Social Icons

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

bre

Monday, February 9, 2015

CHAMA CHA SANAA MBEYA(CHASAMBE) CHAPATA WALEZI WAPYA


Mwenyekiti wa Chama cha sanaa Jiji la Mbeya(Chasambe), Samwel Mwamboma akifuatilia jambo katika hafla ya kuwatambulisha walezi wapya wa chama hicho.

Katibu wa Chasambe, Ramadhan S. Ramadhan akisoma risala ya Chama hicho mbele ya walezi wapya katika hafla iliyofanyika Mbeya Hotel.



Msemaji wa Chasambe, Peter Mambala, akizungumza jambo katika hafla hiyo
.Kamanda wa Polisi Wilaya ya Mbeya mjini(OCD), Julius Mjengi akitoa nasaha zake kwa viongozi wa Chasambe pamoja na kukubali kuwa mlezi wao.


Mkurugenzi wa AJIM Enterprises ltd, James Mwampondele, akiwaeleza namna ya kujiinua na jinsi atakavyoshirikiana na Chasambe katika kuinua sanaa Mkoa wa Mbeya baada ya kukubali kuwa mlezi wao.


Mwenyekiti wa Wamiliki wa Mahotel mkoani Mbeya, Jeremiah Mahenge maarufu kwa jina la Vamponji akizungumza jambo katika hafla hiyo baada ya kuchaguliwa kuwa miongoni mwa walezi wa Chasambe.
.Mwakilishi wa Katibu tawala Mkoa wa Mbeya, Protas Mpogole akitoa salamu za Serikali.



Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Kastor Ngonyani akizungumza jambo na kukubali kumpelekea mapendekezo ya Chasambe Mkurugenzi Musa Zungiza.


Walezi na Viongozi wa Chama cha sanaa Jiji la Mbeya (CHASAMBE) wakibadilishana mawazo katika hafla hiyo.



WADAU wa Sanaa mkoani Mbeya wameishauri Serikali kuweka sheria kali ili kudhibiti kazi za wasanii kuuzwa kiholela madukani bila kuwepo kwa taarifa za wahusika ambao ndiyo wenye kazi.



Aidha wameshauri kuwa maduka yanayouza kazi za sanaa bila kuwa na vibali maalumu kutoka Basata pamoja na wezi wa kazi za wasanii adhabu iongezwe kuwa kali zaidi jambo litakalosaidia kukua kwa uchumi wa msanii mmoja mmoja pamoja na pato la Taifa.



Hayo yalibainishwa jana na Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja, Protas Mpogole, katika hafla iliyoandaliwa na  Chama cha Sanaa Jiji la Mbeya(CHASAMBE)kwa ajili ya kuwatambulisha walezi wapya wa Chama hicho iliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Mbeya.



Mpogole alisema pamoja na Chama hicho kuwaomba kuwa walezi bado ni jukumu la Serikali kuhakikisha kazi za sanaa zinaimarishwa hususani katika fani za michezo na utamaduni ili kukuza uchumi wa Nchi na msanii mmoja mmoja.



Alisema kazi za sanaa zinadharauriwa sana na kuibiwa kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa na utamaduni wa kuthamini shughuli zingine za michezo zaidi ya mpira wa miguu jambo linalochangia Serikali kuongeza juhudi za maksudi ili kuinua kazi za utamaduni.



Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu Jiji la Mbeya, Kastor Ngonyani aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Musa Zungiza katika hafla hiyo alisema Halmashauri ya Jiji la Mbeya linakubali kuwa mlezi wa Chama hicho kutokana na umuhimu wake katika kukuza ukuaji wa Halmashauri.



Ngonyani alisema kutokana na umuhimu wa sanaa katika kutoa ujumbe mbali mbali kwa jamii Halmashauri inavyo vitengo viwili ambavyo ni Idara ya Michezo pamoja na idara ya utamaduni ili kuhakikisha shughuli zote zinazohusu sanaa zinaimarika.



Alisema tangu awali kazi za sanaa ni chombo ambacho kilikuwa kikitumika katika kufikisha ujumbe wowote katika jamii tofauti na michezo mingine kama mpira wa miguu ambapo kupitia uigizaji ujumbe humfikia mlengwa moja kwa moja.



Naye Katibu wa Chasambe, Ramadhan Ramadhan alisema tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 2002 kimekuwa na mlezi mmoja ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Edna Mwaigomole hivyo kuona umuhimu wa kumuongezea nguvu kwa kuteua walezi wapya.



Aliwataja walezi wapya ambao kwa pamoja walikubali kuwa walezi wa Chama hicho kuwa ni pamoja na Kamanda wa Polisi Wilaya ya Mbeya Jiji(OCD)Julius Mjengi, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Musa Zungiza, Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariamu Mtunguja na  Mwenyekiti wa wamiliki wa Mahoteli Mkoa wa Mbeya, Jeremiah Mahenge(Vamponji).



Aliwataja wengine kuwa ni mfanyabiashara maarufu jijini Mbeya, James Mwampondele ambaye pia ni Mkurugenzi wa AJIM Enterprises ltd,ambao wataungana na Mlezi wa Aawali Edna Mwaigomole ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.



Mwisho.
Na Mbeya yetu

No comments: