Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Thursday, February 12, 2015

MWIGULU NCHEMBA AOMBWA KUGOMBEA URAIS UCHAGUZI UJAO.

Mchungaji Gasto Mwaihuti akisoma tamko la viongozi wa kiroho kwa waandishi wa habari.

Baadhi ya Wachungaji wakiwa katika Meza kuu kwa niaba ya viongozi wengine wa madhehebu ya dini ya kikristu katika mkutano na waandishi wa habari.

Wachungaji wakifuatilia kwa makini Mkutano na waandishi wa habari.

Baadhi ya waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya wakichukua maelezo kutoka kwa viongozi wa Kiroho kuhusu mgombea Urais wanayemtaka.

VIONGOZI wa madhehebu ya dini ya kikristu mkoani Mbeya wamemtaka Naibu Waziri wa Fedha na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba,kutokata tamaa ya kugombea Urais katika uchaguzi ujao.

Akisoma tamko kwa niaba ya viongozi wa dini Mkoa wa Mbeya, Mchungaji Gasto Mwaihuti,katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika katika Hoteli ya Suluti iliyopo Uyole jijini Mbeya, alisema viongozi wa Dini wanaunga mkono nchi kuongozwa na Vijana.

Mwaihuti alisema Viongozi wa kiroho kutoka Mkoa wa Mbeya ina unga mkono utafiti uliofanywa hivi karibuni na Asasi ya utafiti wa kielimu Tanzania (TEDRO) na kutoa majibu kuwa vijana ndiyo wenye uwezo wa kuongoza Nchi katika uchaguzi ujao na kukubalika zaidi katika jamii.

Alisema Viongozi wa dini wanamuunga mkono Mwigulu Nchemba kugombea urais katika uchaguzi ujao kutokana na maneno yake, utendaji kazi na historia yake ya kukemea hadharani Rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma sambamba na matumizi mabaya ya madaraka jambo linaloashiria kuwa ni kiongozi anayefaa kuliongoza taifa.

“Tunamtaka Mwigului Nchemba kutokata tamaa ya kugombea uraisi kwa sababu tunajua wazi kuwa kwa kauli yake alisimamia kidete kukemea kwa uwazi sakata la Escrow lililosababisha upotevu mkubwa wa fedha za wananchi na kupelekea wananchi kukosa imani na serikali yao” alifafanua Mchungaji huyo.

Alisema viongozi wa dini wanalazimika kufikia hatua hiyo kutokana na historia mbalimbali kuonesha jinsi vijana wenye umri mdogo wanavyoweza kufanya matendo makubwa akiwemo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye aliweza kusimamia mabadiliko makubwa katika kupigania taifa, upatikanaji wa uhuru wa Tanzania na mataifa mengine barani Afrika akiwa na umri mdogo.

Aliongeza kuwa hata katika maandiko matakatifu ya Biblia yanaonesha jinsi wadogo wanavyoweza kuwatawala wakubwa ambapo kwa umri alionao Mwigulu Nchemba kuwa ni mdogo lakini kwa kufuata maandiko hayo anaweza kuliongoza taifa hili endapo ataungwa mkono na wananchi kwa ujumla na kuthamini mchango wake katika kipindi hiki kifupi alichoongoza Wizara ya Fedha kama Naibu Waziri.

“ Maandiko matakatifu ya Biblia yanatuambia kuwa mdogo atamuongoza mkubwa kwa mfano Yakobo na Esau ambapo Yakobo alichukua nafasi ya Essau ambaye alikuwa Mkubwa, Mfalme Daudi ambaye alikuwa kijana mdogo shujaa, hodari na aliyekuwa amesahaulika katika watoto wa Yese ndiye aliyechukua nafasi ya ufalme licha ya udogo wake hivyo hata sisi viongozi wa kiroho Mbeya tunaona Mwigulu anafaa” alisisitiza Mchungaji Mwaihuti.

Sambamba na hilo Viongozi hao wa kiroho mkoani Mbeya waliwataka wananchi wote kuendelea kuliombea Taifa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu ili uwe wa amani na hatimaye kuwapata viongozi wenye hofu ya Mungu, asiyekuwa na ubaguzi wa kidini, kabila na zaidi wenye uwezo wa kuwaunganisha watu wote.

Aidha waliongeza kuwa Taifa la Tanzania linahitaji Kiongozi msafi asiyekuwa na chembe ya mashaka machoni mwa Watanzania ambaye atakuwa anachukia rushwa na kuikemea hadharani bila kuwaogopa hata marafiki zake.

“ Ni ukweli usiofichika kuwa taifa letu linapita katika majaribu makubwa mfano migogoro ya kidini, kukithiri kwa rushwa katika sekta mbali mbali na maeneo muhimu ya huduma za jamii, mmonyoo wa maadili kwa viongozi pamoja na kushuka kwa kiwango cha elimu hivyo tunawaomba watanzania wote kuomba kwa pamoja ili yote hayo yamalizwe kupitia uchaguzi ujao” walisema viongozi hao.

Mwisho.
Na Mbeya yetu

No comments: