo kuendeshwa kila sehemu hivyo kila Wilaya Daftari litakuwepo kwa siku 28.

Aliongeza kuwa mfumo utakaotumika kuandikishia ni wa kisasa unaojulikana kwa jina la BVR ambao umeonesha mafanikio makubwa katika nchi za Kenya na Ghana hivyo Tume inatarajia kuandikisha watu zaidi ya Milioni 22.

Katika mdahalo huo zaidi ya wanafunzxi 100 walihudhuri kutoka vyuo vilivyo na matawi Mbeya ambavyo ni Mzumbe, Iringa, Chuo kikuu kishirki(OUT), TIA, MUST,, VETA, St. John Nursing, Dar cit college, Tanzania social studies, TEKU, Maendeleo ya Jamii, CBE, SAUT na Chuo cha Kilimo Uyole.

Mwisho.
Na Mbeya yetu

No comments: