HATIMAYE uzinduzi wa Filamu ya Black Valentine
iliyoigizwa na wasanii kutoka jijini Mbeya imezinduliwa rasmi na kuingizwa
sokoni.
Uzinduzi wa Filamu hiyo ulifanyika katika ukumbi
wa Mtenda Sunset iliyopo Soweto jijini Mbeya ukisindikizwa na burudani kabambe
kutoka kwa wasanii nguli wa filamu na mziki wa taarabu kutoka Dar es salaam.
Wasanii hao ni pamoja na Charles Magari kutoka
Bongo Movie, mwimbaji mahiri wa mziki wa taarabu Omari Tego sambamba na wasanii
mbali mbali kutoka jijini Mbeya wakiongozwa na wanafunzi kutoka Vyuo vikuu vya
Teku, Tia, Ilemi na Tumaini Makumira Mbeya.
Akizungumza katika sherehe hizo, Msanii Charles
Magari aliwataka Wazazi na walezi kuvithamini vipaji vya vijana
wao hususani wanaoingia katika tasnia ya filamu kwa kuwaruhusu kwa kile
kilichodaiwa ni sawa na kazi nyingine inayoweza kumuingizia kipato.
Magari alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya
wazazi kuwakatalia watoto wao kujiunga na kazi ya sanaa kutokana na mtazamo
hasi kwamba kazi ya sanaa ni ya kihuni jambo ambalo ni kinyume kabisa.
Alisema kazi ya sanaa husaidia kuleta ajira na
kumuingizia kipato msanii kama zilivyo kazi zingine hivyo kuharibika kwa tabia
ya mtoto kunatokana na malezi aliyoyapata tangu awali kutoka kwa wazazi wake.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi wa
filamu hiyo, Charles Mwakipesile, aliwapongeza wasanii kutoka Mkoa wa Mbeya kwa
kuonesha vipaji na kuongeza kuwa eneo hilo linapaswa kuangaliwa na kuthaminiwa.
Alisema Mkoa wa Mbeya pekee unawasanii wengi
lakini wameshindwa kuonesha uwezo wao kutokana na jamii kutowatia nguvu kwa
kusaidia kununua kazi zao ili waweze kuinuka kiuchumi.
Mwakipesile alisema kazi ya sanaa kwa kiasi
kikubwa imechangia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ambao kwa sasa wengi
wao wamejikita kwenye filamu na mziki hivyo kutokuwa na vijana wanaozurura
mitaani.
Aidha alimpongeza Mkurugenzi wa Shule ya
Sekondari ya Vanessa iliyopo Isyesye jijini Mbeya, Shukrani Gidion, kwa
kuanzisha utaratibu wa kufundisha sanaa kwa wanafunzi wake tangu wakiwa shule.
Alisema kitendo hicho alichokifanya Vanessa
kinasaidia wahitimu baada ya kumaliza masomo kuwa na shughuli ya kufanya pamoja
na kujitegemea kutokana na kuwa na ufahamu wa sanaa alioupata akiwa
shule.
Hata hivyo katika filamu ya Black Valentine
asilimia kubwa ya wahusika ni wanafunzi na wahitimu wa shule ya Sekondari
Vanessa.
Kwa upande wake Mwandaaji wa Filamu ya Black
Valentine, Yekonia Watson maarufu kwa jina la Aman, alitoa wito kwa Wakazi wa
Mkoa wa Mbeya kuacha kushabikia kazi za wasanii kutoka nje ya mikoa yao
Alisema katika filamu hiyo iliyotengenezwa na
Enea Production imebeba ujumbe mzito na unao eleza maana ya siku ya wapendanao
na uvaaji wa nguo nyeusi tofauti na ilivyozoeleka kwa watu wengi kuvaa mavazi
mekundu.
Mwisho.
|
No comments:
Post a Comment